Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknojia Profesa Joyce Ndalichako ameitaka SUMA  JKT Kanda ya Magharibi kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa Chuo Kipya cha Ualimu Kabanga ifikapo Juni 2021.

Profesa Ndalichako ametoa agizo hilo mjini Kasulu baada ya ukaguzi kazi ya ujenzi wa chuo hicho na kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji mradi huo.

 "Ujenzi wa Chuo cha Kàbanga ulianza Machi 19, 2019 na ulipaswa kukamilika Juni 2020, pamoja na mkandarasi kuongezewa muda wa miezi nane bado kazi haijakamilika, hili halikubaliki,"alisema Waziri Ndalichako

Waziri Ndalichako amesema Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 10.6 bado unasuasua, na hata katika eneo la ujenzi hakuna wafanyakazi wala vifaa huku SUMA JKT wakiwa tayari  wameshalipwa bilioni sita.

"Nimetembelea na kukagua kila jengo hapa, majengo mengine hayana wafanyakazi na yaliyo  na wafanyakazi ni wachache na wala hakuna vifaa vya kufanyia kazi hapa. Mradi huu umekuwa ukisuasua tangu umeanza" amesema Waziri Ndalichako

Amesisitiza kukamilika kwa ujenzi huo ili kuokoa wanachuo wanaoendelea kutumia majengo ya chuo cha zamani ambayo ni hatarishi na kwamba ubovu wa majengo ya Chuo cha zamani ndio umepelekea Serikali kuja na uamuzi huo wa kujenga upya  Chuo hicho.

Naye Mkurugenzi  Msaidizi wa Elimu ya Ualimu  kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Huruma Mageni amemwambia Waziri kuwa chuo hicho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kudahili wanachuo 800 kwa mara moja  ambapo awamu ya kwanza ya ujenzi utawezesha kudahili wanachuo 400.

Mageni ametaja majengo yatakayojengwa katika awamu ya kwanza ni pamoja na maktaba, bweni moja  la wanachuo wa kike  na moja wa kiume, ukumbi wa mihadhara pamoja na mikutano, bwalo la chakula na jiko.

Majengo mengine ni jengo moja lenye madarasa  kumi, jengo la utawala, zahanati na nyumba nne za wakufunzi.

Naye msimamizi wa ujenzi kutoka SUMA JKT Luteni Kanali Onesmo Njau  amesema wanashukuru wamepata fedha nyingine kutoka Wizara ya Elimu na kuwa wanakwenda kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri na watakamilisha kazi hiyo kulingana na maelekezo.

Wakati huo huo katika kuonesha msisitizo wa uhitaji wa Chuo hicho kukamilika, Ndalichako ameambatana na wakandarasi hao kuwaonesha  hali halisi ya uchakavu ya majengo yanayotumika sasa.



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...