Na Muhidin Amri,Tunduru
MFUKO wa maendeleo ya Jamii TASAF katika wilaya ya Tunduru mkoani 
Ruvuma,umetumia jumla ya shilingi  664,288,000.00 kama malipo ya 
walengwa 12,785 kutoka vijiji 88 waliopo kwenye mpango wa kunusuru kaya 
maskini wilayani humo.
Hayo yamesemwa jana na Mratibu wa Tasaf wilayani Tunduru Muhidin Shaibu 
wakati wa zoezi la malipo ya  walengwa waliopo kwenye mpango huo katika 
vijiji vya Lipepo na Nalasi ikiwa ni malipo ya mwezi Novemba na Desemba 
2020.
Aidha, amewataka wanufaika  hao kutumia vizuri fedha za ruzuku 
wanazopata kwa kuanzisha na kuendeleza miradi badala ya kutumia  katika 
anasa ili kuepuka kuendelea kutegemea ruzuku ya Serikali ambayo 
inatolewa kila baada ya miezi 2.
Shaibu amewakumbusha walengwa na wanufaika wa mpango huo  kutumia ruzuku
 wanazopata kwa usahihi,kuendelea kuhamasishana kujiunga na mfuko wa 
Bima ya Afya iliyoboreshwa ambapo hadi sasa jumla ya kaya 2620 
zimeshajiunga na mfuko huo.
Kwa mujibu wake, mbali na zoezi la malipo ya fedha hizo TASAF imeendelea
 kuhakiki  mashuleni uwepo wa watoto wanaotoka katika kaya maskini 
wakiwa na vifaa vya shule kama sale na madaftari lengo ni kujiridhisha 
kama mzazi au mlezi anatimiza wajibu wake kutokana na ruzuku 
wanazopokea.
Alisema,hatua hiyo itasaidia sana kuepuka adhan a migogoro ya kisheria 
inayoweza kuwakumba watoto na wazazi wao wakati wa ukaguzi wa maendeleo 
yao shuleni pamoja na wale wanaotakiwa kuhudhuria kliniki.
Kwa upande wake mwezeshaji wa Tasaf katika kijiji cha Nalas Aziz Tausi  
alisema katika kijiji hicho zaidi  ya shilingi milioni 4.836 zimelipwa 
kwa walengwa kama ruzuku ya mwezi Novemba na Desemba.
Alisema, malipo hayo yamekwenda sambamba na uhakiki wa taarifa za 
wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi mwaka 2020 na kujiunga na  kidato 
cha kwanza katika mwaka wa masomo 2021  wanaotoka kaya maskini.
Amewakumbusha walengwa kuzingatia kanuni na taratibu za Tasaf kwa 
kipindi chote cha mradi  kwa kuwa kuna fursa nyingi ambazo Serikali 
inaendelea kuzitoa kwa kaya hizo.
Alisema, dhamira kubwa ya Serikali ni kuona kaya za walengwa 
zinaondokana na umaskini uliokithiri na kuwa kaya zenye uwezo wa 
kujitegemea kwa mahitaji yote muhimu badala ya kuendelea kusubiri na 
kupokea ruzuku ya Serikali inayotolewa na Tasaf.
Mwezeshaji wa Tasaf kijiji cha Lipepo Elienea Mndeme alisema, katika 
kijiji hicho  zaidi ya shilingi milioni  2.912 zimetolewa kama ruzuku 
kwa walengwa wa mpango huo.
Baadhi ya wanufaika wa mpango huo Rajabu Mussa na Abdala Said  
wameishukuru Serikali kuendelea kutoa ruzuku kwao kwani itawasaidia sana
 kuboresha hali za maisha na kuhaidi kutumia vizuri fedha hizo 
kujiimarisha kimaisha na kujiunga na Bima ya Afya kama Serikali 
inavyowataka.
Mwezeshaji wa Tasaf kijiji cha Nalasi Aziz Taus akizungumza na walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini katika kijiji hicho ambapo aliwataka kutumia kiasi cha fedha wanazopata kujiunga na Bima ya Afya.
Picha na Muhidin Amri,Mratibu wa mfuo wa maendeleo ya jamii Tasaf wilaya ya Tunduru Muhidin Shaibu akiongea jana na wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini wa kijiji cha Nalas kata ya Nalasi kabla ya kuanza kwa zoezi la malipo ya ruzuku ya mwezi Novemba na Desemba 2020 ambapo zaidi ya shilingi milioni 664 zimelipwa kwa wanufaika wa mpango huo wilayani Tunduru.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...