Na Munir Shemweta, SAME
Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameshusha neema
kwa vijiji vitatu vya Ndungu, Msufini na Mpirani vilivyopo tarafa Ndungu
wilayani Same mkoani Kilimanjaro kwa kuvipatia ekari mia tatu vijiji
vitatu.
Hatua hiyo
inafuatia wananchi wa vijiji hivyo kuomba kupatiwa sehemu ya ardhi ya
Mwekezaji ambaye ni kampuni LM Investment inayozalisha Katani kutokana
na ardhi ya maeneo wanayoishi kuwa tepetepe ambapo baada ya uamuzi huo
sasa Mwekezaji atabakia na ekari 2,452.844.
Akizungumza
na wananchi wa Ndungu wilaya ya Same mkoa wa Kilimanjaro tarehe 20
Desemba 2020 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema,
baada ya Mwekezaji kuachiwa ekari hizo 2,452.844 serikali inachotaka ni
kuona uwekezaji ukifanyika kwenye shamba hilo na kinyume na hivyo
Mwekezaji atanyang'anywa shamba.
Alimuonya
Mwekezaji LM Investment ahakikishe anaendeleza shamba lake na kupanda
mkonge ili kutoa fursa ya ajira kwa vijana na kusisitiza kuwa
haiwezekani Mwekezaji kuwa na ekari 2,452.844 halafu atoe ajira ya watu
50 tu.
"Hatufukuzi
wawekezaji bali tunataka maendelezo katika shamba na tunataka muwekezaji
kuacha kutumia mkopo kuendeleza maeneo mengine" alisema Lukuvi.
Ombi
la wananchi hao kutaka kumegewa ardhi ya shamba la Mwekezaji
lilisababisha Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William
Lukuvi kuona umuhimu wa wananchi hao kupatiwa ardhi kwa ajili ya makazi
na kuamua kupunguza sehemu ya ardhi la shamba la Mwekezaji na kukipatia
kila kijiji ekari mia moja.
Kwa
mujibu wa Waziri wa Ardhi, tayari taratibu zote za upimaji na upangaji
wa eneo la shamba hilo zimefanyika ikiwemo kusajili ramani na kuweka
wazi kuwa wiki hii ofisi ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Same
itakwenda kukabidhi ardhi kwa vijiji hivyo vitatu pamoja na Mwekezaji .
Waziri
Lukuvi alisema, sasa ardhi ya shamba hilo imehama kutoka mikono ya
kijiji na sasa wananchi wake watapatiwa hati za mjini za miaka 99 na
Hati za Kikila hazitatolewa katika eneo hilo kama ilivyokuwa ikifanyika
huko nyuma.
"
Halmashauri na serikali ya kijiji mtakaa pamoja na kukokotoa gharama za
kuchangia maana tumefanya kazi kubwa ya kuwatafutia ardhi na gharama
zenyewe hazitazidi zile za mjini, pamoja na eneo hilo kupangwa lakini
eneo ambalo wananchi walijenga muda mrefu nalo litarasimishwa" alisema
Lukuvi.
Akigeukia suala
la ukaguzi mashamba, Lukuvi aliagiza kufanyika ukaguzi wa mashamba yote
makubwa kwa lengo la kutaka kujua uwekezaji uliyofanyika pamoja na kujua
namna Wawekezaji yanavyochangia kodi za serikali pamoja na utoaji
ajira kwa wananchi wanaozunguka mashamba hayo.
Waziri
Lukuvi aliagiza Makamishna wa Ardhi Wasaidizi katika mikoa kufanya
ukaguzi haraka na kuona kama uwekezaji wa mashamba makubwa kama una
tija.
Kwa niaba ya
wananchi wa vijiji hivyo Mzee Kabongo mkazi wa Ndungu alimshukuru
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuwezesha kupatikana
kwa ekari hizo mia tatu kwa vijiji vitatu na kumuomba Waziri Lukuvi
kufikiria uwezekano wa kuongeza ekari nyingine katika vijiji hivyo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akifurahiwa na wananchi wa Tarafa ya Ndungu wilayani Same baada ya kuwatangazia kupata ekari mia tatu katika vijiji vya Msufini, Mpirani na Ndungu tarehe 20 Desemba 2020.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akikagua uzalishaji katani katika shamba là Mwekezaji LM INvestment Tarafa ya Ndungu wilayani Same mkoa wa Kilimanjaro alipokwenda kuvipatia vijiji vitatu ekari mia tatu kwa ajili ya makazi tarehe 20 Desemba 2020, kulia kwa Lukuvi ni Mkuu wa wilaya ya Same Rosemery Senyamule.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...