Na Mwandishi wetu, Mbulu
MKAZI
wa Kijiji cha Ngwandakw Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, Rose Danielson
aliyepigwa na ofisa mtendaji wa Kijiji cha Haydom, Adela Kente
amehukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela au kulipa faini ya sh200,000
na fidia ya sh100,000.
Hata
hivyo, mtendaji huyo wa kijiji hicho cha Haydom Adela baada ya kumpiga
Danielson alisimamishwa kazi na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga kwa kudaiwa kupigana hadharani kinyume na
utumishi wa umma.
Rose
amesema hukumu hiyo imetolewa juzi alasiri kwenye mahakama ya mwanzo
Dongobesh, baada ya kukutwa kwenye eneo la kazi na kisha kupigwa kwenye
sikukuu ya mapinduzi ya Zanzibar Januari 12 mwaka huu.
"Nililala
ndani nikanyimwa karatasi ya matibabu na kunyimwa dhamana kisha
nikafunguliwa mashtaka mahakamani ili hali mimi ndiye ambaye nilipigwa
na huyo mtendaji wa kijiji," amesema Rose.
Hata
hivyo, Rose amesema atashirikiana na taasisi za haki za binadamu ili
akate rufaa kwenye mahakama ya wilaya hiyo kwani alipigwa na mtendaji
huyo kisha yeye akashtakiwa mahakamani.
Amesema
baada ya yeye kupigwa na kujeruhiwa na Adela alitegemea angeshtakiwa
lakini haikuwa hivyo ila yeye ndiye ameshitakiwa mahakamani na
kuhukumiwa.
"Ninamshukuru
mbunge wa jimbo Flatei Maasay kwani nilipopigwa nilikosa msaada na pia
namshukuru Mkurugenzi wa halmashauri Kamoga kwa kumsimamisha kazi Adela
baada ya kunipiga," amesema Rose.
Amesema
yeye hakuwa mkazi wa kijiji cha Haydom anaishi kijiji cha Ngwandakw'
amepigwa kutokana na kudaiwa mchango wa madawati na kisha kushtakiwa
hivyo anauliza haki ipo wapi.
Amesema
baada ya kupigwa na mtendaji huyo japokuwa alimweleza kuwa yeye hapaswi
kulipa mchango huo kwani siyo mkazi, alilazwa siku mbili kituo cha
polisi na alinyimwa dhamana na hakupewa fomu namba tatu ya matibabu
(PF3).
Amesema baada ya
kupambaniwa na ndugu zake na kupata matibabu hospital ya Haydom
alipelekwa mahakamani na kisha kushtakiwa kwa kumpiga Adela.
"Tulipeleka
washahidi wanne mahakamani wakatoa ushahidi wao kwenye chumba kimoja
ila haukuzingatiwa na siku hiyo hiyo baada ya ushahidi kutolewa baada ya
saa moja hukumu ikatolewa sehemu ya wazi, " amesema Rose.
Amesema
Adela alikuwa anatamba kuwa "Hawa wamburu hawataniweza subirini hukumu
nitashinda na kazini nitarudi niwanyooshe vizuri."
Akisoma
hukumu ya kesi hiyo ya jinai namba 10 ya mwaka 2020, hakimu wa mahakama
ya mwanzo Dongobesh, Julliet Mbise amesema Rose ametenda kosa la
shambulio la kuzuru mwili Januari 12 mwaka 2021.
Rose
alilipa faini ya sh200,000 na fidia ya sh100,000 kwa Adela hivyo
kuepuka kwenda magereza kutumikia kifungo cha miezi mitatu jela.
Mwishoni
mwa mwezi Januari mwaka huu ilizunguka 'clip' kwenye mitandao ya
kijamii ikimuonyesha Adela akimpiga Rose kwa kile alichosema kutotoa
mchango wa kununua madawati ya shule.


********************************
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...