MJUMBE wa Kamati
Kuu ya Halmashauri Kuu Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa amesema Serikali inapanga kuanzisha Mamlaka ya Maji Chemba hivi karibuni.
Ametoa kauli hiyo
leo (Jumapili, Septemba 13, 2020) wakati akizungumza na wananchi katika eneo la
Mnadani, Kijiji cha Kelema, Kata ya Paranga, wilaya ya Chemba mkoani Dodoma kwenye
mkutano wa kumuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli na mgombea ubunge jimbo
la Chemba, Mohammed Moni na wagombea udiwani wa CCM.
“Wilaya hii
haina mamlaka ya maji. Kwa hiyo tutaanzisha Mamlaka ya Maji ili watumishi
wawepo wilayani. Wasimamie kwa karibu na waweze kufuatilia vyanzo vya maji
kutokea hapa Chemba wakati tukiendelea kutatua tatizo la maji wilayani hapa. Tutaunda
Mamlaka ya maji hivi karibuni.”
Amesema Serikali
ilitoa sh. bilioni 1.688 za kutafuta vyanzo vya maji huko Orada, Kisanga, Moi,
Mondo na Ndaki. “Pia Serikali ya Awamu ya Tano imetoa sh. milioni 677 za
kuchimba visima huko Mondo, Mrijo Juu, Chambalo, Hamai na Chemba.”
“Tuna uhakika
tukipata lita za maji za ujazo 4,700 zinatosha kabisa kujenga mtandao wa maji. Kazi
ya kuboresha miundombinu ya maji inaendelea. Zimetengwa fedha nyingine, sh.
milioni 150 za kusambaza maji Kelema, Msaada na Bumbu.”
Akizungumzia
sekta ya afya, Mheshimiwa Majaliwa amesema zimetolewa sh. bilioni 1.8 za
kujenga hospitali ya wilaya ya Chemba ili wananchi wapate huduma za tiba wakiwa
hapohapo badala ya kwenda Kondoa kama ilivyokuwa awali.
“Nia yetu ni
kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hukohuko aliko kwa kuweka zahanati
katika kila kijiji, vituo vya afya kwa kila kata. Wakimaliza ujenzi, tumetenga
shilingi milioni 500 za vifaa vya hospitali kwa majengo yote saba.”
“Tumepeleka sh.
milioni 400 za kituo cha afya kule Hamai, shilingi milioni 500 kule Mrijo na
shilingi milioni 400 kule Kwa Mtoro. Kazi ya ujenzi ikiisha, kila kimoja
kitapata shilini milioni 250 za vifaa vya tiba.”
Ninawaomba
mumpe kura Rais Dkt Magufuli, Mbunge na madiwani wa CCM ili tukamilishe kazi hizi
kwa sababu Serikali hii ni ya watekelezaji. Tunasema na tunatenda.”
Wakati huohuo, Mheshimiwa Majaliwa
amesema Rais Magufuli anataka umeme usambazwe kote nchini na ndiyo maana
akaamua kupunguza bei ya kuunganisha umeme.
“Rais wetu
kasema anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inawaka umeme. Amepunguza gharama
za kuunganisha umeme kutoka shilingi 380,000/- hadi shilingi 27,000/-. Rais
wetu kasema ni marufuku kulipia nguzo za umeme.
Mwananchi hutakiwi kulipia nguzo yoyote ile. Atakayekuuzia nguzo,
mwambie akupe risiti, leta risiti tumlipue huyo Afisa., amesisitiza.
Mheshimiwa
Majaliwa anaendelea na mikutano ya kuomba kura wilayani Kondoa.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...