Na Ripota Wetu, Michuzi TV-Dodoma.


SPIKA wa Bunge  Job Ndugai amesema leo ni siku ya huzuni na majonzi makubwa kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwasababu ni kweli kabisa wamefiwa na mwenzao, wamehemewa, wamechanganyikiwa.

Amesema hayo leo wakati wa kuaga mwili wa mpendwa wetu Hayati Dk.John Magufuli aliyekuwa Rais wa Tanzania ambaye amefariki dunia Machi 17,2021 na leo anaagwa jijini Dodoma ambapo wabunge wamepata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho katika viwanja vya Bunge.

Spika Ndugai amesema "Ni kweli kabisa tumefiwa na mwenzetu, tumehemewa, tumechanganyikiwa, Watanzania wanalia wamekata tamaa lakini sisi Wabunge tunasema ahsante Mungu kwa maisha ya John Pombe Magufuli ambaye aliishi siku zote kwa kumtanguliza Mungu mbele,ahasante Mungu  kwa kunipa fursa ya kufanya kazi na Magufuli.

"Kwa miaka20 ambayo nimekuwa hapa Bungeni nimefanya naye kazi kwa karibu, kama rafiki yangu, kama ndugu yangu, nilimfahamu vizuri kama kiongozi wangu, lakini safari leo imetimia na mwendo ameumaliza, rafiki yangu John leo umelala hapa mbele yetu, ulikuwa ukinieleza kuhusu Tanzania unayoitaka.

"Na mimi na wabunge wenzangu ni wajibu wetu ni kukuunga mkono kwa kutunga sheria, kwa kupitisha bajeti ambazo zilifanikisha ndoto hizo kutimia,kwa kuhakikisha tunao ushauri kwa Serikali kwa kila nyanja ni wa kuwezesha na kufanikisha, hatutafanya kazi ya kupinga ili yasifanikiwe hapana,tulikuunga mkono mwanzo mwisho,"amesema Spika Ndugai.

Aidha amesema anakumbuka mapema mwaka jana 2020, alikuwa mtani wake wakawa wanazungumza kwa simu."Sikumbuki yalikuwa mazunguzo gani , uliishi kuniuliza, hivi Job ukifa utazikwa wapi, nikamwambia nikifa nitazikwa Kongwa, akauniuliza na mimi nikifa? nikamwambia tutakuzika ugogoni kwasababu umetupa heshima kufanya makao makuu kuwa Dodoma.

"Kwa hiyo tutakuzika Dodoma, pili nina sheria ya mazishi ya viongozi , kwa hiyo wewe Dodoma hutoki na mimi na Bunge tutahakikisha tunakuzika Dodoma.Akasema koma kabisa ishia hapo hapo , mimi nitazikwa Dodoma na safari moha alikuja hapa na Mheshimiwa Lukuvi kuzindua nyumba za NHC na pale chini kulikuwa na eneo la kuzika viongozi , akawarudishia Wagogo ardhi yao, yaani safari yake ni kueleka Dodoma, naishukuru Serikali kwa kutimiliza jambo lake mwenyewe,"amesema Spika Ndugai.

Akiendelea kumuelezea Dk.Magufuli, Spika Ndugai ameema hivi "John ulikuwa mtu ambaye umepanda mbegu, ulikuwa mpanda kama yule mpanda wa kwenye Biblia , naamini mbegu uliyopanda imeanguka kwenye udongo mzuri, umepanda mabarabara ya lami kila kona ya nchi yetu, umepanda mbegu ya madaraja ambayo hatukuamini kama tunayaweza, umejenga masoko na hapa Dodoma kuna soko umelipa jina la mimi ndugu yako, soko la Ndugai.

"Umefanya mengi, umejenga meli, umejanga viwanja vya ndege, umenunua ndege, umefanya mengi, umejenga reli ya treni ya kisasa ya SGR, ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere uaoendelea, umeenga viwanda, umejenga vituo vya afya umejenga hospitali, umejenga , umejenge, umejenga, umejenga hospitali za Rufaa, umejenga Magufuli , hii ni mbegu uliyokuwa umeipada na tunaamini itamea kwenye udongo mzuri."

Amefafanua yapo mengi ambayo Dk.Magufuli amepanda ambayo hayaonekani kwa macho, amepanda uwajibikaji kwenye utumishi wa umma, amepanda uchapakazi, amepanda uzalendo kwa nchi yetu, amepanda uadilifu, amepanda matumizi mazuri ya fedha za Serikali na wale ambao hawakufanya vizuri aliwatumbua hadharani.

"Sasa iko hadithi ya wale Nyani ambao walikuwa wanashambulia shamba la mkulima wa mahindi, mahindi yanapoiva basi wanashambulia, wanavuna  wanakula, basi waliposikia mwenye shamba amefariki wale Nyani walifurahi sana na katika nchi yetu Nyani wa namna hiyo hawakosekani.

"Lakini mwaka uliofuata Nyani wale wakarudi shambani wakale Mahindi, wakasahau kama mwenye shamba alifariki , kwa hiyo hapakuwa na mahindi ya kula,kwa hiyo wakakaa na kuanza kusikitika.Ni kweli mwenye shamba amefariki, lakini sisi hatutakuwa ngedere wa kudhani sasa tufanya mambo tunavyotaka.

"Wabunge wenzangu tumeondokewa na kiongozi , tazama Watanzania wanavyolia kila mahali , na tukumbuke alivyokuja mara mwisho hapa Bungeni alitoa hotuba yake kwa miaka mitano inayokuja , hotuba ile ni vema sisi Bunge tukaitumia sisi wabunge.

"Rafiki yetu JPM umeweza kuhamisha Serikali kuja Dodoma , naamini hili litaendelezwa na Serikali inayofuata , ni jambo kubwa sana  lilishindikana wakati wote likawezekana wakati wako, tunaamini kabisa Dodoma itaendelea kuwa makao makuu ya nchi yetu.

"Nilimwambia umeamua Makao Makuu yawe Dodoma na nilimwambia wakati ule Mheshimiwa umesema lakini Mungu anaweza kukuchukua wakati wowote kwa hiyo nataka tutunge sheria, akasema sawa ,Dodoma ndio makao makuu ya nchi yetu, tulibebe Watanzania , tuhakikishe linakamilika,"amesema Spika Ndugai.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...