Na Munir Shemweta, WANMM SONGEA
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limewataka wapangaji wa nyumba zake wanaodaiwa
kodi na kushindwa kulipa kutokana na changamoto mbalimbali kufika ofisi za
shirika hilo ili kuangalia namna bora ya kufanikisha kulipa kiasi cha fedha
wanazodaiwa kabla ya kuanza kuchukua hatua za kisheria ikiwemo kuwafukuza
katika nyumba zake.
Meneja Huduma kwa Jamii wa NHC Bw. Muungano Saguya alisema, baada ya Shirika
hilo kuwataka wapangaji wake wanaodaiwa kodi za nyumba zake wawe wamekamilisha
kulipa madeni kufikia januari 30 mwaka huu, wapangaji hao wanaodaiwa wameanza
kuitikia wito huku wengine wakiwa bado hawajakamilisha kulipa malimbikizo
wanayodaiwa.
Akizungumza mbele ya watendaji wa sekta ya ardhi na Wakurugenzi wa halmashauri
za mkoa wa Ruvuma tarehe 24 februari 2021 mkoani Ruvuma wakati wa ziara ya
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula, Bw.
Saguya alisema, ni vizuri wale wadaiwa wenye changamoto za malipo wakaenda
ofisi za shirika zilizopo kila mkoa na kuonana na watendaji wa Shirika hilo ili
kuangalia namna bora ya kulipa madeni yao kwa wakati.
Alisema, Shirika la Nyumba la Taifa lina zaidi ya nyumba 17,000 nchi nzima na
hadi kufikia Januari 2021 linadai malimbikizo ya zaidi ya bilioni 27 kutoka kwa
wapangaji wake ambao wamelimbikiza kodi yao.
"Tulitoa mwezi mmoja hadi tarehe 30 mwezi wa januari ili wadaiwa wote wawe
wameshalipa madeni ya kodi ya nyumba na wale watakaoshindwa wataondolewa katika
nyumba za shirika na kufikishwa katika vyombo vya sheria" alisema Bw.
Saguya.
Alibainisha kuwa baada ya muda waliopewa wadaiwa sugu kuisha shirika limeanza
kufanya uchambuzi wa wadaiwa wote ili kubaini mwenendo wa ulipaji wa
malimbikizo hayo na zoezi hilo linakamilika mwezi huu wa februari 2021 na mwezi
Machi Shirika litaanza kufuatilia wapangaji nyumba hadi nyumba ili kubaini
walioshindwa kulipa na wale wenye changamoto ambazo shirika linaweza kukaa
pamoja kutafuta ufumbuzi.
Kwa mujibu wa Bw. Saguya, Nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa ni za watanzania
wote hivyo mpangaji anayeishi katika nyumba za shirika anapaswa
kulipa kodi kwa wakati kwa lengo la kuliwezesha shirika kujiendesha
lenyewe, kulipa kodi mbalimbali za serikali, kuzifanyia matengenezo nyumba zake
na kujenga nyumba mpya kwa ajili ya watanzania wengine wasiopata fursa ya
kupanga katika nyumba za Shirika.
Aliwashukuru wapangaji wote waliokuwa wanadaiwa ambao wameweza kulipa
kodi kwa wakati baada ya wito wa shirika la nyumba na kusisitiza kuwa
nyumba za NHC ni za watanzania wote milioni 50 hivyo uhalali wa waliobahatika
kupata upangaji unatokana na kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi na kufuata
sheria na taratibu za upangaji.
Aidha, Meneja huyo alieleza kuwa mbali na NHC kupangisha nyumba zake imekuwa
ikishiriki katika upangaji miji na ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati
ikiwemo ujenzi wa hospitali za rufaa za Mwl Nyerere mkoani Mara na ile ya Kanda
ya kusini iliyopo Mtwara.
Meneja Huduma kwa Jamii wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Muungano Saguya akieleza mikakati ya shirika lake wakati wa kikao kazi baina ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na watendaji wa sekta ya ardhi pamoja na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Ruvuma tarehe 24 Februari 2021.
Sehemu ya watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Ruvuma wakimsikiliza Meneja Huduma kwa Jamii wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Muungano Saguya wakati wa kikao kazi baina yao na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula tarehe 24 Februari 2021.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...