NA Woinde Shizza, michuzi Tv - ARUSHA
UDONGO NI NINI
Udongo ni tabaka dogo la juu ya ardhi ambako mimea huweza kuota, nao hutumiwa kwa kilimo, pia ni mchanganyiko wa vipande vidogo vya mwamba na madini yaliyosagwa pamoja mabaki ya mimea na wanyama yaliyooza, (mboji), pia wadudu na vijidudu vinavyoishi ndani yake.
Udongo huwa pia na hewa na maji ndani yake zinazojaza nafasi kati ya vipande vidogo vya mwamba.
Udongo wenye afya ni msingi katika kilimo, ikumbukwe rutuba ya shamba hupungua kadri tunavyopanda na kuvuna mazao shambani, hivyo ni muhimu kufahamu afya ya udongo shambani ili kuweza kutunza rutuba kwa kilimo endelevu, Mbegu bora, Mbolea bora bila kufahamu afya ya udongo haiwezi kuongeza tija katika kilimo.
Kila mmea ukimea huhitaji virutubisho katika ukuaji, hufika wakati virutubisho hivo hupungua au kuisha katika udongo na kupunguza rutuba ya shamba, Rutuba ikiisha au kupungua hupelekea wakulima wengi kuhamia sehemu nyingine na kuanzisha mashamba mapya na hivyo huchangia katika uharibifu wa mazingira.
Kufahamu afya ya udongo kutawezesha kutambua virutubisho mbalimbali vilivyopo shambani kwako. Hii itasaidia kujua utumie mbolea gani, kiasi gani na wakati gani mzuri wa kuweka mbolea ili kuongeza uzalishaji. Hii itasidia kupunguza gharama kwa kuweka virutubisho sahihi.
WAKULIMA WANAELEWAJE UNAVYOSEMA SWALA LA UPIMAJI WA UDONGO
Mwandishi wa makala hii ameweza kuongea na wakulima kutoka kata ya Musa kijiji cha Likamba wilaya ya Arumeru akiwemo Winifrida Teta ambaye alisema kuwa anafahamu kuwa udongo ndio unaosaidia mmea kukua kwa kushirikiana na maji lakini hajui kuwa kuna umuhimu wa kupima afya ya udongo ili kujua virutubisho vilivyopo.
“Mimi napanda shamba langu kawaida tu sijui kuhusu suala la afya ya udongo kuna wakati napata mazao ambayo naona ni kawaida na kuna wakati sipati kabisa na hilo nalichukulia kuwa ni kutokana na msimu na wakati mwingine tuaambiwa kuwa shamba limechoka kulimwa zao moja kila mwaka,” alisema Winifrida.
Neema Wilson ambaye pia ni mkazi wa kijiji hicho alisema amewahi kusikia upimaji wa udongo lakini hajui kama kuna umuhimu kwani yeye hafanyi kilimo kwaajili ya biashara bali chakula japo kuwa kuna wakati analazimika kuuza mazao yake kwa sababu ya changamoto za maisha.
Alisema katika shamba lake la ekari mbili kila mwaka idadi ya mavuno inatofautiana na alikuwa anaelewa kuwa ni kutokana na hali ya mvua kwa kipindi hicho lakini hakujua kuwa udongo nao unachangia.
“kwa kawaida kwenye shamba langu naweza kupata magunia manne hadi kumi kulingana na msimu na hii ni kwa upande wa mahindi lakini kwa upande wa maharage naweza kupata magunia mawili hadi matano na wakati mwingine kama mvua zikiwa ni ndogo naweza kurudisha mbegu tuu niliyoitumia,”alieleza.
Lomayani Lotha alisema yeye ajawahi kusikia swala linalohusiana na upimaji wa udongo ,na amezoea tu kilimo cha kawaida ambacho walikuwa wanakilima tangu enzi za mababu zao hivyo ,anaona ni vyema wakaelimishwa zaidi kuhusiana na kilimo hiki ,ili nao waweze kulima kilimo cha uhakika chenye kuwapatia mazao mengi yenye ubora na yenye kuleta tija.
MTAALAMU WA UPIMAJI UDONGO AONGEA
Mkurugenzi wa kampuni binafsi inayojishughulisha na upimaji wa udongo kwa wakulima wakubwa, wakati na wadogo (LSSL) Dkt Edmond Matafu alisema kuwa elimu juu ya umuhimu wa afya ya udongo bado haijawafikia wakulima wengi jambo linalowafanya waendelee kufanya kilimo cha mazoea hivyo ni muhimu wakulima kupata elimu juu ya umuhimu wa kupima afya ya udongo ili waweze kulima kwa tija kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla .
Dkt Matafu alisema kuna faida kubwa za kupima udongo moja wapo ikiwa ni kujua aina ya mazao yanayofaa katika shamba la mkulima, kujua virutubishi vilivyopo katika udongo na ni kwa kiasi gani, pamoja na mkulima kununua mbolea kulingana na upungufu wa virutubishi vinavyohitajika kwenye udongo.
“Hii itasaidia kupunguza gharama kwani wakulima wamekuwa wakitumia mbolea hata kwa mashamba ambayo yana virutubisho vya kutosha na wakati mwingine kutumia mbolea isiyofaa kwa eneo husika jambo linaloongeza gharama na kuleta hasara kwa kutokupata mazao ya mimea aliootesha,”Alisema Dr Matafu.
Alifafanua kuwa faida nyingine ni kusaidia kutunza mazingira kwasababu baadhi ya virutubishi vikizidi kwenye udongo huweza kuharibu mazingira na kufanya mimea ya aina yoyote isiweze kuota ambapo mkulima atakapo pima udongo katika shamba lake atajua mahitaji ya mbolea au virutubishi vinavyohitajika na kujua jinsi ya kuboresha udongo huo.
Alieleza kuwa lengo la kuhamasisha upimaji wa udongo ni ili kuwasaidia wakulima wote nchini kujua afya ya udongo hasa tindikali (pH), kujua virutubishi vilivyo katika udongo kabla ya kulima zao lolote na kuwezesha kujua kiasi cha mbolea inayojitajika katika mmea.
“Kwa kupima udongo mkulima atajua virutubishi vilivyoko kwenye udongo Kama vile Naitrojeni, Potasiam, Fosforasi, Salfa pamoja na virutubisho vidogo vidogo ambavyo ni muhimu kwa ukuaji na uzalishaji wa mmea Kama vile boron, zinc, na kuendelea,” Alieleza.
Alifafanua kuwa ni muhimu kwa wakulima kabla ya kulima au kuotesha kujua kujua afya ya udongo wa shamba lake ili kuweza kufanya kilimo chenye tija ambapo anatakiwa kuchukua sampuli ya udongo kwa njia ya kupishanisha (zigzag)na kupeleka katika maabara ili kujua aina ya mbolea na mazao yanayokubali katika eneo hilo.
“Majibu mazuri ya udongo yanatokana na umakini wa uchukuaji wa sampuli katika shamba ambapo anayechukua udongo anatakiwa kuchimba vishimo zaidi ya 15 vyenye kina Kati ya sentimita 15 hadi 20 na kukusanya sapuli hizo toka maeneo mbalimbali ya shamba analotarajia kulima,”alifafanua.
Aliendelea kusema kuwa baada ya kukamilika kwa zoezi la ukusanyaji wa sampuli, udongo huo utapelekwa katika maabara ambapo majibu yake yatatoka baada ya siku kaadhaa lakini pia kuna kifaa cha kupima udongo papo kwa hapo.
“LSSL tuna aina mbili za teknolojia za kupima udongo moja ya papo kwa hapo na nyingine ni ya maabara ambapo hii ndio inayotoa matokeo kwa kina zaidi ikiwa ni pamoja na aina ya mazao yanayofaa katika shamba lakini Kuna maeneo mengine pia majibu yanatoka kuwa hapafai kulima zao lolote na hapa panahitajika jitihada za kurutubisha udongo,” Alisema.
BAADHI YA MADHARA YANAYOWEZA KUTOKEA USIPO PIMA UDONGO
“Kuna madhara unapoweka mbolea mahali pasipo hitajika mbolea mojawapo ikiwa ni kuharibu udongo na kupunguza uzalishaji wa mazao na sisi tunapima udongo ili kusaidia wakulima kuongeza tija ya mazao wanayozalisha,”alibainisha.
MKURUGENZI AELEZA NIA YA KUANZISHA KAMPUNI HII
Akiongelea lengo halisi la kuanzisha huduma hii ya upimaji udongoni ni kutaka kumsaidia mkulima kuweza kulima kilimo cha uhakika na chenye tija,pamoja na kumshauri zao ambalo linaweza kustawi katika ardhi ambayo anataka kutumia kwa ajili ya kilimo
MKULIMA AONGEA NAMNA ALIVYONUFAIKA BAADA YA KUPIMA UDONGO
Mmoja wa wakulima waliopata uelewa juu ya upimaji wa afya ya udongo Antony Mosha kutoka Njombe, Lupembe alieleza tangu alipopima udongo katika shamba amepata manufaa kwani maparachichi anayolima na mahindi yametoa mazao mengi.
Alisema baada ya kufanya vipimo majibu yalionesha kuwa udongo ulikuwa sio mzuri ambapo alielekezwa jinsi ya kurutubisha na hatimaye akafanikiwa.
“Kabla ya LSSL kuja mazao yalikuwa yanaita lakini yanadumaa ila hivi sasa tunapoongea mabarachi yanerefuka na hata nikipanda mahindi yanakuwa mazuri na napata mazao Mengi,” Alisema
Kwa upande wake Fabian Mwambinga mkulima wa zao la maharage kutoka kata ya kikatiti iliopo ndani ya halmashauri ya Arumeru alisema kuwa awali alipoanza kulima alipata hasara kubwa hadi alikata tamaa ya kuendelea na kilimo kwani aliweza kulima maharage katika shamba la hekari tatu na kupata magunia matatu .
‘ ’Nilidhani nikiweka mbolea ndio nitapata mazao mengi lakini nilipokuwa nikienda kununua mbolea ndipo nilipokutana na kampuni hii ya kupima afya ya udongo LSSL ambao walinishauri nipime udongo kwanza kabla ya kulima ndipo wakanipimia na kukuta udongo wangu hauna tatizo la rutuba bali lina tatizo la pH( chumvi chumvi na tindikali)na kunieleza niweke chokaa ya kilimo na baada ya kuweka nilipotesha katika shamba lele lile nilipovuna awali nikapata gunia tatu nilipovuna baada ya kuweka chokaa katika shamba lilelile la eka tatu nilipata gunia 18‘’ alibainisha Mwambinga
WALIOPIMA MASHAMBA NA KUONA FAIDA WANASHAURI NINI
Kupima udongo ni gharama ndogo ukilinganisha na gharama ya kulima hivyo waliwashauri wakulima wenzao kupima afya ya udongo kabla ya kulima ili waweze kupata mazao yatakayoinua uchumi wa familia zao na taifa kwa ujumla pamoja na kuwa na kilimo endelevu chenje tija.
WITO KWA SERIKALI
Imebainika kuwa wakulima wengi hawana elimu ya upimaji wa udongo,na wengine hawajui kabisa kama kuna kitu kinaitwa kupima afya ya udongo hivyo basi serikali itumie maafisa ugani wa kata kuwapa elimu wakulima juu ya umuimu wa upima wa afya ya udongo
Aidha taasisi za kilimo ,mashirika mbalimbali ya kilimo yaendelee kutoa elimu juu ya faida za upimaji udongo kwa kupitia vyombo vya habari pamoja na vikundi vya wakulima vilivyopo vijijni ili elimu hii iendelee kusambaa zaidi.
Picha ikionyesha wakulima wakiendelea kupewa elimu ya upimaji wa udongo Katika vijiji tofauti tofauti.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...