Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA)
Bibi Immaculata Senje akieleza jambo kwa
wananchi walionufaika na MKURABITA kupitia urasimishaji ardhi, biashara na
makazi katika Halmashauri ya Mji wa Njombe mkoani Njombe wakati wa ziara
ya Kamati hiyo.
Wananchi walionufaika
na urasimishaji ardhi, biashara na makazi katika Halmashauri ya Mji wa Njombe
mkoani Njombe wakifuatilia hotuba ya
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA, Mhe. Balozi (Mstaafu)
Daniel Ole Njoolay wakati wa mkutano kati yao na kamati hiyo mjini Njombe
kilicholenga kujionea hatua zilizofikiwa baada ya urasimishaji.
Na Mwandishi Wetu- Njombe
WAFANYABIASHARA na wakulima waliorasimisha biashara, ardhi na makazi yao katika Halamashauri ya Mji wa Njombe, wametumia hati za hakimili za kimila kukopa zaidi ya Shilingi bilioni 3.1 katika taasisi za fedha zikiwemo benki za NBC, CRDB, NMB na Benki ya Posta kati ya mwaka 2018 na 2020.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) kutembea wanufaika wa Mpango huo leo Januari 29, 2021, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Balozi (Mstaafu) Daniel Ole Njoolay, amesema Halmashauri ya Mji wa Njombe ni mfano bora wa kuigwa na halmashauri nyingine kwa namna ilivyotekeleza kikamilifu dhana ya urasimishaji hali iliyowawezesha wananchi kupata mikopo katika taasisi za fedha baada ya urasimishaji tasilimali zao na kupata hati za hakimiliki za kimila.
“Viwanja zaidi ya elfu 10 vimepimwa hapa katika Mji wa Njombe na hii ni ishara kuwa urasimishaji umekuwa na matokeo chanya, hivyo nawapongeza wananchi na viongozi wa Njombe kwa kutumia fursa hii iliyoletwa na MKURABITA,” alisema Njoolay.
Amesema kila halmashauri ina jukumu la kutenga bajeti kila mwaka ili kutekeleza dhana ya urasimishaji kwa vitendo hali itakayowawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kwa kutumia rasilimali zilizopo ikiwemo ardhi na biashara zao.
Mratibu wa MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe, amesema maafisa biashara kote nchini wanalo jukumu la kuwaelimisha wananchi kuhusu namna bora ya kuendesha biashara zao huku wakitumia huduma za vituo jumuishi vya biashara vilivyopo katika kalmashauri kama Njombe Mji hali itakayokuza biashara zao na kuongeza tija.
“MKURABITA ilijenga uwezo kwa Halmashauri ya Mji Njombe na sasa imeonesha mfano kwa kuendeleza dhana hii ya kuwawezesha wananchi kupitia rasilimali zao ikiwemo ardhi na tayari matokeo chanya yameanza kuonekana kupitia kwa wajasiriamali hapa Njombe nah ii ndiyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano,”alisisitiza Dkt. Mgembe.
Mmoja wa wanufaika wa urasimishaji ardhi katika Halmashauri ya Mji wa Njombe Bibi Lucy Yona Kitavile anayemiliki kiwanda cha Mama Seki Group Ltd kinachoongeza thamani mahindi kwa kuzalisha unga amesema kuwa baada ya urasimishaji ardhi alianza kukopa shilingi laki 4 hadi sasa ameweza kukopa milioni zaidi ya 400 zilizomuwezesha kuanzisha kiwanda hicho mwaka 2019.
“ Kwa siku kiwanda changu kinazalisha unga tani 30 hivyo niwashauri akinamama wote kujituma na kutumia fursa zinazotokana na urasimishaji kujikwamua kiuchumi ikiwemo kuanzisha viwanda vidogo”, alisisitiza Bi. Kitavile
Akieleza zaidi amesema kuwa MKURABITA imewezesha wananchi waliorasimisha biashara na mashamba yao kujikwamua kiuchumi baada ya kupata mikopo katika Taasisi za fedha.
Halmashuri ya Mji wa Njombe ni moja
ya Halmashauri zilizonufaika na mpango wa urasimishaji wa biashara,makazi na ardhi
hapa nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...