Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV
SHIRIKA la Amend kwa kushirikiana na Total Foundation wametoa mafunzo ya elimu ya usalama kwa vijana wadogo(wanafunzi) 40 wakiwamo wa Shule ya Sekondari Tuliani jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mkakati wa kupunguza ajali za barabarani nchini.
Utolewaji wa mafunzo hayo umepongezwa na Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam huku ikielezwa umuhimu wa mafunzo hayo kwa jamii ya Watanzania kama mkakati wa kuendelea kupunguza ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikitokea nchini.
Akizungumza leo Desemba 17,2020, wakati wa akikabidhi vyeti madereva wa pikipiki na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Tuliani waliopatiwa mafunzo ya mwezi mmoja ya usalama barabarani, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZTO), ACP Nuru Seleman amesema anatoa pongezi kwa Amend na Total Foundation kwa uamuzi huo wa kutoa elimu hiyo.
Mradi mpango huo unaendeshwa na Amend kwa kushirikiana na Total Faundation umefikia wanafunzi 40 kati yao 20 ni wa Shule ya Sekondari ya Tuliani, iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam na wengine 20 wa shule ya Sekondari Tanga pamoja na waendesha pikipiki.
"Hali ya usalama barabarani inaendelea kuridhisha nchini, ingawa idadi ya ajali za barabarani ni kubwa zikigharimu maisha, muda na mali za Watanzania. Kutokana na hali hiyo Serikali inawajibika kuhakikisha ajali zinapungua.
"Hivyo tunapongeza wanaounga jitihada hizi,"alisema ACP Seleman na kuongeza kuwa ajali nyingi za Dar es Salaam zinatokana na uzembe na chanzo kikubwa ni makosa ya binadamu.Kwa hiyo tunawapongeza waandaji wa mafunzo haya Total Foundation na Amend, tunatarajia kile ambacho wamefundishwa tutakiona kwenye uhalisia. Kwa wanafunzi mafunzo haya yatapunguza ajali," amesema Seleman.
Kuhusu waendesha bodaboda , ACP Selemani amewakumbusha wajibu wa kutumia elimu waliyoipata kuhakikisha wao na abiria wao wanakuwa salama kwa kuzingatia yale yote ambayo wamefundishwa. "Mtumie mafunzo haya kama mabalozi, kwa waendesha pikipiki na abiria wao uvaaji kofia ngumu ni jambo la lazima, kwani kati ya majeraha yanaayosababisha vifo kwa wingi na ulemavu wa kudumu ni ya vichwa."
Aidha ametoa mwito kwa wadau mbalimbali kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kupunguza ajali na hiyo itatokana na kufuata sheria za usalama barabarani pamoja na matumizi sahihi ya barabara.
Awali Naibu Mkurugenzi Amend, Thom Bishop, amesema kwamba takwimu zinaonesha watu milioni 1.3 duniani wanakufa kwa ajali za barabarani kwa kila mwaka wakati watu zaidi ya milioni 50 wanajeruhiwa kwa ajili na Afrika ndizo ni hatari.
Amesisitiza kutokana na madhara yanayosababishwa na ajali wameamua kuanzisha mradi huo ili waliopata elimu hiyo ya usalama barabarani wakawe mabalozi kwa wengine.Mradi huo wameuendesha jijini Dar es Salaam ni hatua ya kwanza."Tumefundisha masuala ya usalama barabarani wanafunzi wa sekondari kwa kipindi cha mwezi mmoja wa shule ya Tuliani na Tanga,"
Amesema kwa madereva wa bodaboda wamefundishwa kwa vitendo matumizi ya barabara ili waweze kuchukua tahadhari huku Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Tuliani Yasinta Nandi akieleza wazi mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kufuata taratibu zote za barabarani.
"Ujumbe ambao wameupata wanafunzi wetu 20 tunaamini utawafikia wanafunzi wote 1,610 waliopo shule hapa na elimu hii itafika hadi majumbani kupitia wanafunzi hawa,"amesema.
Wakati huo huo Zelda Kwayamba ambaye ni mmoja wa waathirika wa ajali za pikipiki (bodaboda), ameeleza jinsi ajali iliyopata na kusababisha afanyiwe upasuaji wa nyonga mara 10 huku akitaka jamii hususan waendesha bodaboda kuzingatia sheria ili kuepusha madhara makubwa ikiwamo kupoteza maisha.
Akitoa ushuhuda kuhusu athari na madhara ya ajali za bodaboda yanayioikumba jamii, Zelda ambaye anatembea kwa msaada wa fimbo maalumu, amesema ajali hiyo ilimkuta mwaka 2012 katika eneo la Msamvu mkoani Morogoro na ilimlazimu kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kujitibu ndani na nje ya nchi.
Ushuhuda huo ameutoa wakati wa utolewaji vyeti kwa kwa vijana wadogo(wanafunzi) na madereva wa bodaboda iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Tuliani, Magomeni Dar es Salaam.
"Ajali za barabarani hususan za bodaboda zinaweza kuzuilika au kupunguza madhara yake iwapo kila mmoja atazingatia sheria za usalama barabarani, binafsi ni muhanga wa ajali hizo, nimeona madhara yake, naisihi jamii kufanya kila linalowezekana kuepusha ajali za bodaboda," Zelda.
Kuhusu Amend ni shirika lisilo la kiserikali linaloendeleza, kutekeleza na kuthamini mipango iliyohakikiwa ili kupunguza matukio ya ajali za barabarani kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara. Shirika hili linafanyakazi katika nchi mbalimbali na ina ofisi nchi za Ghana, Tanzania na Msumbiji.
Wakati kwa Total Foundation ni shirika
linashughulikia mipango ya pamoja inayofanywa kila siku ulimwenguni na Total
pamoja na ushirika. Kupitia Programu hii Total Foundation inakusudia kuchangia
mabadiliko ya jamii katika maeneo iliyopo kwa kulenga zaidi vijana kwenye
maeneo manne, ambayo ni ushirikishwaji wa vijana, elimu ya usalama barabara,
hali ya hewa na mazingira.
Mkurugenzi Mtendaji wa Total Tanzania Jean
Francois akizungumza kuhusu uamuzi wa Total Foundation kushiriki katika
kuhakikisha elimu ya usalama barabarani inatolewa kwa watumiaji wa barabara
wakiwemo wanafunzi wa shule za sekondari.

Mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Turiani
akijiandaa kumpa mkono Naibu Mkurugenzi wa Amend Thob Bishop kabla ya
kukabidhiwa cheti chake cha kuhitimu mafunzo ya usalama barabarani yaliyokuwa
yakitolewa kwa siku 30 na Amend kwa kushirikiana na Total Foundation.
Baadhi ya wanafunzi waliopata mafunzo ya elimu ya usalama wa barabarani wakifuatilia hotuba mbalimbali zilizokuwa zikitolewa wakati tukio la utolewaji vyeti kwa wanafunzi na maendesha bodaboda waliopata mafunzo ya usalama barabarani.Mafunzo hayo yametolewa na Amend kwa kushirikiana na Total Foundation na mpango huo wa kutoa elimu hiyo utakuwa endelevu.
Sehemu ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Turian wakisubiri kupata vyeti vyao baada ya kushiriki mafunzo ya elimu ya usalama barabarani, mafunzo hayo yametolewa kwa muda wa siku 30 kupitia Shirika la Amend ambalo limejikita katika kutoa elimu ya usalama barabarani kwa kushirikiana Total Foundation.
Baadhi ya waendesha bodaboda ambao wamepatiwa mafunzo ya elimu ya usalama barabarani wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa tukio la kukabidhiwa vyeti vya kuhitimu mafunzo hayo yaliyotolewa na Shirika la Amend kwa kushirikiana na Total Foundation.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Turian Yasinta Nandi akitoa shukrani zake kwa Amend na Total Foundation kwa kushirikiana katika mafunzo ya elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Wanafunzi wa Sekondari ya Turian wakitoa ujumbe unaohusu elimu ya usalama barabarani kupitia igizo ambalo wamefundishwa wakati wakipatiwa mafunzo ya usalama barabarani.Mafunzo hayo yametolewa na Amend Tanzania kwa kushirikiana na Tofal Foundation.Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZTO), ACP Nuru Seleman akiteta jambo na Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Amend Thom Bishop(wa pili kulia).
Zelda Kwayamba kutoka mkoani Morogoro akitoa ushuhuda wa ajali ya bodaboda iliyomsababishia ulemavu wa kuduma akitoa ushuhuda mbele ya wageni waalikwa, wanafunzi na madereva bodaboda wakati wa uzinduzi wa programu maalum ya usalama barabarani inayotolewa na Amend kwa kushirikiana na Total Foundation.Katika kuhakikisha elimu hiyo inafaka kwa jamii ya Watanzania ,Amend na Total Foundation wametoa mafunzo hayo kwa wanafunzi na madereva bodaboda.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZTO), ACP Nuru Seleman akizungumzia umuhimu wa elimu ya usalama barabarani kama mkakati wa kupunguza ajali au kumaliza kabisa.
Naibu Mkurugenzi wa Amend Tanzania Thom Bishop akizungumza leo Desemba 17,2020 jijini Dar es Salaam wakati wa utoaji vyeti kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Turian pamoja na baadhi ya madereva bodaboda ambao wamepatiwa elimu ya mafunzo ya usalama barabarani .Mafunzo hayo yametolewa na Amend kwa kushirikiana na Total Foundation.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZTO), ACP Nuru Seleman (katikati) akiangalia igizo la elimu ya usalama barabarani lililokuwa likioneshwa na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Turiani(hawapo pichani) ambao wamepatiwa mafunzo ya usalama barabarani kutoka Shirika la Amend kwa kushirikiana na Total Foundation ikiwa ni mkakati wa kupunguza ajali za barabarani nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...