Na Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma
Bodi
na Mabaraza ya kitaaluma ya sekta ya afya yamekutana kuandaa mpango
mkakati wa pamoja wa kuweza kudhibiti mmomonyoko wa maadili kwa watoa
huduma za afya nchini hali ambayo hivi sasa imeongezeka kwa kiwango
kikubwa kwa wanataaluma wengi.
Hayo yameelezwa leo na Msajili wa
Baraza la Wauguzi na Wakunga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wasajili wa
Bodi na Mabaraza ya kitaaluma Bi. Agnes Mtawa wakati wa kikao cha
pamoja kilichofanyika kwenye ukumbi wa wizara jijini Dodoma.
Mtawa
amesema hivi sasa maadili, uwajibikaji na utendaji wa kazi kwa
watumishi wa sekta ya afya umekua ukishuka kila siku hivyo sasa
wanajipanga kuweza kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza kuinua hali ya
utoaji huduma za afya kwenye vituo vya afya.
“Hali ilivyo sasa
kumekua na ongezeko la mmomonyoko wa maadili ambao unaathiri utoaji wa
huduma zetu za afya kwahiyo tumekaa na kupanga maeneo yote ambayo
tunahusika na kutekeleza kwa pamoja ili kuhakikisha wanataaluma wetu
wanafanya kazi kwa kufuata maadili,taratibu,kanuni na sheria za taaluma
zetu pamoja na wananchi wanapata huduma bora”.Alisema.
Aidha,
amesema kuwa katika maeneo ya kazi wamepanga kuweka mfumo madhubuti
ambao utawawezesha kama bodi na mabaraza kuweza kuwapata taarifa kwa
wale ambao wamekuwa wanafanya kazi nje ya maadili na kuchukua hatua
stahiki kwenye ngazi zote za utumishi.
Kwa upande wa
wauguzi,Mtawa amesema kweli kumekuwa na malalamiko ambayo wananchi
wamekuwa wakiwalalamikia wauguzi na wakunga kutokana na baadhi yao
kutotekeleza majukumu yao ipasavyo.
“lakini pia malalamiko
mengine ni wananchi kutokujua mipaka ya utekelezaji wa majukumu ya
wauguzi na wakunga hivyo kwa kuweka mfumo wa ushirikiano utaweza
kuhakikisha wanapatia ufumbuzi malalamiko hayo”.
Hata hivyo
amesema sheria zote za mabaraza ya kitaaluma yanatambua viongozi
wasimamizi katika ngazi zote za vituo vya afya hivyo wanawajengea uwezo
ili kutoa elimu na kuwakumbusha wataalam masuala ya maadili na
uwajibikaji kule wanapotoa huduma pamoja na kuchukua hatua kwa wale
ambao wanaendeleza vitendo ambavyo vinawakera wanachi.
Naye
Msajili Baraza la Famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe amesema kuwa upande wa
dawa bado kumekuwa na tazizo kutokana na kutowajibika kwa wanataaluma
na kutozingatia maadili wakati wa kutekeleza majukumu yao.
“Sisi
tunategemewa na wananchi katika kuhakikisha kwamba wanapata dawa,ni kosa
kwa mwanataluma kutoa dawa kwa mgonjwa ambayo imekwisha muda wake”.
Shekalaghe
amesema Sheria ya Famasi, Sura 311 ikisomwa pamoja na Kanuni za
Maadili na Utendaji wa Taaluma za Mwaka 2020,zimeweka bayana kuwa
mwanataaluma anapokutwa na kosa la kutowajibika na Baraza kuthibitisha
hilo anastahili kusimamishwa katika utendaji na ikibidi kufutiwa usajili
pamoja na leseni yake.
“Niwaeleze wafamasia na fundi dawa
sanifu na wasaidizi kwamba unapokosa wakati unapofanya kazi kwenye sekta
ya umma haiwezekani ukaenda kwenye sekta binafsi ukidhani kuwa ni
mbadala kwa sababu Baraza la Famasi ni chombo cha Serikali na unapokosa
huwezi kufanya kazi sehemu nyingine hivyo ni bora mkawajibika na
kuzingatia maadili katika maeneo yenu ya kazi kwani hatutosita
kumchukulia hatua yeyote atakayeenda kinyume na maadili na taratibu
zilizowekwa”Alisisitiza
Aidha, amesisitiza kufanya kazi kwa
kushirikiana na kuwataka watendaji kwenye halmashauri kuibua hoja na
kutoa taarifa za ukiukwaji ili matatizo hayo yaweze kushughulikiwa
kuliko kuwasubiri viongozi kwenda huko chini.
Wakati huo huo
Msajili wa Baraza la Madaktari Tanganyika Dkt. David Mzava amewataka
madaktari wote nchini kufuata taratibu za utoaji huduma bora kwa
wagonjwa kwani wananchi wamekuwa wakilalamika sana katika eneo hilo
kwani mgonjwa anapotoka kwa daktari anatakiwa awe amefarijika.
Dkt.
Mzava amesema kutomshirikisha mgonjwa ipasavyo ni kukiuka miiko na
viapo vya taaluma vya utoaji huduma za afya kwenye taaluma hii.
Pia
amewata madaktari kuzingatia utaratibu wa kuhakikisha wanamtaarifu
mgonjwa ana tatizo gani ili mgonjwa aweze kuchukua hatua kwenye kuongoza
nini afanyiwe kwenye matibabu anayofanyiwa.
“Ni vyema mwana
taaluma kuzingatia kuwaona wagonjwa wako kwa wakati ili kujua kama
mgonjwa ana dharura. Hivi sasa wagonjwa wengi wanaonwa na mwana taaluma
mwenye ngazi ya chini muda wote hii hapana kwani kuna ngazi mbalimbali
za kumuona mgonjwa”.Alisisitiza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...