Wanawake wajasiliamali na wafanyabiashara nchini wameshauriwa kuongeza jitiahada zao zaidi katika kuboresha zaidi mawazo ya biashara sambamba na kuongeza ubora za wa bidhaa zao ili kuongeza ushawishi kwa taasisi za kifedha nchini ziweze kuwakopesha kwa urahisi.

Akizungumza wakati wa kufunga Maonesho ya Wafanyabiashara wanawake Tanzania yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku nne, Meneja Mahusiano wa Benki ya NBC, Bi Consolatha Shayo alisema taasisi za kifedha zinashawishika zaidi kutoa mikopo kwa kuzingatia ubora wa wazo la biashara na sio jina au jinsia ya mkopaji.

Alisema hiyo ndio sababu benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inaendelea kuwaongezea ujuzi wajasiliamali hao ili kuboresha mawazo na bidhaa zao ili kuwajengea uwezo utakaowezesha kufanya biashara zao kwa weledi na kutengeneza faida itayowawezesha kurejesha mikopo yao.

“Ndio maana kupitia wataalamu ambao tunawatumia kutoa elimu kwa wajasiliamali kupitia maonesho kama haya, tumekuwa tukifundisha na kusisitiza sana juu ya umuhimu wa kujenga zaidi majina ya bidhaa zao kuliko majina yao binafsi kwa kuwa taasisi za kifedha zinatazama zaidi biashara zao na sio jinsia wala majina yao binafsi,’’ alisema  Consolatha.

Pamoja na kudhamini maonesho hayo, benki hiyo pia iliandaa programu kadhaa za mafunzo kwa wajasiliamali ikiwemo kliniki ya biashara kwa kushirikisha taasisi na mamlaka mbalimbali ikiwemo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Zaidi benki hiyo ilitumia fursa hiyo kutangaza huduma zake mahususi kwa ajili ya wanawake na wajasiliamali zikiwemo akaunti za NBC Kua Nasi na akaunti mpya ya Johari.

“NBC Kua Nasi ni akaunti maalum kabisa kwa wote wanaojihusisha na biashara ndogo ndogo kama vile mama na baba lishe, wenye maduka ya reja reja, wasindikaji wa vyakula na mazao, bodaboda, wazabuni wa taasisi mbalimbali wakati akaunti ya Johari ni mahususi kwa ajili ya wanawake na inawezesha kuweka akiba kidogo kidogo kwa kianzio cha shilingi 10,000 tu. Akaunti zote hizi hazina makato ya mwezi,’’ alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Wafanyabiashara wanawake Tanzania (TABWA) Bi Noreen Mawala ambae taasisi yake ndio iliratibu maonesho hayo pamoja na kuipongeza benki ya NBC pamoja na wadau wengine kwa kufanikisha maonesho hayo, alisema taasisi hiyo kwasasa inaandaa safari ya mafunzo na maonesho ya biashara katika nchi za Oman na Comoro ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara hao kutangaza biashara zao katika mataifa hayo.

“Baada ya mafanikio kupitia maonesho haya yaliyokwenda sambamba na maadhimisho ya siku ya mwanamke Duniani  tunatarajia kuwa na safari za maonesho ya biashara zetu katika nchi za Oman na Comoro ili kufungua milango zaidi ya kutangaza biashara zetu nje nchi,’’ alisema.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Wafanyabiashara wanawake Tanzania (TABWA) Bi Noreen Mawala (kushoto) akikabidhi zawadi kwa niaba ya wanawake wajasiliamali nchini kwenda kwa Meneja Mahusiano wa Benki ya NBC, Bi Consolatha Shayo (Kulia) na Meneja Bidhaa na Huduma za Kibenki kutoka Benki ya NBC Bw Jonathan Bitababaje (katikati) ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa benki hiyo katika kuwasaidia na kuwawezesha wanawake wajasiliamali nchini. Makabidhiano hayo yalifanyika jana wakati wa kufunga Maonesho ya Wafanyabiashara wanawake Tanzania yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku nne kwa udahamini wa benki hiyo.

Meneja Mahusiano wa Benki ya NBC, Bi Consolatha Shayo akizungumza na washiriki wa maonesho hayo waliohudhulia mafunzo ya ujasiliamali yaliyodhaminiwa na benki ya NBC kwa kushirikiana na TABWA pamoja na wadau wengine.


Wajasiliamali wakifuatilia mafunzo hayo.


Baadhi ya wajasiliamali wakipokea vyeti vya ushiriki wa mafunzo hayo.       







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...