WAZIRI WA MAJI AAGIZA WAPEWE AJIRA...ATATUA CHANGAMOTO ZA CHUO
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso ameagiza wahitimu wa Chuo cha Maji ambao wamehitimu mafunzo yao ya kada mbalimbali katika chuo hicho wapewe ajira huku akitoa maagizo kwa Katibu wa Wizara hiyo kutoa Sh.milioni 500 ndani ya siku saba ili kukarabati majengo na ujenzi wa miundombinu chuoni hapo.
Pia ametoa maelekezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji kuhakikisha anatafuta fedha Sh.milioni 251 ambazo zitakwenda kutumika katika kuboresha miundombinu ya zahanati ya Chuo cha Maji ambayo kwa sasa imebaki kuwa gofu.
Ametoa maagizo na maelekezo hayo wakati wa mahafali ya 12 ya Chuo cha Maji yaliyofanyika jijini Dar es Salaam ambapo wahitimu 529 watunukiwa vyeti baada ya kuhitimu ngazi mbalimbali za kitaaluma.
Wakati wa mahafali hayo mbali ya Mgeni rasmi Aweso pia alikuwepo Naibu Waziri Wizara ya Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Naibu Katibu Mkuu, Bodi ya Chuo cha Maji, Wakurugenzi na wakuua wa idara na taasisi za sekta ya maji pamoja na menejimenti ya Chuo.
Kuhusu wahitimu wa Chuo cha Maji kupewa ajira, Waziri huyo wa Maji, amesema kuna miradi mingi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini ambayo inatumia fedha nyingi za Serikali lakini wanaopewa nafasi ya kusimamia miradi hiyo zikiwemo kamati za maji hazina watalaamu wa sekta ya maji.
Hivyo matokeo yake miradi mingi inakosa usimamizi mzuri na katika kuondoa changamoto hiyo, ameagiza wahitimu wa Chuo cha Maji kwa kuanza na waliotunukiwa vyeti vyao mwaka huu wapewe ajira ili wakasimamia miradi hiyo kote nchini.
"Haiwezekani wahitimu wa Chuo cha Maji waendelee kulalamika suala la kukosa ajira, watalaamu wanazalishwa kila mwaka katika chuo hiki lazima jeshi hili kubwa tulitumie, hivyo naagiza hawa wahitimu wote wa mwaka huu wapewe ajira , waende wakafanye kazi katika sekta yetu ya maji, huu si wakati wa kulalamika , ni wakati wa kufanya kazi.
"Kwanini Zahanati au kituo cha afya kinapojengwa na kukamilika wanaopangiwa kufanya kazi ni wale waliosomea mambo ya afya, lakini katika miradi ya maji inapokamilika wanapewa watu ambao sio waliosomea masuala ya maji, hivyo tunataka hawa wahitimu hawa wapewe ajira, tuwaaamini na wanaweza."
Akizungumzia miundombinu ya Chuo cha Maji , amesema kuna kila sababu ya Wizara ya Maji kuwekeza nguvu katika kukisaidia na kukiendeleza chuo hicho kwa kuanza na utatuzi wa uchakavu wa majengo , na katika kushughulikia changamoto hiyo, menejimenti iliomba Sh.bilioni moja lakini haijatoka kwa muda mrefu.
"Hivyo nakuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Maji ndani ya siku saba chuo hiki kiwe kimepata Sh.milioni 500 ili kuanza ukarabati wa majengo na ujenzi wa miundombinu mingine inayohitajika.Hatuwezi kukiacha chuo kibaki kilivyo sasa ambacho kimechoka.Nimekagua majengo ya chuo mengi yamechakaa.Mimi na Wizara hatutakuwa kikwazo kwa chuo hiki, bali tutahakikisha tunashirikiana katika kutatua changamoto zilizopo.
"Lengo la kuwepo kwa chuo hiki ni mahususi katika kuzalisha watalaam wa sekta ya maji ambao watakwenda kutatua changamoto zilizopo hasa za uhaba wa maji na kwa sasa tunayo kampeni ya kumtua ndoo mama kichwani, jeshi hili kubwa linalozalishwa ni maalum kwa kazi hiyo.Fedha hizo lazima zije na zifanye kazi inayotakiwa,"amesema Aweso
Aidha amesema amekagua zahanati ya Chuo cha Maji, ambayo imekuwa kama gofu kutokana na kuchakaa kwa miundombinu yake, na kwamba huwezi kuwa na watalaam wa maji ambao hawana uhakika na afya zao, hivyo ameagiza kutolewa kwa Sh.milioni 251 kwa ajili ya zahanati hiyo ambapo Katibu Mkuu Wizara hiyo ameahidi Jumanne ya wiki inayokuwa atakabidhi fedha hizo kwa chuo hicho.
Wakati huo huo Aweso amewahimiza watumishi wa sekta ya maji kufanya kazi kwa weledi na kujituma huku akiwapa salamu wale wote ambao wamekuwa na mawazo ya kukwamisha sekta ya maji kwamba watambua mwisho wao umefika kwani hawatavumiliwa.
"Pia kuna wale ambao wenyewe wapo kwa ajili ya kutafuta fedha za miradi ya maji, naambiwa wajiandae kuondoka na hawana nafasi katika sekta ya maji.Waache kuchezea fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maji, ni bora wakachezea videvu au vitambi vyao lakini si kucheza na fedha zinazotolewa kwa ajili ya kutatua changamoto katika sekta hii ya maji,"amesema Aweso.
Amefafanua anatambua kuna changamoto ya kubwa ya kukosena wazalendo katika sekta ya maji, baadhi ya watalamu wababaishaji pamoja na wahandisi washauri wasiokuwa waaminifu, hivyo Serikali kupitia Wizara ya Maji imeweka mkakati wa kushughulika na chongamoto moja baada ya nyingine.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Dk.Adam Karia alitumia mahafali hayo kueleza changamoto zinazoikabili chuo hicho ambazo Waziri wa Maji alizitolea majibu huku akitoa maelekezo ya kwamba chuo hicho pia kiwepe miradi mitano ya maji ambayo wataisimamia wao kwani uwezo huo wanao.
Awali akielezea mahafali hayo, Naibu Mkuu Taaluma katika Chuo hicho Dk.Yona Kimori ameeleza jumla ya wahitimu 529 wamefuzu ba kutunukiwa vyeti baada ya kuhitimu ngazi mbalimbali za masomo katika Chuo cha Maji na kwamba mahafali hayo ni ya 12 katika mwaka 2019/2020.
Amefafanua wahitimu 14 ni Astashahada ya msingi ya uhandisi wa usambazaji wa maji na usafi wa mazingira wahitimu, wahitimu watatu ni wa Astashahada ya msingi ya teknolojia ya maabara na ubora wa maji wahitimu watatu na Mhitimu mmoja ni wa Astashahada ya msingi ya uhandisi umwagiliaji.
Pia amesema wahitimu watatu ni wa Astashahada ya uhandisi wa usambazaji mji na usafi wa mazingira ,wahitimu 170 ni wa Astashahada ya uhandisi wa usambazaji wa maji na usafi wa mazingira, wahitimu 26 ni wa Stashahada ya hydrojiolojia na uchimbaji wa visima wahitimu, wahitimu 15 ni wa Stashahada ya haidrolojia na mateorojia.
Aidha Dk.Kimori amesema wahitimu 107 ni Stashahada ya teknolojia na ubora wa maji, wahitimu 37 ni wa Stashahada ya Uhandisi Umwagiliaji wahitimu 37 na wahitimu 153 wamehitimu Shahada ya uhandisi wa rasilimali za maji na umwagiliaji.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...