WATU 64 waliokuwa wamezamia nchini Afrika Kusini wametiwa hatiani mbele ya Mahakimu wawili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na wamehukumiwa kulipa faini ya sh. laki nane ama la kutumikia kifungo cha mwaka mmoja na nusu gerezani.
Watuhumiwa hao wametiwa hatiani kwa kosa la kutoka nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kuwa na kibali.
Hukumu hiyo imesomwa leo Januari 25, 2021 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi na Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustina Mbando baada ya washtakiwa hao kukiri shitaka linalowakabili.
Akisoma hukumu kwa washtakiwa 32 kati yao, Hakimu Shaidi amesema, kosa la kutoka nje ya nchi bila kibali sheria imeeleza wazi adhabu yake ni kifungo kisichopungua mwaka mmoja gerezani na faini isiyopungua laki tatu au vyote kwa pamoja.
"Hakuna familia ambayo iko tayari kumlisha mtu bure hivyo mnahitaji maandalizi ya kwenda mtaani kupambana na maisha, pamoja na maelezo yenu kuomba mpunguziwe adhabu, Mahakama imewatia hatiani na mnahukumiwa kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Shilingi laki tano," amesema Hakimu Shaidi.
Kwa upande wake hakimu Mmbando amewahukumu washitakiwa wengine 32, kwenda jela miezi sita au kulipa faini ya Shilingi 300,000 kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kutoka nje ya nchi bila kibali.
Mapema kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo Wakili Shija Sitta amedai kuwa, washtakiwa hao wamekiri wenyewe kutenda kosa na kuisababishia Serikali hasara katika kuwarudisha nchini ni vyema mahakama iwape adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.
Washtakiwa hao wanadaiwa, Januari 22,2021 katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere ulioko Ilala Jijijini Dar es Salaam,washitakiwa hao wakiwa ni raia wa Tanzania walikutwa uwanjani hapo wakirejea kutoka Afrika ya Kusini bila kuwa na kibali.
"Januari 22, walipelekwa katika ofisi za Uhamiaji zilizopo Kurasini Jijini Dsm ambapo walichukuliwa maelezo ya awali na kabla ya kufikishwa Mahakamani kujibu shitaka lililoko mbele yao.
Miongoni mwa washitakiwa hao ni Frank Martine, Abdullah Kujali, Feisal Mnakoma, Ally Bashuti, Ally Mputo, Mtoro Mohamed, Omar Mpoki, Hussein Mnywmani, na Ally Zuh.
Wengine ni Martin Mwerela,Limbinda Kapondo,Andrew Makule, Ramadhan Mtopela,Shukuru Totoro,Saray Both na Jabir Sobo.
Hata hivyo baadhi ya washtakiwa wamefanikiwa kukwepa kifungo baada ya kufanikiwa kulipa faini na wengine kwenda jela kufuatia ndugu zao kutokuwepo Mahakamani hapo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...