
Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard
Kalemani, akimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mha.
Leonard Masanja, alipokuwa akiwasilisha taarifa ya Majukumu ya Wizara ya
Nishati pamoja na Taasisi zake kwa Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard
Kalemani na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato, (hayumo
pichani) kwenye kikao cha Menejimenti ya Wizara hiyo kilichofanyika leo
kwenye ofisi za Wizara ya Nishati zilizopo Mtumba jijini Dodoma.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mha.
Leonard Masanja akiwasilisha taarifa ya Majukumu ya Wizara ya Nishati
pamoja na Taasisi zake kwa Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani
na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato, ( hawamo pichani)
katika mkutano wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati uliofanyika leo
katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtumba jijini Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya
Nishati wakifuatilia kwa umakini maelekezo ya Waziri wa Nishati, Mhe.
Dkt. Medard Kalemani wakati wa kikao cha Menejimenti kilichofanyika leo
katika ofisi za Wizara hiyo, zilizopo Mtumba, jijini Dodoma.
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani,
akizungumza na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato, ofisini
kwake leo katika mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma kabla ya kukutana
na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati.
*************************************
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani,
amewataka watumishi wa Wizara ya Nishati kufanya kazi kwa kasi na kwa
ubunifu ili kuhakikisha sekta ya Nishati inaendelea kukua ili kuwezesha
upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika kwa maendeleo ya Viwanda
na kuliletea Taifa maendeleo.
Waziri Kalemani ameyasema hayo leo Desemba 10,
2020 wakati akiwa kwenye kikao na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya
Nishati kilichofanyika katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo katika Mji
wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Kikao hicho cha Waziri na wajumbe wa Menejimenti
ya Wizara ya Nishati, kilichohudhuriwa na Naibu Waziri Mhe. Stephen
Byabato, kimelenga kutambulisha viongozi wa Wizara hiyo na kutoa
maelekezo yanayolenga kuwa na utekelezaji mzuri wa malengo yaliyowekwa
katika Sekta ya Nishati.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Kalemani
ameiagiza Menejimenti ya Wizara hiyo kuhakikisha kuwa umeme wa uhakika
na wa kutosha unazalishwa nchini kutoka kwenye vyanzo vya gharama nafuu
hasa maji.
Pia, ameitaka Menejimenti ya Wizara ya Nishati,
kuhakikisha kuwa ujenzi wa miundombinu ya kusafirishia umeme kutoka kona
zote nne unakamilika kwa wakati na kuwe na mtandao wa njia ya
kusambazia umeme kwa kona zote nne kaskazini, Kusini, Mashariki na
Magharibi.
Vilevile, Waziri Kalemani, ameuagiza uongozi wa
Wizara ya Nishati, kuhakikisha kuwa vijiji vyote 2884 ambavyo
havijaunganishwa na umeme, ifikapo mwezi Desemba 2022, viwe
vimeunganishwa na huduma hiyo.
Naye Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen
Byabato, ameahidi kutoa ushirikiano mzuri na kufanya kazi kwa weledi
katika kuhakikisha majukumu ya Waziri wa Nishati yanafanyika kwa ufanisi
mkubwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...