Mgeni rasmi ya hafla ya kwanza ya wauguzi na Wakunga
waliofaulu mitihani ya usajili na leseni Bi.Ziada Sellah Mkurugenzi wa
Idara ya wauguzi na Ukunga wizara ya afya akiongea na wahitimu hao mjini
Kibaha

Mmoja wa mhitimu akiwasha mshumaa kabla ya Kula kiapo Cha taaluma ya Uuguzi na Ukunga


Afisa kutoka Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TNMC) Bi.Jane Mazigo alitia mada kwa wahitimu

Mmoja wa wahitimu hao akipokea Cheri na leseni kutoka kwa mgeni rasmi

Picha ya pamoja ya mgeni rasmi
na wahitimu hao nje ya ukumbi wa kituo Cha Maendeleo Cha wauguzi na
Wakunga kilichopo mjini Kibaha

Bw.Gustav Moyo akiwasilisha mada ya kuwakumbusha wauguzi na Wakunga majukumu yao kabla ya hafla hiyo

Mgeni rasmi bi. Ziada Sellah akimkabidhi cheti muhitimu wakati wa hafla hiyo leo(Picha zote na Emmanuel Malegi-WAMJW)
*****************************************
Na. Catherine Sungura,WAMJW-Kibaha
“Huduma
za Uuguzi na Ukunga zinapimwa zaidi na uadilifu wa watoa huduma,
uadilifu unasaidia kuzingatia matumizi sahihi ya elimu aliyonayo
mtaaluma kwani elimu bila maadili ni Bure”.
Hayo
yamebainishwa leo Kwenye hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima iliyosomwa kwa niaba yake
na Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi na Ukunga Bi. Ziada Sellah wakati wa
hafla ya kwanza ya kuwasajili Wauguzi na Wakunga wapya iliyofanyika
Kwenye ukumbi wa kituo Cha Maendeleo ya Uuguzi na Ukunga mjini Kibaha.
Bi.Sellah
amesema kuwa wanataaluma hao wanapaswa kuzingatia viapo vyao vya
taaluma na kutoa huduma kwa kujali utu, heshima na upendo kwa wagonjwa
ambao wanawahudumia katika vituo vyao vya kazi.
“Tukio
hili la Leo litasaidia kutoa msisitizo kwa wanataaluma kutambua wajibu
wao katika utoaji wa huduma huku wakizingatia maadili ya taaluma zao,
kitendo hiki kilitakiwa kutekeleza kipindi kirefu kilichopita na ni
vyema kikatekelezwa na taaluma zote za sekta ya afya nchini ili
kuwafanya wahitimu kuheshimu taaluma zao”. Amesisitiza Mkurugenzi
Sellah.
Kwa
upande wa kuboresha uwezo wa kutekeleza majukumu ya Baraza la wauguzi
na Wakunga nchini, Bi.Sellah amelitaka Baraza hilo kuzingatia ubora wa
stadi na maadili ya taaluma ili kushuhudia mabadiliko makubwa ya ubora
wa huduma za afya nchini.
“Tumeendelea
kushuhudia changamoto nyingi za huduma zinazotolewa bila kuzingatia
maadili ikiwa ni pamoja na kunyanyaswa wateja, natoa msisitizo tena kwa
wanataaluma wote wa sekta ya afya zingatieni viapo vyenu”. Ameongeza Bi.
Sellah.
Vilevile
Bi. Sellah amewahimiza viongozi katika ngazi za mikoa na hospitali za
Rufaa ambao wamepewa mamlaka na Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya mwaka 2010
kuchukua hatua za mapema pale panapobainika Kuna upungufu katika utoaji
wa huduma.
“Tekelezeni
majukumu yenu kwa haraka iwezekanavyo na kisha mtoe taarifa kwa Baraza
la Uuguzi na Ukunga makao makuu kwa hatua zaidi, wateja wanapenda
kushuhudia haki inapatikana mapema, kuchelewa kuchukua hatua panapotokea
upungufu kunaleta picha mbaya kwa wateja na kuleta taswira kuwa Kuna
kulindana au udhaifu katika usimamizi wa maamuzi”.
Bi.
Sellah amelipongeza Baraza hilo kwa kuandaa tukio hilo na kuwahimiza
liwe endelevu kwa vile linatoa wasaa kwa wanataaluma kuelewa maana ya
Baraza na majukumu yake pia amewasisitiza kuhusu maadili ya taaluma yao.
Naye
Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Bw. Abner Mathube amesema
Sheria iliyounda Baraza hilo ilitungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa lengo la kuhakikisha watanzania wanapata huduma za
Uuguzi na Ukunga zilizo salama hivyo Baraza hilo limehakikisha
linawasajili wataalamu wenye sifa za kitaaluma na kuwachukulia hatua kwa
mujibu wa Sheria wale ambao wanatoa huduma chini ya viwango
vinavyotegemewa.
Wakati
huo huo Kaimu Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Bi. Happy Masenga
amesema Baraza linahakikisha leseni ya kutoa huduma za kitaaluma za
Uuguzi inatolewa kwa waombaji waliopitia mafunzo yaliyokubalika kutoka
vyuo vinavyotambulika na kufaulu mitihani ya usajili inayoendeshwa na
Baraza.
Bi.
Masenga amesema toka mwaka 2014 Baraza limekuwa likiendesha mitihani ya
usajili na leseni ili kupima umahiri wa wahitimu kwa lengo la
kujiridhisha kama wanao uwezo wa kutoa huduma salama kwa wateja na hadi
sasa wahitimu 30,715 wamekwishafanya mitihani hiyo.
Katika
hafla hiyo jumla ya wauguzi na Wakunga 839 waliohitimu masomo ya Uuguzi
na ukunga katika ngazi mbalimbali na kufaulu mitihani ya usajili na
leseni iliyofanyika Novemba, 2020 na mahafali hayo yaliyoandaliwa na
Baraza yamefanyika kwa Mara ya kwanza tangu Baraza hilo kuanzishwa mwaka
1953.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...