Na Grace Gurisha
yatangaza utabiri wa hali ya hewa,
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetangaza utabiri wa hali ya hewa kwa msimu wa mvua za masika kuwa mvua za wastani zinatarajiwa kunyesha katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
Aidha, imesema katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, upungufu wa unyevunyevu kwenye udongo unaweza kujitokeza.
Taarifa hiyo ya hali ya hewa, imetolewa Leo Februari 18,2021 na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa mamlaka hiyo ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA,
,Dkt. Hamza Kabelwa kutoka na utabiri uliyofanywa na joto la wataalamu kuelekea mvua za masika ambazo zitanyesha za wastani na chini ya wastani.
Amesema msimu mvua za masika ambao ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki kwa mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), Pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani ikijumuisha visiwa vya mafia, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Mkurugenzi huyo, anataja maeneo mengine kuwa ni ukanda wa Ziwa Victoria kwa mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
"Kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na inavyotarajiwa katika kipindi chote cha msimu, kwa ujumla mvua za wastani zinatarajiwa kunyesha katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka," amesema Dkt.Kabelwa
Pia, amesema katika taarifa yake, kuwa maeneo mengi ya nyanda za juu kaskazini mashariki na ukanda wa Ziwa Viktoria yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, aidha, maeneo ya Pwani ya kaskazini yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
"Msimu wa mvua za masika unatarajiwa kuambatana na vipindi vya mvua kubwa hususani katika kipindi cha mwezi Machi”, amesema Dkt. Kabelwa
Dkt. Kabelwa amesema katika ukanda wa Ziwa Viktoria, mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, wilaya za Kakonko na Kibondo, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya ukanda wa huo, pamoja na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.
"Mvua hizi zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2021 na kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Mei, 2021," amesema Dkt. Kabelwa wakati anatoa taarifa ya utabiri wa hali ya hewa.
Amesema kuwa ukanda wa Pwani ya Kaskazini, (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani, ikijumuisha visiwa vya Mafia, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, ambapo mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani ya kaskazini.
"Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza mapema katika wiki ya nne ya Februari, 2021 na zinatarajiwa kuisha katika wiki ya tatu ya mwezi Mei, 2021," amesema Dkt.Kabelwa
Akizungumzia kuhusu upande wa Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), Dkt. Kabelwa amesema mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi na zinatarajiwa kuanza mapema katika wiki ya nne ya Februari, 2021 na kuisha katika wiki ya tatu ya Mei, 2021.
Amesema katika kipindi cha masika Machi hadi Mei, 2021, hali ya unyevunyevu wa udongo na maji ya kutosha kwa ajili ya umwagiliaji inatarajiwa kuwepo katika baadhi ya maeneo.
Hata hivyo, hali hiyo ya unyevunyevu hususan katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria na Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, inaweza kuathiri ukuaji wa baadhi ya mazao yasiyohitaji maji mengi, kama vile mahindi, maharagwe na mazao ya mizizi.
Pia, Mkurugenzi huyo ametoa ushauri wa kumarisha miundombinu ya kilimo ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na vipindi vifupi vya mvua kubwa.
"Teknolojia ya uvunaji maji ya mvua izingatiwe ili kuhifadhi maji kwa matumizi ya baadae. Wakulima tunawahimiza kutafuta na kutumia ushauri wa wataalam wa kilimo ikiwa ni pamoja na maafisa ugani katika maeneo yao," amesema Dkt. Kabelwa .
Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Hamza Kabelwa katikati akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani wakati anatoa utabiri wa hali ya hewa kwa kipindi cha masika, kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Uchambuzi wa Utabiri, Dkt.Kantamla Mafuru, kulia ni Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri, Samwel Mbuya.
Mchambuzi wa Hali ya Hewa, Joyce Makwata akiwafafanulia waandishi wa habari jinsi utabiri utakavyokuwa, baada ya Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri TMA, Dkt. Hamza Kabelwa kutoa utabiri wa hali ya hewa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...