Naibu Waziri wa Ujenzi
na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala
wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Rukwa mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara
ya Sumbawanga - Matai – Kasanga Port
yenye urefu wa kilometa 112, mkoani
Rukwa.
Naibu Waziri wa Ujenzi
na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akizungumza na waandishi wa habari
mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Sumbawanga - Matai – Kasanga Port yenye urefu wa kilometa
112 na upanuzi wa bandari ya Kasanga,
mkoani Rukwa.
NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,
Mhandisi Godfrey Kasekenya, amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo
kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kutatua kero na malalamiko ya wananchi
kwa wakati katika miradi na huduma wanazozitoa.
Akizungumza mkoani Rukwa mara baada ya
kukagua ujenzi wa barabara ya Sumbawanga -
Matai – Kasanga Port yenye urefu wa kilometa 112 na upanuzi wa bandari ya Kasanga, Naibu Waziri
Kasekenya ameridhishwa na utekelezaji wa barabara hiyo na kumtaka mkandarasi
China Railway 15 Group kukamilisha sehemu iliyobaki yenye urefu wa mita 150
katika kipindi cha siku 45.
Aidha, amemtaka Mkandarasi Shanxi
Construction Engineering anaetekeleza mradi wa upanuzi wa bandari ya Kasanga
kutathmini kazi anayoifanya kama iko katika viwango vinavyokubalika kwa mujibu
wa mkataba kabla ya kuchukuliwa hatua.
“Hakikisheni kazi za ujenzi wa
barabara na upanuzi wa bandari zinakamilika katika kipindi kifupi kuanzia sasa,
kwa kuwa muda uliopangwa kimkataba umemalizika”, amesema Naibu Waziri Kasekenya.
Naibu Waziri huyo amemuagiza
Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Meneja
wa Bandari ya Kigoma kufika eneo la mradi ndani ya wiki moja kwa ajili ya kukagua
maendeleo ya mradi huo na kutoa ripoti.
Kukamilika kwa barabara ya Sumbawanga
- Matai – Kasanga Port na upanuzi wa bandari ya Kasanga ni mkakati wa Serikali
wa kuhuisha uchumi katika ukanda wa Magharibi wenye mikoa ya Songwe, Rukwa na
Katavi na hivyo kuchochea biashara kati ya Tanzania na nchi za Zambia, Burundi
na Congo DRC.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Karolius
Misungwi, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa kukamilika kwa miradi hiyo
kuchochea shughuli za kibiashara za Wilaya na kuiomba Serikali kuendelea kuibua
fursa za kiuchumi kwenye ukanda huo wenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula
na biashara.
Naibu Waziri Kasekenya yupo katika
ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa miundombinu katika Ukanda wa mikoa ya Magharibi
ambapo pamoja na mambo mengine anakutana na watumishi wa Wizara ili
kubadilishana uzoefu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...