Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imesema jumla ya akina Mama 219764 wamejifungulia kwenye Vituo vya Afya vipya 487 ambavyo vimejengwa ndani ya kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Dk John Magufuli.

Pia zaidi ya wazee laki moja wamepata huduma za kiafya kwenye vituo hivyo huku wanaume na wagonjwa wengine zaidi ya 6000 wakipata matibabu kwenye vituo hivyo.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo leo wakati akizindua wiki ya Tamisemi ambayo imelenga kueleza mafanikio yaliyopatikana kwenye Wizara hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.

Jafo amesema ndani ya siku tatu za wiki hii kuanzia leo Agosti 3 hadi 5 wataitumia kuwaeleza watanzania mafanikio ya miaka mitano ya maboresho ya huduma ya Afya ya Msingi, Mafanikio ya Elimu na Miundombinu.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Jafo amesema ni muhimu kama Wizara kuwaeleza watanzania namna ambavyo Serikali inayoongozwa na Rais Magufuli ilivyopiga hatua kubwa katika kuwahudumia wananchi wanyonge katika sekta ya Afya.

Amesema jumla ya Vituo vya Afya 487 vimejengwa ndani ya miaka mitano ikiwa ni mafanikio makubwa kwani Vituo vya Afya vya Afya vilivyojengwa vimeokoa idadi kubwa ya maisha ya watanzania waliokua wakifariki kwa kukosa huduma za afya.

" Ni mafanikio makubwa na sisi kama Tamisemi tuna kila sababu ya kumshukuru na kumpongeza Rais Magufuli kwa utendaji uliotukuka na wenye maono ambao leo unawafanya watanzania waliokua wakipata tabu ya Afya wafurahie matunda ya Nchi yao," Amesema Jafo.

Amesema siyo vituo vya afya tu hata ongezeko la Hospitali za Wilaya limekua ni kubwa katika kipindi hiki cha miaka mitano ya Rais Magufuli kwani zimejengwa Hospitali mpya 99 za Wilaya ambapo kabla zilikuepo 77.

" Huu ni muujiza ambao Rais wetu ametuonesha, kujenga Zahanati 1198 ndani ya miaka mitano pekee ni mafanikio ambayo tunapaswa tuyaseme bila kificho, hiki alichokifanya Rais ni ibada ameokoa maisha ya watanzania wanyonge ambao walikua wanateseka kufuata huduma za afya mbali," Amesema Jafo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk Binilith Mahenge akizungumza kwa niaba ya Wakuu wenzake wa Mikoa ameipongeza serikali kwa kuboresha miundombinu ya afya ambayo imekua msaada mkubwa kwa wananchi wanyonge hasa wa Vijijini.

" Mhe Waziri tufikishie salamu zetu kwa Rais Magufuli kwamba tumeona utendaji wake na tutakua mabalozi wa kuyasema yale yote makubwa aliyoyafanya kwenye Nchi hii, siyo kwenye Afya tu hata Elimu na Miundombinu kote huko tumeshuhudia mabadiliko makubwa ambayo hatujawahi kuyaona kwenye Nchi yetu," Amesema Dk Mahenge.
 Waziri w Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo akizungumza katika uzinduzi wa siku ya Tamisemi Idara ya Afya ambapo ameeleza mafanikio ya Wizara yake kwenye idara ya afya ndani ya miaka mitano
 Washiriki mbalimbali wa Siku ya Tamisemi wakiwemo wandishi wa habari, watumishi wa Tamisemi wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo leo wakati wa uzinduzi wa siku ya Tamisemi idara ya Afya.
  Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge akizungumza kwa niaba ya Wakuu wenzake wa Mikoa leo katika uzinduzi wa siku ya Tamisemi uliofanywa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...