Mgeni rasmi katika kilele cha #SimbaSuperCup, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akimkabidhi nahodha Mohamed Hussein kombe la ubingwa wa SIMBA SUPER CUP 2021 🏆

Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

NI Mashindano madogo lakini yalionekana kuwa makubwa kutokana na ujio, ushiriki wa timu kubwa barani Afrika, hapa nazizungumzia TP Mazembe Englebert ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Al Hilal SC ya Sudan pamoja na uwepo wa wenyeji wa Mashindano hayo, Mabingwa wa Tanzania, Simba SC.

Ujio wa timu hizi zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika tena hatua ya Makundi imedhihirisha ukongwe na ukomavu wa Soka la Tanzania katika usimamizi na uongozi ili kuleta ustawi na mafanikio katika Klabu binafsi. Katika hili Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez amefanya jitihada kubwa sambamba na Menejimenti yote ya Klabu hiyo, Kualika timu za TP Mazembe, Al Hilal SC si jambo la kawaida.

Tunafahamu Simba SC inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua ya Makundi, ujio wa timu za hizo kubwa barani Afrika kumedhihirisha Simba SC inajiandaa vizuri na ushiriki wa Michuano hiyo mikubwa barani Afrika ikiwa Kundi moja na timu za Al Ahly SC ya Misri, AS Vita Club ya DR Congo na El Marreikh ya Sudan.

Timu za TP Mazembe, Al Hilal SC zote zinashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, tena wapo Kundi moja, bila shaka wao kwa wao wamepeana mazoezi kabla ya kwenda kuchuana kwenye Michuano husika ya CAF CL inayotarajiwa kuanza Februari 12-13, 2021.

Simba SC wameileta TP Mazembe ambayo inacheza Ligi moja na AS Vita Club kule DR Congo (LinaFoot) sambamba pia na Al Hilal inayocheza Ligi moja na El Merreikh kule Sudan. Hapo Simba SC imelenga kitu kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Malengo yao makubwa ni kufika Nusu Fainali ya Michuano hiyo. Naam! tunamini kwa maandalizi haya watafika mbali.


KUONDOKA KOCHA SVEN KIKOSINI SIMBA SC

Simba SC baada ya kufuzu Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Aliyekuwa Kocha wao, Sven Vandenbroeck aliondoka Kikosini hapo mara moja na Simba SC wakaachwa njia panda, hawajui hili wala lile ijapokuwa walifuzu hatua hiyo ya Makundi.


UJIO WA KOCHA MPYA KIKOSINI

Haikuwa rahisi kwa Simba SC kuzoea mazingira ya kuondokewa na Kocha wao mpendwa mwenye Mifumo kabambe pale Uwanjani, Kocha Sven lakini yote yalipita na kuletwa Kocha mpya Mfaransa Didier Gomes Da Rosa ambaye naye alitoka katika Kikosi cha El Merreikh ya Sudan ambayo nayo imefuzu Makundi ya CAF CL ikiwa Kundi moja na Simba SC (Hii inaitwa Piga Nikupige).


Kocha Didier Da Rosa amepewa nafasi kuwafahamu zaidi Wachezaji wake kupitia Mashindano ya Super Cup ambayo pia yatamsaidia Kocha huyo kujiandaa na Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika kuwakabili Al Ahly, AS Vita na El Merreikh kwa ujumla na maandalizi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam Sports Federation Cup (ASFC).


WACHEZAJI WA SIMBA SC KUPATA UZOEFU KUPITIA SUPER CUP

Wapo wale waliosajiliwa kwa lengo ya Ligi ya Mabingwa Afrika akina Junior Lukosa, Peter Muduhva sambamba na baadhi ya Watu wa Benchi la Ufundi kama Mtathmini watakaokuwepo kuangalia katika kipindi chote ambacho Simba SC inashiriki Michuano hiyo.

Wapo kina Perfect Chikwende ambao tunaambiwa atakuwa katika Ligi Kuu Soka Tanzania Bara pekee kutokana Kanuni na Sheria za CAF kutoruhusu kucheza Michuano ya Ligi Mabingwa katika timu mbili tofauti ndani ya msimu mmoja.


USHINDANI NDANI YA SIMBA SUPER CUP

Si mchezo Simba SC imedhirisha kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, viwango vya Wachezaji wake si mchezo mchezo, angalia kina Rally Bwalya mechi ya kwanza dhidi ya Al Hilal mpaka kuibuka Mchezaji Bora, angalia Bernard Morrison (Mzee wa Busha) ni viwango vya hali ya juu. Simba SC ilibuka na ushindi wa bao 4-1 katika mchezo wake wa kwanza wa Mashindano ya Super Cup 2021.

Mchezo wa Pili dhidi ya TP Mazembe mchezo wa mwisho wa kufunga mashindano hayo ya Super Cup, Simba SC walitoka sare ya 0-0 na Miamba ya Soka kutoka DR Congo. Hivyo kumaliza mashindano na alama nne, wakifuatiwa na Al Hilal SC wenye alama tatu na TP Mazembe wenye alama moja.

Mchezaji Bora wa Mashindano ni Kiungo wa SIMBA SC, Rally Bwalya ambaye ameondoka na kitita cha Shilingi Milioni 2 za Kitanzania wakati Golikipa Bora akiwa ni Beno Kakolanya wa Simba SC aliyeruhusu bao moja katika dakika 180 ameondoka na Shilingi Milioni Moja na Mfungaji Bora ni Bernard Morrison ni Mshambuliaji wa Simba SC mwenye mabao mawili ameondoka na kitita cha Shilingi Milioni Moja. 









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...