
………………………………………………………………………..
MWAMVUA MWINYI,PWANI
WAKAZI wa Vijiji
,Kata ya Kibindu, jimbo la Chalinze, Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wanatarajia
kuondokana na shida ya ukosefu wa maji safi na salama,inayowakabili kwa
muda mrefu.
Taarifa ya James
Kionaumela Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mzingira Vijijini
(RUWASA), katika ziara katika vijiji vya Kibindu, Kwamduma, Kwamsanja na
Kwakonje, inaeleza, utekelezaji wa miradi hiyo Serikali imetoa kiasi
cha sh. Bilioni 1.6 ambapo milioni 700 kwa ajili ya Bwala la Kijiji cha
Kwamsanja na Kijiji cha Mjembe kuna milioni 900.
“Kijiji cha Kibindu
kina wakazi 11,154 wanapata maji kupitia mradi uliofadhiliwa na JIC
mwaka 2009, vyanzo vyake visima viwili kila kimoja kina uwezo wa kutoa
lita 6,000 kwa saa, unatumia Jenereta mbili una vituo 20 huku wateja 40
wameunganishiwa watu 10,238,” ilieleza taarifa hiyo..
Kionaumela alieleza,
upanuzi wa mradi utaongeza mtandao wa bomba lenye urefu wa mita 830
kuelekea Vulala, shule ya Sekondari Kibindu na ujenzi wa vituo viwili
vya kuchotea maji, na ufungaji wa pampu ya kutumia nguvu ya jua sanjali
na ujenzi wa tenki dogo lenye ujazo wa lita 22,000.
“RUWASA kushirikiana
na Wataalamu kutoka Ofisi ya Bonde la Wami/Ruvu wamefanya upimaji hali
ya upatikanaji wa maji ya chini ya ardhi, taarifa ya awali imewasilishwa
na kuainisha maeneo ya uchimbaji wa visima, hatua inayofuata ni
uchimbaji ili kupata vyanzo vya huduma,” ilibainisha Kionaumela.
Nae mkuu wa wilaya ya
Bagamoyo ,Zainab Kawawa aliishukuru Serikali kwa kuweka kipaumbele
katika miradi ya maji ambayo ndio changamoto kubwa.
Aliwataka viongozi wa RUWASA kutekeleza majukumu yao mapema ili kazi hizo zikamilike hatimae wanancji wanufaikea na huduma.
“Wakati anazungumza
na Taifa kupitia ufunguzi wa bunge, Rais Dkt. John Magufuli alisema
Serikali yake itaendelea kuelekeza nguvu katika kutatua kero za
wananchi, hususani sekta ya maji, leo tunashuhudia kazi inayofanyika,
niwaombe hii kazi ikamilike mapema,” alisema Kawawa.
Mbunge wa jimbo la
Chalinze,Ridhiwani Kikwete alifafanua,kero ya maji katika vijiji
vinavyounda Kata ya Kibindu ilikuwa kubwa, na kwamba pamoja na uwepo wa
mikakati hiyo wananchi walikuwa wanalalamikia ujenzi wa mabwawa hayo,
lakini amepata faraja kubwa kuona RUWASA wakiwa katika harakati hizo.
“Wananchi wetu wa
Kata ya Kibindu kwa muda mrefu walikuwa wanasubiri ujenzi wa mabwawa
haya kwa ajili ya upatikanaji wa maji, leo nimefarijika sana kuona
mikakati iliyopo ya kuwaondolea adha ya maji wananchi hawa,” alisema
Ridhiwani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...