Na Woinde Shizza, Michuzi Tv -ARUSHA.
Kampuni inayojishughulisha na upimaji wa udongo kwa wakulima wakubwa,wakati na wadogo (LSSL) imeiomba serikali kupitia maafisa ugani kutoa elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa afya ya udongo.
Akiongea na waandishi wa habari mkurugenzi wa kampuni hiyo Dkt Edmond Matafu alisema kuwa bado wakulima wengi hawana uelewa juu ya afya ya udongo ambayo ndio msingi mkubwa wa kilimo.
Alisema elimu bado haijawafikia wakulima walio wengi hali inayopelekea kutokuona umuhimu wa kupima udongo na kuendelea kulima kilimo cha mazoea kisichokiwa na tija.
Dkt Matafu alieleza kuwa Kuna faida kubwa za kupima udongo moja wapo ikiwa ni kujua aina ya mazao yanayofaa katika shamba la mkulima, kujua virutubishi vilivyopo katika udongo na ni kwa kiasi gani, pamoja na mkulima kununua mbolea kulingana na upungufu wa virutubishi vinavyohitajika kwenye udongo.
“Hii itasaidia kupunguza gharama kwani wakulima wamekuwa wakitumia mbolea hata kwa mashamba ambayo yana virutubisho vya kutosha na wakati mwingine kutumia mbolea isiyofaa kwa eneo husika jambo linaloongeza gharama na kuleta hasara kwa kutokupata mazao ya mimea aliyootesha,”Alisema Dr Matafu.
Alifafanua kuwa faida nyingine ni kusaidia kutunza mazingira kwasababu baadhi ya virutubishi vikizidi kwenye udongo huweza kuharibu mazingira na kufanya mimea ya aina yoyote isiweze kuota ambapo mkulima atakapo pima udongo katika shamba lake atajua mahitaji ya mbolea au virutubisho vinavyohitajika na kujua jinsi ya kuboresha udongo huo.
Alieleza kuwa lengo la kuhamasisha upimaji wa udongo ni ili kuwasaidia wakulima wote nchini kujua afya ya udongo hasa tindikali (pH), kujua virutubishi vilivupo katika udongo kabla ya kulima zao lolote na kuwezesha kujua kiasi cha mbolea inayojitajika katika mmea.
“Kwa kupima udongo mkulima atajua virutubishi vilivyoko kwenye udongo Kama vile, Naitrojen, Fosiforasi, Potasiamu, Salfa pamoja na virutubisho vidogo vidogo ambavyo ni muhimu kwa ukuaji na uzalishaji wa mmea Kama vile boron, zinc, copper, na kuendelea,” Alieleza.
Alifafanua kuwa ni muhimu kwa wakulima kabla ya kulima au kuotesha kujua kujua afya ya udongo wa shamba lake ili kuweza kufanya kilimo chenye tija ambapo anatakiwa kuchukua sampuli ya udongo kwa njia ya kupishanisha (zigzag)na kupeleka katika maabara ili kujua aina ya mbolea na mazao yanayokubali katika eneo hilo.
“Majibu mazuri ya udongo yanatokana na umakini wa uchukuaji wa sampuli katika shamba ambapo anayechukua udongo anatakiwa kuchima vishimo zaidi ya 15 vyenye kina Kati ya sentimita 15 hadi 20 na kukusanya sapuli hizo toka maeneo mbalimbali ya shama analotarajia kulima,”alifafanua.
Aliendelea kusema kuwa baada ya kukamilika kwa zoezi la ukusanyaji wa sampuli, udongo huo utapelekwa katika maabara ambapo majibu yake yatatoka baada ya siku kaadhaa lakini pia kina kifaa cha kupima udongo papo kwa hapo.
“LSSL tuna aina mbili za teknolojia za kupima udongo moja ya papo kwa hapo na nyingine ni ya maabara ambapo hii ndio inayotoa majibu mengi zaidi ikiwa ambayo Ni pamoja na aina ya mazao yanayofaa katika shamba lakini Kuna maeneo mengine pia majibu yanatoka kuwa hapafai kulima zao lolote na hapa panahitajika jitihada za kurutubisha udongo,” Alisema
“Kuna madhara unapoweka mbolea mahalo pasipo hitaji mojawapo ikiwa ni kuharibu udongo na kupunguza uzalishaji wa mazao na sisi LSSL tunapima udongo ili kusaidia wakulima kuongeza tija ya mazao wanayozalisha,”alibainisha.
Kwa upande wake Alen Andrew meneja masoko wa kampuni hiyo alisema kuwa kampuni hiyo inafanya kazi nchi mzima ambapo asilimia kubwa ya wakulima waliojitokeza kupima udongo wao ni kutoka nyanda za juu kusini na katika meneo mengine mwamko bado ni mdogo.
“Hii ni huduma mpya wengi bado hawana uelewa ww umuhimu wa kupima udongo lakini nisisitize kuwa kutumia mbegu Bora na mbolea bila kufahamu afya ya udongo hakiwezi kuleta tija,”Alieleza Alen.
Alieleza ikumbukwe kuwa udongo ndio msingi wa kilimo hivyo wakulima wawekeze kwenye afya ya udongo ili waweze kulima kilimo Bora chenye manufaa kwao na kwa taifa zima.
Alisema teknolojia waliyonayo inauwezo wa kupima udongo kwa haraka zaidi bila kuhitaji kenikali ambapo kwa siku wanaweza kupima sampuli zaidi ya 30.
Meneja masoko wa kampuni ya LSSL Allen Andrew akiwaonesha baadhi ya waandishi wa habari vifaa wanavyotumia kupima afya ya udongo (picha na Woinde Shizza , ARUSHA)
Mtaalam wa maabara ya udongo kutoka kampuni ya LSSL akiwaonyesha waandishi wa habari namna ya kupima udongo ukiwa maabara
Mkurugenzi wa kampuni inayojishughulisha na upimaji wa afya ya udongo (LSSL) Dkt Edmond Matafu akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu upimaji wa udongo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...