Na Munir Shemweta, WANMM GEITA
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
ametaka kuundwa vikosi kazi kwa ajili ya kuendesha zoezi la upimaji
ardhi katika mikoa ili kuongeza kasi ya upimaji ardhi.
Dkt
Mabula alitoa kauli hiyo leo tarehe 16 Februari 2021 wakati wa ziara
yake ya siku moja katika mkoa wa Geita kukagua utendaji kazi wa sekta ya
ardhi na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi.
Alisema,
katika kuharakisha zoezi la upimaji katika maeneo mbalimbali nchini ni
lazima mikoa kupitia ofisi zake za wilaya kwa kushirikiana na ofisi za
ardhi kuunda vikosi kazi vya upimaji vitakavyopita wilaya moja hadi
nyingine ili kuharakisha upimaji.
Aliongeza
kuwa, cha muhimu ni wakati wa zoezi hilo ni kuangalia ni halmashauri
gani yenye vifaa na iliyo tayari kupimiwa ambapo mkurugenzi wake
atawajibika kuihudumia timu itakayofanya kazi na kubainisha kuwa pamoja
na zoezi hilo kuongeza kasi ya upimaji lakini litasaidia kuondoa
migogoro.
" Tunataka kila
mkurugenzi katika eneo lake ahakikishe anapima maeneo yake kwa kuwa
halmashauri ni mamlaka ya upangaji na tukifanya hivi ndani ya mwaka
mmoja tutakuwa tumepima maeneo mengi" alisema Dkt Mabula.
Aligeukia
suala la utoaji hati za ardhi kwa wamiliki, Dkt Mabula amezitaka ofisi
za ardhi katika halmashauri kuanza kujiwekea malengo ya utoaji hati
ambapo aliweka bayana kuwa kumekuwa na kasi ndogo ya utoaji hati kwenye
baadhi ya halmashauri.
"
Haiwezekani mkoa mzima wa Geita kwa miezi sita uwe umetoa hati 586 pekee
hapa lazima kila ofisi ijiwekee malengo, kila mtumishi wa sekta ya
ardhi awekewe malengo ya kuandaa idadi ya hati kwa siku" alisema Naibu
Waziri Mabula.
Aidha, Dkt
Mabula amezitaka halmashauri kusaidia kutoa elimu kwa wananchi
kuhusiana na zoezi la urasimishaji linalofanywa na makapuni ya upimaji
katika maeneo mbalimbali mkoani Geita
Alisema,
Makampuni ya upimaji katika mkoa wa Geita yamefanya kazi kubwa ikiwa ni
pamoja na kupima maeneo kwa kutumia fedha zake hivyo halmashauri za
mkoa huo zinatakiwa kuwaeleza wananchi umuhimu na faida ya kupimiwa
maeneo yao.
Mwakilishi wa
Kampuni ya Upimaji ya Amboni Land Survey Ngusa Juda alimueleza Naibu
Waziri wa Ardhi Dkt Mabula kuwa, pamoja na kampuni yake kukamilisha kazi
ya upimaji katika maeneo iliyopangiwa likiwemo eneo la Nyalugusu katika
mkoa wa Geita lakini wananchi wameshindwa kulipa fedha kwa wakati na
kuiomba serikali kupitia halmashauri kusaidia kuhamasisha wananchi
waweze kukamilisha malipo.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Wakurugenzi pamoja na Watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za mkoa wa Geita wakati wa ziara yake ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi tarehe 16 Februari 2021. Kushoto kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Geita Fadhili Juma.
Sehemu ya Watendaji wa Sekta ya Ardhi wakimsikiliza
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
(Hayupo pichani) wakati wa ziara ya siku moja kukagua utendaji kazi wa
sekta ya ardhi na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi katika mkoa
wa Geita tarehe 16 Februari 2021.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...