Na Leandra Gabriel- Michuzi TV

*Clouds Media yapongezwa kwa uhamasishaji

*Taasisi za fedha zaombwa kuandaa mifumo ya ukusanyaji mikopo baada ya majanga kutokea

KATIKA Kuyafikia malengo na kujenga jamii imara zaidi wanawake wameshauriwa kuthubutu na kufanya bidii katika shughuli za maendeleo ili kujenga taifa imara na lenye nguvu.

Akizungumza kwa njia wa video katika kilele cha siku ya malkia wa Nguvu leo jijini Dar es Salaam Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson amewashauri wanawake kuthubutu na kuingia ulingoni kupambana ili kuyafikia malengo.

"Wanawake wote ni Malkia wa nguvu ila tufahamu kuwa hakuna kitu kizuri kitakachokuja ukibweteka tupambane, tusipindue meza...tupindue viti tukalie tuendeshe shughuli za maendeleo kwa ubunifu na ustadi wa juu." Amesema Dkt.Tulia.

Amesema kuwa lazima wanawake watumie fursa mbalimbali katika kuonesha uwezo mkubwa waliojaaliwa kwa kufuata nyayo za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.

"Kwa Malkia wa nguvu wanaopenda siasa karibuni mtatukuta ila kila mmoja aangalie njanja anayoweza kuifanyia kazi na kuifanyia bidii kwa kuonesha uthubutu wa hali ya juu." Amesema.

Vilevile ameipongeza Clouds Media kwa kuendeleza juhudi hizo ambazo zina mchango chanya kwa jamii ya Tanzania na kuwashauri kuendeleza mapambano hayo yanayoleta hamasa kwa wanawake wengi katika Kuyafikia malengo yao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Mhandisi. Zena Said amesema uhamasishaji unafanya na Clouds Media ni wa kuigwa kwa kuwa mapambano ni sasa na juhudi hizo zinatakiwa kuungwa mkono na wadau mbalimbali ili waweze kuwafikia wanawake wengi zaidi.

Mhandisi. Zena amewashauri wanawake kutokatishwa tamaa kwa kuwa kila aliyefanikiwa ana historia ya milima na mabonde katika safari yake ya kuyafikia maendeleo.

Awali akitoa neno kwa wanawake waliohudhuria hafla hiyo mfanyabiashara Maza Sinare maarufu kama Maznat ameziomba taasisi za kifedha zikiwemo benki kuandaa mifumo ya utoaji Bima za afya kwa wanawake wajasiriamali ili kuwaweka salama zaidi katika harakati zao za kutafuta kipato.

Pia Maznat ameziomba benki na taasisi nyingine za kifedha zinazotoa mikopo kwa wanawake kuweka mifumo ya urejeshaji wa mikopo hiyo hasa baada ya majanga kutokea.

"Tunafahamu kuwa wanawake wanauthubutu katika masuala ya uchumi, tunaomba mabenki na Taasisi za kifedha kuandaa mifumo rafiki ya urejeshaji wa mikopo ya wanawake wajasiriamali baada ya majanga kutokea kama hali ilivyo sasa baada ya kutokea kwa janga la Corona." Amesema.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...