Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Klabu ya Soka ya Simba imeanzisha Mashindano maalum kwa ajili ya kujiandaa na Michuano ya Kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya Makundi yatakayoanza Februari mwaka huu wa 2021.
Kupitia Mkutano wake na Waandishi uliofanyika jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo, Barbara Gonzalez amesema Simba SC imealika wageni watakaoshiriki Mashindano hayo ambao ni timu za TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Al Hilal ya Sudan.
Barbara amesema mashindano hayo yataanza Januari 27 siku ya Jumatano kwa mchezo mmoja wa ufunguzi majira ya Saa 11 kati ya wenyeji Simba SC dhidi ya Al Hilal, siku ya Ijumaa Al Hilal dhidi ya TP Mazembe mchezo wa mwisho Simba SC watacheza na TP Mazembe ambapo utakuwa mchezo wa kufunga mashindano hayo.
“Tunategemea Kikosi chetu kuingia kambini kesho Jumamosi kabla ya hapo tutatangaza Kocha Mkuu wa Kikosi chetu ambaye atakuja na Wasaidizi wake wawili ambaye pia watasaidiana na Kocha Msaidizi Suleiman Matola katika majukumu yao ya kazi”, amesema Barbara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Klabu hiyo, Haji Manara amesema kutakuwa na sherehe za ufunguzi na kufunga Mashindano hayo, Manara amesema lengo kubwa la Mashindano hayo mahsusi kujiandaa na Mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya Makundi ambayo Simba SC inashiriki.
“Wana Simba pokeeni Mashindano haya, Timu zinazokuja ni timu kubwa sana barani Afrika, TP Mazembe inakuja hapa sio timu ndogo Afrika, imeshiriki sana Ligi ya Mabingwa na kutwaa Taji la Michuano hiyo zaidi mara tano sambamba na Al Hilal ya Sudan imeshiriki Mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara nyingi sana”, amesema Haji Manara.
“Lengo kubwa mwaka huu kufika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na lengo Mama, kwetu ni kutwaa Taji la Ligi Kuu Soka Tanzania Bara msimu huu sambamba na Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC)”, ameeleza Manara.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba SC, Barbara Gonzalez akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Dar,kuhusu Klabu hiyo kuanzisha Mashindano maalum kwa ajili ya kujiandaa na Michuano ya Kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya Makundi yatakayoanza Februari mwaka huu wa 2021,Barbara amesema Simba SC imealika wageni watakaoshiriki Mashindano hayo ambao ni timu za TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Al Hilal ya Sudan.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Klabu hiyo, Haji Manara akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani),leo jijini Dar kuhusiana na sherehe za ufunguzi na kufunga Mashindano hayo, amesema lengo kubwa la Mashindano hayo mahsusi ni kujiandaa na Mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya Makundi ambayo Simba SC inashiriki.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...