Na Muhidin Amri, Madaba
HALMASHAURI ya Madaba wilayani Songea, imefanikiwa kupeleka watoto
wote 1148,waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka jana
na kuchaguliwa kuanza elimu ya sekondari katika muhula wa masomo 2021
kwenye shule walizopangiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Afisa Elimu sekondari wa
Halmashauri hiyo Michael Hadu alisema, wamefanikiwa kupeleka watoto
wote walio kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari mwaka huu baada
ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Hadu alisema, kati ya wanafunzi hao wavulana 585 na Wasichana 563
ambapo wanafunzi 10 wamechaguliwa kwenda katika shule mbalimbali za
Bweni za serikali zilizopo nje ya Halmashauri ya Madaba.
“ katika Halmashauri yetu ya Madaba tumefaulisha wanafunzi 1148 na
wote wamepata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule
walizopangiwa na hakuna mwanafunzi aliyekosa nafasi na wote wako
shuleni”alisema Hadu.
Alisema, Rais Dkt John Magufuli ameweka dhamira ya dhati ya kutoa
elimu bure, na Halmashauri imehakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa
wanaendelea na elimu ya sekondari ambapo ameipongeza Serikali kwa
kutoa fedha za kujenga madarasa mapya kwa ajili ya wanafunzi hao.
Kwa upande wa vyumba vya madarasa alisema, mahitaji kwa wanafunzi hao
ilikuwa 25 na wakati wanachaguliwa kulikuwa na vyumba 23 hivyo kuwa
na upungufu wa vyumba 2,hata hivyo darasa moja limekamilika
lililojengwa kwa ushirikiano kati ya wananchi na Halmashauri.
Alisema,darasa lingine lipo katika hatua ya boma ambapo Ofisi ya
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya imeshatoa kiasi cha
shilingi milioni 6 ili kukamilisha ujenzi wake.
Kuhusu mahitaji ya viti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2021
ilikuwa 1148,vilivyokuwepo 987 na pungufu 161,mahitaji ya meza 1148
zilizowepo 976 hivyo kuwa na upungufu wa meza 172.
Hata hivyo, kutokana na uhusiano mzuri kati ya Halmashauri na wadau
mbalimbali, ikiwemo Benki ya NMB Tawi la Madaba iliyotengeneza viti
50 na meza 50 na Halmashauri imetoa shilingi milioni 10 ambazo
zimesaidia kumaliza upungufu huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Shafi Mpenda,
ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha ambazo zimetumika kuboresha sekta
ya elimu mwaka hadi mwaka.
Alisema, Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 299.678 kwa ajili
ya kutekeleza miradi ya P4R kwa kujenga vyumba vya madarasa,matundu
ya choo kwa baadhi ya shule.
Alieleza kuwa,changamoto kubwa katika utekelezaji wa miradi ni
kuchelewa kwa vifungu vya matumizi ya fedha,saruji kutopatikana kwa
wakati,ukiukaji wa maadili katika matumizi ya fedha na uzembe kwa
walimu uliosababisha baadhi ya miradi kuchelewa kukamilika.
Alisema, kutokana na kasoro hizo amelazimika kuwavua madaraka walimu
waliofanya uzembe na kutumia fedha hizo vibaya, na hatua hiyo
inalenga kujenga nidhamu juu ya matumizi ya fedha za miradi.
Mpenda alitoa mfano wa Mkuu wa shule ya Sekondari Gumbiro aliyemlipa
fedha nyingi fundi aliyepewa kazi ya kujenga matundu ya vyoo katika
shule hiyo kupitia fedha za mradi wa ujenzi wa vyoo bora unaofahamika
kwa jina la Swash kuliko kazi iliyofanyika ambapo amemtaka Mwalimu
huyo kumalizia kazi hiyo kwa gharama zake.
Katika hatua nyingine Mpenda alisema, Halmashauri hiyo imetekeleza
agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa lililowataka Wakurugenzi wa
Halmashauri za wilaya,miji,Manispaa na Majiji kumaliza ujenzi wa
vyumba vya madarasa, madawati na viti kwenye shule za sekondari
ifikapo tarehe 28 Mwezi uliopita.
Mpenda alibainisha kuwa, Halmashauri kwa kushirikiana na wadau
wengine wa elimu imekamilisha agizo hilo kwa asilimia 100 na hakuna
mtoto anayekaa chini kwa kukosa kiti na meza au kusoma chini ya miti.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...