Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Lindi Mhandisi Ephata Mlavi, akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wakati walipotembelea moja ya eneo korofi katika barabara ya Lindi – Dar es Salaam, sehemu ya Marendegu – Nangurukuru hadi Mbwemkuru (km 155), mkoani Lindi. Kazi za ukarabati wa barabara ya kutoka Lindi hadi Dar es Salaam kipande cha kilometa 2.5 zikiendelea, mkoani Lindi. Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wakitazama eneo ambalo mifereji ya maji itawekwa katika barabara ya Lindi – Dar es Salaam ili kukabiliana na maji mengi yanayoharibu miundombinu ya barabara hiyo kipindi cha mvua, mkoani Lindi. Muonekano wa sehemu ya eneo korofi ya barabara kipande cha kilometa 2.5 cha barabara ya Lindi – Dar es Salaam kinachoendelea kukarabatiwa ikiwa ni mwanzo wa utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli baada ya kukagua barabara hiyo na kutoridhishwa na hali yake.Mkurugenzi wa Barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Rogatius Mativila, akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wakati wa ukaguzi wa barabara ya Lindi – Dar es Salaam, sehemu ya Marendegu – Nangurukuru hadi Mbwemkuru (km 155), mkoani Lindi.

*************************************

Bodi ya Mfuko wa Barabara imesema imeridhishwa na utekelezaji wa ukarabati unaofanywa na Wakala wa Barabara katika barabara ya Malendegu – Nangurukuru hadi Mbwemkulu iliyokuwa imeharibika kabla ya msimu wa korosho na mvua nyingine kuanza.

Aidha, imeutaka wakala huo kuhakikisha wanazingatia ukarabati wa barabara zote nchini kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi.

Hayo ameyaeleza Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw. Joseph Haule, wakati wajumbe wa bodi walipopita kukagua barabara ya Dar es Salaam – Lindi -Mtwara ili kuona uharibifu uliojitokeza sambamba na kukagua maendeleo ya ukarabati wa maeneo yaliyoharibiwa na mvua.

“Hakikisheni mnakarabati barabara hii kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi kwani mvua zilizonyesha mwaka jana zinaweza kijirudia kipindi kingine na hivyo kuleta athari kubwa hivyo mzingatie uwekaji wa mitaro katika maneneo korofi yote”, amesema Bw. Haule.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa bodi inasubiria mapitio ya mapendekezo mapya katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2020/21 kutokana na changamoto zilizojitokeza katika mkoa huo na kubadilisha vipaumbele ili kuweza kuweka msisitzio au mkazo katika maeneo yenye matatizo makubwa.

“Kwa sababu mwaka wa fedha umeshaanza ni vizuri TANROADS kuangalia tena kama kuna mapendekezo ya bajeti juu ya suala hili kwa makini katika ukarabati wa ushoroba wa barabara hii ambayo iliathirika sana na sisi tutayapokea na kuyafanyia maaumzi haraka”, amesisitiza Bw. Haule.

Vilevile, Bodi hiyo imeridhishwa na hatua iliyofikiwa ya ukarabati huo na kuwahakikishia wakala huo kuwapa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha kipande kinachohitajika cha matengenezo chenye urefu wa kilometa 2.5 kinakamilika na baadae kukamilisha kilometa 30 zilizobakia katika sehemu hiyo.

“Kazi nzuri iliyoanza kufanyika na Meneja ameanza kazi kwa kasi inayotakiwa na kama ataendela hivi ni matarajio yetu ndani ya wiki mbili hadi tatu atamaliza kuziba mashimo yote na ndani ya miezi mitatu barabara nzima itakuwa imekamilika”, amefafanua Mwenyekiti huyo.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa ukarabati wa barabara hiyo, Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Lindi, Mhandisi Ephata Mlavi, ameeleza kuwa mpaka sasa hivi tumeshapata wakandarasi na wameshaanza kazi katika maeneo korofi yenye mashimo makubwa na katika maeneo ambayo lami ilikuwa imetoka ndani ya wiki mbili tutakuwa tumeshairudishia.

“Mkandarasi wa awali anaendelea na kazi na mkandarasi wa pili ameanza kuleta vifaa sehemu ya ujenzi wakati taratibu za mwisho zikiendelea kumpata makandarasi wa tatu ili kuharakisha matengenezo ya km 30 kabla ya mvua kuanza” amesema Mhandisi Mlavi.

Amebainisha kuwa tayari wamepokea fedha kutoka Mfuko wa Barabara na kasi ya ujenzi inaendelea mkandarasi wa awali anaendelea na sehemu iliyoharibika itafanyiwa ukarabati na makandarasi watatu kwa gharama ya bilioni 13.

Naye, Mkurugenzi wa Barabara kutoka Sekta ya Ujenzi ambaye ni mjumbe wa bodi hiyo, Mhandisi Rogatius Mativila, amesema kuwa serikali ilitumia bilioni 40 katika kukarabati maeneo yaliyoharibiwa na mvua katika mwaka wa fedha 2019/20 na hivyo Wizara itahakikisha inaweka sawa bajeti ya matengenezo ili kuhakikisha barabara zinakarabatiwa kwa wakati ili kuondoa usumbufu wa usafirishaji wa abiria na mizigo.

Mfuko wa Barabara (RFB), pamoja na majukumu mengine ni kuhakikisha kuwa shughuli za kiufundi na kifedha za Wakala wa Barabara na mfuko wenyewe zinafanyika kwa ufanisi mkubwa pamoja na kufuatilizia matumizi ya fedha zinazopelekwa katika miradi ya ujenzi na matengenezo ya barabara ili kuhakikisha kuwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na Mfuko.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...