Charles James, Michuzi TV

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe ametolea ufafanuzi suala la mpango wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kukagua bidhaa na magari hapa nchini badala ya magari hayo kukaguliwa kwenye nchi ambazo yamekua yakiagizwa.

Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma leo, Waziri Mwambe amesema hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa na utaratibu wa kukagua magari yanayoagizwa nje ya Nchi kwani miaka ya 2003 na 2004 utaratibu huo ulikuepo.

Mwambe amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa TBS kuingia mkataba na Chuo cha Usafirishaji na VETA ili kuwapata watalaamu kutoka kwenye taasisi hizo ambao watapatiwa mafunzo na baadae kuajiriwa kwenye vituo vya ukaguzi wa magari hayo.

Amesema kuanzia Machi mwaka huu magari yote yanayoagizwa nje ya nchi yatakua yanafanyiwa ukaguzi na yatayobainika kuwa na shida yatapelekwa kwenye Gereji za hapa hapa nchini kabla ya kukaguliwa tena ndipo yapatiwe leseni na usajili wa namba kutoka TRA.

" Niwahakikishie kama Serikali tumejipanga kwenye hilo, tayari tumeshaagiza vifaa maalum vya kisasa nchini Ujerumani ambavyo vitafika hivi karibuni na wataalam wetu watapatiwa mafunzo kabla ya kuanza kazi rasmi.

Magari yatakayoonekana kuwa na shida yatapelekwa kwenye gereji zetu kisha yatakaguliwa tena kabla ya kupewa leseni, na vifaa vyetu vina uwezo wa kukagua gari moja kwa muda wa dakika 15," Amesema Mwambe.

Amesema kupitia uamuzi huo wa kukagua magari hapa nchini itasaidia kupunguza tatizo la ajira nchini kwani vijana kutoka vyuo vya NIT na VETA watachukuliwa lakini pia Serikali itapata mafuta kwani zile bei za ukaguzi zilizokua zikilipwa kwenye nchi hizo zitalipwa hapa kwetu na zaidi tutakua na uhakika wa kuletewa magari yenye ubora kwani wakileta gari zilizo chini ya ubora watakua wanajiharibia soko wenyewe, " Amesema Mwambe.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora TBS, Lazaro Msasalaga amesema wanatarajia vifaa hivyo kuingia nchini Februari 15 na wataalamu wao wapatiwa mafunzo kabla ya kuanza kwa kazi hiyo.

" Wataalamu tayari wameanza kuripoti jijini Dar es Salaam tunaamini utaratibu utakua mzuri hivyo watanzania wasiwe na wasiwasi na chombo chao," Amesema Msasalaga.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma leo alipokua akizungumzia suala la serikali kukagua magari yanayoagizwa kutoka nje ya Nchi.
Mkurugenzi wa Udhibiti na Ubora TBS, Lazaro Msasalaga akielezea namna ambavyo wamejipanga kufanya ukaguzi wa magari ambayo yanawasili nchini.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...