KUTOKANA na wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kuongoza kwa maambukizi
makubwa ya ugonjwa wa kifua mkoani Ruvuma,Hospitali ya wilaya yaTunduru
kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma imeanza kampeni ya kudhibiti
ugonjwa huo kwa kutoa elimu ya uelimishaji na uchunguzi wa vimelea vya
ugonjwa huo kwa wahudumu wote wa Bar.
Mratibu wa kifua kikuu na Ukoma wa wilaya hiyo Dkt Mkasange Kihongole
amesema, wamelazimika kuwafikia wahudumu wa Bar kwa kuwa ni kati ya
makundi hatarishi kutokana na kuishi na kufanya kazi kwenye mikusanyiko
na kukutana na watu wengi mara kwa mara.
Alisema, katika kampeni hiyo inayojulikana kwa jina la Kilinge kwa
kilinge,nyumba kwa nyumba na shule kwa shule wanatarajia kuzifikia
Bar,Grocery na vilabu vyote vinavyouza pombe kwa ajili ya kutoa elimu
na kufanya uchunguzi wa ugonjwa huo kwa watoa huduma na watu wengine
watakaokutwa katika maeneo hayo.
Dkt Mkasange ametoa kauli hiyo jana wakati akizindua rasmi elimu ya
uhamasishaji, uelimishaji na uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa kifua
kikuu kwa wahudumu wa Bar wilayani Tunduru uliofanyika katika Bar
maarufu ya Laprasido wilayani humo.
Alisema, mbali na wahudumu wa Bar makundi mengine yalioko katika hatari
ya kupata ugonjwa wa kifua kikuu ni wasafiri,wanywa pombe
kupindukia,wazee,wanafunzi wanaoishi bweni,watu wanaofanya shughuli zao
kwenye misongamano na wafugaji.
Alitaja watu wengine wanaoweza kupata kifua kikuu kwa urahisi ni wale
wote wenye magonjwa yanayosababisha kushuka kwa kinga mwilini kama
ukimwi,kisukari,kansa,utapiamlo kwa watoto na watu wazima,wasio na
makazi maalum ambao wanalazimika kulala zaidi ya watu watano katika
sehemu moja,umaskini au hali duni ya kipato na wanaotumia dawa bila
kupata ushauri wa mtaalam.
Alisema, TB ni ugonjwa unaoenea kwa njia ya hewa kutoka kwa mtu mwenye
vimelea vya ugonjwa huo ambaye hajaanza tiba kwenda kwa mtu mwingine
kwa kupiga chafya, kutema mate ovyo au makohozi.
Alisema, vimelea vya TB kwa kawaida ushambulia mapafu na vina uwezo wa
kushambulia viungo vyote vya mwili isipokuwa nywele,meno na kucha.
Alitaja dalili za mtu mwenye kifua kikuu ni kukohoa kwa wiki mbili na
zaidi,homa za mara kwa mara kwa wiki mbili na kuendelea,kutokwa jasho
jingi usiku, kukohoa makohozi yenye damu,kupungua uzito,kukosa hamu ya
kula, kwa mtoto kukosa raha na kulia lia,kupungua uzito au kudumaa na
kupumua kwa shida.
Amewataka wahudumu hao kuchukua tahadhari na kuwa na utaratibu wa
kuchunguza afya zao mara kwa mara na kwa wale watakaobainika kuwa na
ugonjwa huo wataanzishiwa matibabu ambayo yanatolewa bure katika
zahanati,vituo vya Afya na Hospitali zote za Serikali hapa nchini.
Aidha, amewashauri wahudumu hao na jamii kuhakikisha watoto wanachomwa
chanjo ya BCG mara baada ya kuzaliwa,kuziba pua na mdomo kwa kitambaa au
mikono unapokohoa au kupiga chafya,kufanya mazoezi mara kwa mara ili
kuimarisha kinga za mwili.
Mkasange alisema,njia nyingine za kujikinga na kifua kikuu ni kula
vyakula vyenye virutubisho vyote muhimu kwa afya bora,kutumia dawa kinga
kwa wale walio kwenye hatari ya kuambukizwa,kuepuka mikusanyiko au
mirundikano ya watu na kuishi kwenye nyumba yenye mfumo mzuri wa hewa.
Baadhi ya wahudumu wa Bar wameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu na
huduma ya uchunguzi kwa wahudumu mara kwa mara kwani itasaidia kuepuka
kupata ugonjwa huo kutoka kwa watu wengine wanaofika katika shughuli
zao.
Emeliana Komba muhudumu wa Bar ya Laparsido alisema,elimu waliyoipata
imewasaidia kufahamu ugonjwa wa kifua kikuu na jinsi ya kuchukua
tahadhari na kuepuka kupata maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu.
Meneja wa Bar ya Terminal Ali Pinde alisema, changamoto kubwa kwa
wahudumu ya Bar ni kukutana na watu tofauti mara kwa mara pamoja na
suala zima la kuishi watu zaidi ya watano katika chumba kimoja.
Picha,Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma
Dkt Mkasange Kihongole akizungumza na baadhi ya wahudumu wa Bar maarufu
ya Laprasido wilayani humo wakati akifungua kampeni ya uelimishaji na
uhamasishaji wa ugonjwa wa kifua kikuu wilayani humo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...