Na Mwandishi wetu, Haydom

WANARIADHA 410 wa Mikoa ya Manyara, Singida na Arusha wamechuana
vikali kwenye mashindano ya Haydom Marathon 2020 kwa lengo la
kukusanya fedha za ujenzi wa wodi ya watoto wachanga ya hospitali ya
rufaa Haydom.

Mkurugenzi wa tiba wa hospitali ya rufaa ya Haydom Dkt Paschal Mdoe
akizungumza kwenye mashindano hayo amesema kwa mwaka huu wa 2020 lengo lilikuwa ni kukusanya shilingi milioni 100.

Amesema wamekusanya shilingi milioni 40 na wanaendelea kukusanya ili
ifike lengo la kukusanya shilingi milioni 100 ambazo watazichanganya
na zile shilingi milioni 100 za mwaka jana ili ujenzi wa jengo jipya
la wodi ya watoto wachanga uanze mapema Januari 2021.

Amesema lengo lao ni kufikisha shilingi milioni 300 ili kufanikisha
gharama za ujenzi hivyo kupitia mashindano hayo na michango ya wadau
wengine watafanikisha fedha za ujenzi wa jengo hilo la watoto wa
changa.

"Kwenye wodi ya watoto hivi sasa wa siku ni kati ya 20 hadi 30 awali
tulikuwa na watoto watano au sita, jengo la sasa ni dogo, linahitajika
lingine ambalo litawekewa vifaa vingi zaidi vya teknolojia," amesema
Dkt Mdoe.

Amesema mbio hizo zinatarajiwa kuendelea tena mwezi Mei mwaka 2021 kwa
lengo la kuchangia wodi hiyo ya watoto wachanga kupitia Haydom
Marathon Run for life saves neonates.

Katika mashindano ya mbio za kilomita 21 mwanariadha chipukizi kutoka
kata ya Endamilay wilayani Mbulu, Herman Sulle alishika nafasi ya
kwanza na kujipatia shilingi 250,000 kwa muda wa 1.06.13.95 Joseph
Martin wa wilaya ya Babati alishika nafasi ya pili kwa muda wa
1.06.35.31 na kujipatia shilingi 125,000 huku Anthony Moya wa wilaya
ya Hanang' akishika nafasi ya tatu kwa muda wa 1.06.48.85 na kujipatia
shilingi 75,000.

Kwa upande wa wanawake kilomita 21 mshindi alikuwa Tunu Andrea wa
mkoani Singida aliyejtumia muda wa 1.28.16.75 nakujipatia shilingi
250,000 huku mshindi wa pili Neema Sanka wa Karatu akijipatia shilingi
125,000 na kutumia muda wa 1.32.52.71 na watatu ni daktari wa
hospitali ya rufaa ya Haydom, Dkta Laura Chuwa aliyepata shilingi
75,000 kwa kutumia muda wa 1.59.90.91.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga
akizindua mashindano ya Haydom Marathon kilomita 21, kilomita 10 na
kilomita mbili alisema Mbulu ndiyo chimbuko la riadha nchini.

Kamoga amesema huwezi kuzungumzia historia ya riadha nchini bila
kumtaja mwanariadha maarufu Stephen John Akwary ambaye ametokea
wilayani Mbulu.

Amesema eneo la Mbulu ni sahihi kwa serikali kuweka kambi kuliko
kuweka maeneo yenye kiwango cha juu cha joto kwani Haydom hali ya hewa
kutoka usawa wa bahari ni nzuri na inafaa kwa riadha.

Mbunge wa jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Maasay amesema michezo ni
afya kwani ukishiriki utakuwa mbali na daktari hasa kwenye magonjwa
yasiyoambukizwa ya kisukari na shinikizo la damu.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya
Mbulu, Nicolaus Nsangazelu amewapongeza washiriki wote na waandaji wa
Haydom Marathon.

Mwanafunzi wa utabibu wa chuo cha uuguzi Haydom (HIHS), Glory Naman
amesema ameshiriki mbio hizo siyo kea lengo la mashindano bali
kuchangia wodi ya watoto wachanga.

Mwanafunzi mwingine wa utabibu wa chuo cha uuguzi Haydom (HIHS),
Sweetbert Msofe amesema jamii inapaswa kuunga mkono mbio hizo kwa
kushiriki riadha endapo zitafanyika tena mwezi Mei 2021.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...