Na John Nditi, Morogoro 
MKUU wa Wilaya ya Morogoro ,Bakari Msulwa amewataka wananchi waliovamia  na kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji  kwenye  Kitalu cha uwindaji cha Gonabis kilichopo hifadhi ya jamii ya wanyamapori katika eneo la Duthumi kuondoka mara moja kwa vile uwepo wao ni  kinyume cha  sheria na  wanachangia kuharibu  uoto wa asili. 
Msulwa ,alitoa agizo hilo kwa wananchi  wa vijiji 11 vinavyopakana na eneo  la Hifadhi ya jamii ya wanyamapori   akiwa  ameambatana na wajumbe wa  kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo pamoja na viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya  Morogoro. 
Alisema eneo hilo ambalo nimevamiwa limetengwa mahususi kwa ajili ya kuhifadhi na kutunza uoto wa asili ambapo ndani yake kuna vyanzo vya maji, mazalia ya wanyama wanaoingiliana na Hifadhi ya Mwalimu Nyerere. 
" Eneo hilo ambalo limetengwa kwa hifadhi  lakini kuna uvamizi mkubwa umekuwepo hapo kwa shughuli za kibinadamu  na tunakata tuwapelekee ujumbe wananchi wa hapo ya kwamba wakati umefika wa kuondoka  na jambo hili limekuwa muda mrefu takribani miaka saba “ alisema Mkuu wa wilaya . 
Mkuu wa wilaya huyo , alisema : Lakini sasa imefikia mahali tumejipanga waachie uoto wa asili uendelee  , sasa waondoke maeneo hayo , ni ujumbe ambao tunataka kuusimamia kwa sababu  si ujumbe mpya  na sasa tunataka tuusimamie tunataka wananchi katika maeneo hayo waanza kujidnaa kisakilojia ya kuondoka eneo hilo” alisisitiza  Msulwa. 
Hata hivyo ,Mkuu wa wilaya  na ujumbe wake  walishindwa kufika  eneo la hifadhi  hiyo  kujionea uharibifu unaofanyika kutokana na shughuli za kibinadamu baada ya magari ya msafara wake kukwama  kwenye njia ya kuelekea ndani ya hifadhi hiyo na kutotimiza lengo la  ziara hiyo. 
Mkuu wa Wilaya aliamua kukutana na uongozi wa Jumuiya ya Kuhifadhi Matumizi Bora ya Maliasili (JUKUMU) katika kijiji cha Duthumi ambao aliwapa  majukumu ya  kusimamia na kuhifadhi  eneo hilo. 
Pamoja na jukumu hilo pia aliitaka  jumuiya hiyo kuhakikisha inatekeleza majukumu yake ipasavyo yakiwemo ya  kusimamishwa  wananchi kuendelea na shughuli za binadamu  katika hifadhi hiyo. 
  Mkuu wa wilaya hiyo  aliitaka pia kuhakikisha kusimamia  maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya vitalu yabaki bila kuingiliwa na shughuli nyingine za kilimo na ufugaji na kuangaliwa upya kwa mikataba ya kampuni zilizowekeza kwa shughuli za uwindaji. 
Naye Mkurugenzi  Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Morogoro, Rehema Bwasi, alisema  kuwa kuna kila sababu ya kuhakikiwa upya mipaka ya eneo hilo na kuweka bikoni . 
Bwasi pia alisema ya kwamba, halmashauri hiyo itahakikisha kuwa  hifadhi hiyo inalindwa na sio kubadili matumizi kwani ina manufaa makubwa kuanzia  ngazi ya vijiji, Halmashauri na Taifa. 
Naye Mwenyekiti JUKUMU , Galeko Magawa alisema kuwa  eneo hilo limevamiwa  na wafugaji pamoja na wakulima  na chanzo kinaweza kuwa ni  Kampuni ya Morogoro Hunting Safari kushindwa kwalipa malipo yao ya ulinzi na usimamizi wa eneo hilo tangu mwaka 2018 walipofunga mkataba baina yao. 
Magawa ,alisema  kutokana na jambo hilo  kampuni hiyo imeshindwa kuendesha shughuli zake ipasavyo kutokana na uvamizi ndani ya hifadhi hiyo. 
Msemaji wa Kampuni hiyo yenye kitalu cha uwindaji cha Gonabis , Ally Kingalu , licha ya kupongeza uamuzi huo wa Mkuu wa Wilaya, alisema  zoezi aliloanzisha si jepesi kiutendaji kwani wafugaji waishio eneo hilo hutumia mishale kujihami. 
Hata hivyo , alisema ya  kwamba viongozi waliopita hawakutambua majukumu yao wakidhani kuwa eneo hilo ni mali ya kampuni si ya kwao. 
Eneo hilo la Hifadhi ya jamii ya wanyamapori limezungukwa na vijiji  11 ambavyo vimepewa  mamlaka ya kusimamia hifadhi hiyo yenye kitalu cha Gonabis chenye wanyama aina ya tembo,  Chui, Kongoni, Nyumbu na Swala wanaotajwa kutoweka kwa kasi kutokana na shughuli za binadamu . Hata hivyo , Kampuni ya Morogoro Hunting Safari inayomiliki kitalu hicho inashindwa  kushindwa kuendesha shughuli zake kutokana na mahema yao kuchomwa moto na wananchi.
Baadhi ya askari na viongozi wengine wakilinasua gari lililokwama kwenye barabara kuelekea katika hifadhi ya jamii ya wanyamapori ambapo mkuu wa wilaya hiyo, Bakari Msulwa ( hayupo pichani ) na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na kushindwa kufika eneo husika kwa ajili ya kujionea uharibifu unaofanyika kutokana na shughuli za kibinadamu za kilimo na ufugaji ndani ya hifadhi hiyo.( Picha na John Nditi).

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro ,Bakari Msulwa ( waili kutoka kulia) akisisitiza jambo kwa viongozi wa JUKUMU , Kampuni ya Morogoro Hunting Safari pamoja na wa Halmashauri ya wilaya ya Morogoro kuhusu usimamizi wa hifadhi .


 


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...