MBUNGE wa jimbo la Kibamba  Mhe.Issa Mtemvu  amewatembelea wagonjwa katika  Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila na kutoa    zawadi kwa  baadhi ya wagonjwa wenye uhitaji .

Zawadi hizo zimejuisha pampasi za watu wazima, mafuta ya nazi,Maji ya kunywa,sabuni,miswaki  pamoja na dawa ya meno.

Akipokea zawadi hizo kwa niaba ya Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Deogratias Manyama amemshukuru mbunge huyo kwa kuwatembelea wagonjwa na kutumia fursa hiyo kueleza baadhi ya changamoto zinazoikabili hospitali ikiwemo gharama za uendeshaji pamoja na changamoto ya vyombo vya usafiri.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi katika wodi ya wagonjwa wenye uhitaji hospitalini hapa,  Mhe. Issa Mtemvu amesema kuwa lengo la kutembelea Mloganzila ni kutoa mkono wa pole kwa wagonjwa na kuwatakia heri ya mwaka mpya.

 “Nimekuja kuwapa mkono pole kama mwakilishi wenu bungeni na kuwatakia heri ya mwaka mpya pamoja na kutumia fursa hii kusikiliza changamoto zinazoikabili hospitali hii ili niweze kuziwasilisha bungeni kwa waziri mwenye dhamana”amesema Mhe. Mtemvu

Mhe. Mtemvu amewataka wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya afya ambayo itawasaidia kupata matibabu kwa uhakika.










Mratibu wa Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Bahari Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish), Dkt. Nichrous Mlalila ameziomba Halmashauri kuvitambua Vikundi vya Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) na kuzipa uwezo wa kukusanya mapato yatokanayo na shughuli za uvuvi ili ziweze kusaidia vikundi hivyo kujiendesha na kuendeleza sekta ya uvuvi nchini. 

Dkt. Mlalila alitoa rai hiyo katika ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya BMU inayojengwa na Mradi wa SWIOFish katika Kata ya Dunda, Wilayani Bagamoyo Januari 7, 2021. 

Kwa mujibu wa Dkt. Mlalila sehemu kubwa ya mapato yanayokusanywa kwa sasa na Halmashauri hayarudishwi kwa Jamii ya wavuvi kwa ajili ya kuendeleza shughuli za sekta na uchumi wa jamii husika.

Dkt. Mlalila alisema anatambua kuwa kuna changamoto ya kisheria ambayo baadhi ya Halmashauri zimetumia kuzizuia BMU kukusanya mapato yanayotokana na rasilimali za uvuvi.

“Tunahamasisha Halmashauri kuwapa uwezo BMU kukusanya mapato ili kuziwezesha kupata kipato cha uhakika cha kuendesha shughuli zao za kulinda rasilimali za Uvuvi lakini pia mapato hayo yatawezesha kuendeleza sekta ya uvuvi tofauti na ilivyo sasa,” alisema Dkt. Mlalila

Katika baadhi ya Halmashauri ambazo wamewapa kazi BMU ya kukusanya mapato kama vile Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Mkoani Tanga, Mapato yanayotokana na uvuvi yameongezeka kutoka shilingi milioni 9 kwa robo mwaka hadi milioni 51 na kutoka shilingi milioni 36 hadi milioni 256 kwa mwaka.

“Nazishauri Halmashauri nyingine zichukue mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani kwa sababu sisi tumezipa mafunzo ya kina hizi BMU katika kusimamia fedha na ukusanyaji wa mapato, hivyo tunaamini hilo ni suala la mchakato na tumewasilisha andiko TAMISEMI ili kuangalia namna ya kuzifanya BMU kuendelea na shughuli zake hata pale ambapo mradi wa SWIOFish utakapokwisha muda wake,” aliongeza Dkt. Mlalila

Akizungumzia suala hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alisema kuwa BMU ya kata ya Dunda na zingine zikajifunze Pangani kuona wao wanafanyaje na sisi kama Wizara tutaangalia kama kuna chanzo ambacho wataalam wa Halmashauri wanakusanya na hakifanyi vizuri na kuna BMU mahali inakusanya vizuri basi tutaibua hiyo hoja tuone tutafanyaje.

“Ukweli ni kwamba kwenye vyanzo hivi vya leseni na ushuru wa rasilimali za uvuvi katika halmashauri zetu nyingi hazifanyi vizuri na hivyo kuna haja ya kuviangalia vizuri hasa wataalam wetu wanaotumika kukusanya hayo mapato kwa sababu kuna baadhi yao wamefanya hapo ndio maeneo yao ya kupatia pesa zao,” alisema Gekul.

Alisema Wakurugenzi wanaweza kuwa na nia njema kabisa lakini wale wanaotumwa kukusanya hayo mapato wanarudisha maduhuli hayo kama walivyotumwa? Kama kuna watu wanauwezo wa kukusanya zaidi ya wataalam wa Halmashauri sidhani kama kuna haja ya kuwa na kigugumizi cha kuwatoa hao watu ili kazi hiyo apewe anayeweza kukusanya vizuri.

“Kwa sababu mwisho wa siku sisi wananchi tunachotaka ni maendeleo hivyo nisingependa niseme moja kwa moja hapa kuwa BMU wapewe kazi hiyo isipokuwa Halmashauri ziangalie kama sheria inawaruhusu kuwatumia BMU kukusanya mapato,” aliongeza Gekul

Gekul alisema kuwa wao kama Wizara watawasiliana na TAMISEMI kuona maelekezo yakoje kwa sababu anasema kuna vyanzo Halmashauri zenyewe zinakusanya na vingine vinaruhusiwa kukusanywa na wakala na pale ambapo BMU itaonekana inafaa ipewe uwezo wa kukusanya.

Mradi wa SWIOFish unafadhiliwa na Benki ya Dunia kuhamasisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za bahari na ndio umeimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi wa rasilimali za bahari (BMU) kwa ajili ya kulinda na kuhamasisha uvunaji endelevu wa rasilimali za bahari katika Wilaya za Mkinga, Pangani, Bagamoyo, Lindi Vijijini na Tanga Jiji.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...