Na Shukrani Kawogo, Njombe.

Kutokana na uhitaji mkubwa wa wananchi  juu ya uwepo wa kituo cha kuuzia mafuta ya petrol na disel katika halmashauri ya wilaya ya Ludewa mkoani Njombe hatimaye halmashauri hiyo imefanikisha kumpata muwekezaji atakayenunua eneo lililotengwa kwa ajili ya shughuli hiyo.

Hayo ameyasema mkurugenzi wa halmashauri hiyo Sunday Deogratias katika kikao cha baraza la madiwani baada ya mwenyekiti wa kamati ya huduma za uchumi, ujenzi na mazingira Robert Njavike kuwasilisha taarifa ya robo ya pili ya mwaka wa fedha 2020/2021 walipokuwa wakijadili taarifa za kamati mbalimbali za madiwani na kuulizwa swali na diwani wa kata ya Mavanga Daudi Luoga juu ya hatua iliyofikia katika mchakato wa kutafuta muwekezaji wa kujenga kituo hicho.

 Amesema wamekuwa wakitangaza kwa muda mrefu kuhitaji muwekezaji na awali walijitokeza wawekezaji wawili ambapo wakwanza alishindwa kulipia pesa kwa wakati na mwingine alikuwa tayari kununua lakini hakutaka kuwekewa kikomo cha muda wa kujenga kituo hicho.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo waliamua kuendelea na mchakato wa kutafuta muwekezaji mwingine kwakuwa wao wanachohitaji si fedha bali kituo cha mafuta ambapo ndani ya wiki hii walifanikiwa kumpata na kukubaliana kuuziana eneo hilo kwa Sh.  Ml. 28 na mpaka sasa muwekezaji huyo tayari amekwishalipa kiasi cha shilingi Ml. 14.

"Makubaliano ya mkataba wetu ni kujenga kituo hicho ndani ya miezi sita ambapo baada ya kutanguliza nusu hiyo ya fedha tumekubaliana ndani ya miezi mitatu atamalizia kiasi kilichobaki kisha atasaini mkataba na baada ya hapo ataruhusiwa kurasimisha na kupata hati ya kiwanja", Alisema Deogratias.

Wakati huo huo diwani wa kata ya Makonde Chrispin Mwakasungura alimuuliza mkurugenzi huyo hatua iliyofikia katika mkakati wa upimaji viwanja katika maeneo mbalimbali na utoaji hati za kimila kwa gharama nufuu kwakuwa katika vikao vya awali walikwisha adhimia uendeshwaji wa zoezi hilo huku akitia mkazo upimwaji katikati eneo la Ludewa kijijini.

Akijibu swali hilo Mkurugenzi huyo amesema katika bajeti ya 2020/2021 wanatarajia kurasimisha maeneo mawili ambayo ni kata ya Mlangali ambapo mpaka sasa tayari wananchi 50 wamesha rasimishiwa pomoja na Lugarawa nako mpaka sasa wananchi 25 wamesha rasimishiwa sambamba na hilo pia kuna maeneo ambayo yanaendelea kukua hivyo ili kurasimisha ni lazima kuwepo na tangazo la serikali.

 Ameongeza kuwa tangazo hilo limekwisha andaliwa katika maeneo ya Madope, Madilu, Mavanga, Luilo, Lupingu pamoja na Makonde hivyo tangazo hilo litakapotoka maeneo hayo pamoja na mengine yatakuwa yameingia katika mpango wa kurasimisha na kuahidi kulifanyia kazi eneo la Ludewa kijijini.

Sanjari na hilo pia mkurugenzi aliwataka madiwani kupeleka maombi rasmi ya wananchi watakaokuwa wamejikusanya na kuhitaji kupimiwa maeneo yao naye atawatuma wataalamu kwa ajili ya kufanya kazi hiyo ya urasimishaji kwani anapoomba mwananchi mmoja mmoja gharama yake inakuwa kubwa zaidi.

"Wananchi watakapoungana na kuomba kurasimishiwa ardhi hii itawasaidia kupatiwa huduma kwa haraka na kwa gharama nafuu ukilinganisha na maombi ya mtu mmoja mmoja, hivyo madiwani nawaomba muwasaidie wananchi kufikisha maombi ya pamoja ya urasimishaji ili waweze kuhudumiwa kwa haraka", Alisema Deogratias.

Diwani wa kata ya Mavanga Daudi Luoga akiulizwa swali juu ya upatikanaji wa muwekezaji Katika eneo la ujenzi wa kituo cha mafuta, Katika kikao cha baraza la madiwani.
Diwani wa kata ya Makonde Chrispin Mwakasungura akiulizwa swali juu ya urasimishaji wa maeneo mbalimbali ya vijiji, Katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Katika ukumbi wa halmashauri.
Madiwani wa kata mbali mbali za wilaya ya Ludewa wakijadili taarifa za kamati mbalimbali za baraza la madiwani wakati wa kikao cha baraza hilo.

Wananchi pamoja na wakuu wa idara mbalimbali wakifuatilia taarifa za kamati mbalimbali za madiwani katika kikao cha baraza la madiwani.
Mkuu wa wilaya ya Ludewa Andrea Tsere (Aliyesimama) akiongea na baraza la madiwani wilayani humo katika kikao cha kujadili taarifa za kamati mbalimbali za madiwani hao. Kulia kwake ni Makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo Leodga Mpambalioto, mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo Stanley Kolimba pamoja na katibu wa CCM wilaya hiyo Bakari Mfaume.

 Diwani wa kata ya Milo Robert Njavike ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya huduma za uchumi, ujenzi na mazingira akiwasilisha taarifa ya kamati yake Katika kikao cha baraza la madiwani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...