Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
KATIKA jitihada za kuunga mkono kazi za Wasanii nchini Tanzania, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel kwa kushirikiana na Bodi ya Filamu, Shirikisho la Filamu nchini sambama na Wasambaji wa kazi hizo wamezindua rasmi Airtel TV App lengo ikiwa ni kukuza kazi za Wasanii na kuongeza kasi katika usambazaji.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini, Dkt. Kiagho Kilonzo amesema Kampuni ya Airtel imeunga mkono usambazaji wa Filamu nchini na wao wanaunga mkono Mfumo huo wa usambazaji kupitia Airtel TV App.
“Airtel ni wasambazaji wapya wa Filamu nchini, tulikuwa tunatumia mfumo wa zamani wa Analojia kwa sasa tunaenda kwenye Digitali tunashukuru Airtel wametuunga mkono”, amesema Dkt. Kilonzo.
Dkt. Kilonzo amesema ukuaji wa Soko la Filamu nchini umekuwa kwa kasi kupitia Mitandao mbalimbali, amesema Mtandao wa Simu za Mkononi wa Airtel umeleta chachu katika usambazaji wa Filamu hizo.
“Mwaka jana (2020) Sekta ya Filamu imezalisha Ajira si chini ya Elfu 25, kwa Filamu ya Panguso peke yake imezalisha ajira za Watu 200. Miaka ya nyuma sura zilikuwa sasa hivi sura mpya kwa kweli zinafanya vizuri”, amesema Dkt. Kilonzo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano amesema Kampuni ya Airtel imeleta fursa kwa Wasanii kuonyesha na kuuza kazi za Wasanii nchini.
Singano amesema Airtel TV App itawasaidia Wasanii wa Tanzania kutokana na App hiyo kupatikana popote, amesema Wasanii watapata pato zaidi kupitia Filamu zao pale inapoangaliwa zaidi kupitia App hiyo.
“Tutafanya kazi na Serikali tunawashukuru sana COSOTA na BASATA katika kusimamia misingi na kuwalinda Wasanii wa ndani, na sisi tutahakikisha kazi zinazoletwa katika Airtel App TV zina ubora, kuzingatia utaratibu wa Bodi ya Filamu maudhui yake na kufuata misingi ya Vyombo mbalimbali vinavyosimamia Sanaa nchini”, amesema Singano.
Naye Rais wa Shirisho la Filamu Tanzania, Elia David Mjatta ameishukuru Airtel Tanzania kutambua umuhimu wa Filamu za Tanzania, amesema Shirikisho hilo lipo tayari kufanya kazi na Taasisi yeyote hapa nchini.
“Sisi tunaenda kuwaambia Wasanii kuwa kuna Airtel TV App ambayo mtaweza kuweka kazi zenu, kusambaza na kuuza sehemu mbalimbali kupitia hiyo App ya Airtel, tutatoa elimu ili wachangamkie fursa”, amesema Mjatta.
Mwenyekiti wa Chama wa Wasambazaji wa Filamu nchini, Athuman Juma amesema watashirikiana na Bodi ya Filamu na Kampuni ya Airtel kuhakikisha kazi za Wasanii zinasambazwa ipasavyo na Wasanii hao kupata faida kupitia kazi zao.
Wasanii wataweka kazi zao kupitia www.airteltv.co.tz ambayo kazi itatolewa bure.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano akionyesha Mfano wa APP ambayo inatumika kuweka Filamu za Wasanii mbalimbali nchini kupitia www.airteltv.co.tz aliyeshika kutoka Kulia ni Rais wa Shirisho la Filamu Tanzania, Elia David Mjatta na anayeshuhudia ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini, Dkt. Kiagho Kilonzo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...