*Wasema walioteuliwa na Rais wajue wana deni kubwa
*Wasisitiza wakasimamie ukusanyaji mapato ya Serikali
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MAKAMU
wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Philip Mpango
amewaambia walioteuliwa na kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika
Serikali watambue wamepewa heshima kubwa na Rais Samia Suluhu Hassan,
hivyo hilo ni den ambalo wanatakiwa kulilipa kwa kufanya kazi kwa bidii
katika kuwatumikia Watanzania.
Akizungumza leo Aprili 6, mwaka 2021
Ikulu jijini Dar es Salaam, Dk.Mpango pamoja na mambo mengine amesema
anaungana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwapongeza wote walioteuliwa
na kula kiapo."Nataka kusisitiza kuteuliwa kwenu ni imani kubwa ambayo
mmepewa na Rais, lakini hilo ni deni kubwa kwa Rais na deni kubwa kwa
watanzania, ni deni ambalo mnatakiwa kulilipa kuanzia sasa.
"Mnatakiwa
kulipa kwa kazi nzuri ambayo imetukuka, nchi yetu bado, tumefikia
uchumi wa kati lakini tunatakiwa kuitoa nchi yetu hapa ilipo na kwenda
mbele zaidi.Naomba kusisitiza Waziri Mkuu,amewasisitiza kwenda kusimamia
ukusanyaji wa maduhuli, mimi nataka kusisitiza upande wa pili kila
mmoja weu mkasimamie matumizi adili ya rasilimali za umma mkianza na
watumishi wenyewe.
"Ninyi mnatakiwa kuwa makini katika kusimamia
rasilimali hizo, lakini pia rasimali fedha mzingatie kanuni na sheria ya
matumizi ya fedha za umma, nendeni mkasimamie mafuta ya magari,
matengenezo kwenye magari, mkasimamie miradi ya maendeleo kuna
udanganyifu mkubwa,"amesema Dk.Mpango.
Ameongeza kwa sasa bajeti ya
Serikali inaandaliwa hivyo wakaisimamie ipasavyo huku akionya tabia ya
utaratibu wa kila baada ya muda mfupi kuomba uhamisho wa fedha kwani
inaonesha bajeti haiandaliwi vizuri."Kwenye hilo Rais nitakusaidia.Pia
wanaosimamia Muungano naomba mwende mkasimamie ipasavyo kwa kushirikiana
na wenzetu wa Zanzibar, tunataka changamoto zilizopo tuzimalize kabisa,
hivyo wale wanaoshughulika na changamoto za Muungano mhakikishe
mnazimaliza kabisa".
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amewataka walioteuliwa na kula kiapo kwenda kutekeleza majukumu yao
lakini wakasome ,waelewe Wizara zao na majukumu yao ili wakawatumikie
Watanzania. "Makatibu Wakuu na Manaibu wanalo jukumu kubwa
sana,hakikisheni majukumu ya Wizara ya kila siku yanakwenda vizuri.
"Muwe
na mpango kazi ambao unakidhi mahitaji ya Rais, lakini mahitaji ya
kuwatumikia Watanzania, hakikisheni kila mwenye dhamana ambaye yuko
chini yenu utendaji wao uwe wenye nidhamu wa hali ya juu, tunataka
wananchi wasikilizwe na wahudumiwe na ofisi zetu.
"Mbali ya nidhamu
tunajukumu kila palipo na ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali yakusanywe
vizuri ili tutatekeleze miradi, tunataka kuhakikisha miradi yote iliyopo
na ile ambayo imeahidiwa lazima itekelezwe. Hivyo kila mmoja ahakikishe
miradi inakamilka kabla ya mwaka 2025,kila mtendaji akaangalie miradi
iliyopo kwenye wizara yake ili itekelezwe,"amesema Waziri Mkuu.
Aidha
amesisitiza wahakikishe uchumi wa nchi yetu uwiano sawa ." Alhamis
nitakuwa na kikao kazi na watendaji wote wa taasisi, tutapeana maelekezo
ya nini kinatakiwa kufanyika."



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...