Na Mwandishi wetu, Kiteto
WADHAMINI
wawili waliomdhamini mshtakiwa Moita Tepeno aliyejipatia fedha kwa
kutumia jina la Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, Kanali Patrick
Songea, wamepelekwa mahabusu baada ya mshtakiwa huyo kutoroka.
Wadhamini
hao wawili Munjuri Tepeno na Leshoni Moita walimdhamini Tepeno kwenye
kesi hiyo namba 122/2020 kwa sh500,000 kila mmoja, walishindwa kulipa
fedha hizo na kupelekwa mahabusu gereza la Kiteto.
Hakimu
mkazi mfawidhi wa mahakama ya Wilaya ya Kiteto, Mossy Sasi akizungumza
jana mahakamani hapo aliamuru wadhamini hao wawili wa kesi hiyo ya jinai
waende mahabusu hadi Machi 15 mwaka huu.
Hakimu
aliwataka wadhamini hao wawili watoe fungu la dhamana ya sh500,000 kwa
kila mmoja baada ya mshtakiwa kuruka dhamana wakashindwa kulipa na
kupelekwa mahabusu.
Awali,
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani
Manyara, Holle Joseph Makungu amesema walimfikisha mahakamani hapo
Tepeno ambaye ameruka dhamana na kumfungulia shtaka la kujipatia fedha
kwa njia ya udanganyifu.
Makungu
amesema Tepeno alijipatia sh500,000 kwa njia ya udanganyifu kwa kutumia
vibaya jina la mkuu wa wilaya hiyo Keepanali Songea kinyume na kifungu
cha 302.
Amesema pia kosa
hilo lililofanywa na mshtakiwa huyo ni kinyume cha kifungu cha 301
vyote viwili vya kanuni ya adhabu ya sura ya 16.
Amesema
Tepeno alijipatia sh500,000 baada ya kumrubuni raia mwema kuwa
anampelekea Kanali Songea baada ya binti yake mwanafunzi kupata ujauzito
alipokuwa kwenye likizo ya corona mwaka jana.
"Binti
huyo alikuwa anasoma mkoani Arusha na akapata ujauzito huo wilayani
Kiteto wakati shule na vyuo vikiwa vimefungwa mwaka jana kwenye janga la
corona," amesema Makungu.
Amesema
TAKUKURU wanaendelea kumtafuta Tepeno na wanaomba wadau wa mapambano
dhidi ya rushwa popote watakapomuona wawafahamishe ili aweze kukamatwa
kwenda kupambana na kesi yake.
"Rai
yetu kwa watanzania kuacha tabia za kuwadhamini washtakiwa wasio
waaminifu kwa kuwa sheria inasema ukishindwa kutekeleza wajibu wa
kuhakikisha unamleta mahakamani mshtakiwa uliyemdhamini utalipa faini,"
amesema Makungu.
Amesema inabidi ukipe fungu la dhamana uliloahidi au uiache familia yako na kulazimika kwenda kutumikia kifungo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...