HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imeokoa kiasi cha Tzs. 2.4 bilioni ikiwa ni fedha ambazo zingetumika nje ya nchi kuwapandikiza vifaa vya kusaidia kusikia (cochlear implant) watoto 37 kati ya 41 ambao wamepatiwa huduma hiyo baada ya kuzaliwa wakiwa na tatizo la kutokusikia.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Sufiani Baruani ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji amesema jumla ya watoto 40 na mtu mzima mmoja wamepandikizwa vifaa hivyo ambapo kati yao 37 wamelipiwa na Serikali na watoto wanne wamelipiwa na wazazi wao gharama za vifaa na upasuaji kwa asilimia 100.

Ameeleza kuwa wagonjwa hao 37, Serikali imewalipia kila mmoja Tzs. 37 milioni sawa na Tzs. 1.3 bilioni na kuongeza kuwa iwapo wangeenda nje ya nchi Serikali ingewalipia kiasi cha Tzs. 3.7 billioni sawa na Tzs. 100 milioni kwa kila mgonjwa mmoja. Hivyo Serikali imeokoa kiasi cha Tzs. 2.4 bilioni kwa kutoa huduma hii hapa nchini.

“Huduma hii kwa mgonjwa mmoja akienda nje ya nchi inagharimu kiasi cha Tzs. 100 milioni na hapa kwetu Tanzania inagharimu Tzs. 37 milioni kwa sababu kifaa chenyewe (device) kinauzwa Tzs. 31 milioni  na upandikizaji Tzs. 6 milioni”, amesema Dkt. Baruani.

Katika hatua nyingine Dkt. Baruani ameeleza kuwa huduma hii imefikisha miaka minne tangu kuanzishwa kwake  nchini mwezi Juni, 2017 ambapo wagonjwa 41 waliopandikizwa vifaa vya kusaidia kusikia ni sawa na asilimia 82 ya wagonjwa 50  ambapo Serikali iliwapeleka nje ya nchi kwa kipindi cha miaka 13 kuanzia mwaka 2003 hadi mwishoni mwa 2016.

Dkt. Baruani amesema huduma za kupandikiza vifaa vya kusaidia kusikia sasa zinatolewa MNH kupitia watalaamu wazalendo bila kutegemea wenzao kutoka nje na hii inaashiria kuwa zitakuwa endelevu.

Tanzania ni nchi ya pili kutoa huduma hii ya upandikizaji wa kifaa cha kusaidia kusikia kwa nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki baada ya Kenya na ya kwanza kutoa huduma hii kupitia hospitali za umma katika ukanda huohuo. Wenzetu wanatoa huduma hii kupitia hospitali binafsi.

Chanzo cha watoto kuzaliwa wakiwa hawasikii ni pamoja na maambukizi ya mama wakati wa ujauzito, matatizo wakati wa kujifungua ikiwemo mtoto kukosa hewa, matumizi mabaya ya dawa, magonjwa ya kurithi, homa ya manjano, homa ya uti wa mgongo, degedege n.k

Ukosefu wa usikivu ni hali ya kupoteza uwezo wa kusikia ambapo dalili za tatizo hilo kwa mtoto ni kutokushituka au kutazama anaposikia sauti za watu, milango au milio ya Radio, TV, kushindwa kuongea, kupata ugumu katika kujifunza mambo mbalimbali kama vile kusoma na kujibu tofauti wakati akiongea na mtu/watu au kushindwa kujibu.

Aidha dalili za kutokusikia kwa watu wazima ni kushindwa kuelewa maneno kwenye watu wengi, kushindwa kusikia konsonanti, kuchanganya au kukosea kutamka maneno anapoongea, mara nyingi hutaka watu wengine waongee taratibu na kwa sauti kubwa na kuongea kwa sauti ya juu hata kama anaeongea nae yupo karibu.

Jinsi ya kumkinga mtoto dhidi ya kupoteza uwezo wa kusikia au kuwa kiziwi ni kwa mama mjamzito kuhudhuria kliniki mara anapojihisi mjamzito ili kupata huduma za uchunguzi na kupata matibabu stahiki, kuhakikisha mtoto anapata na kukamilisha chanjo dhidi ya magonjwa ya surua na uti wa mgongo. Watoto wanaozaliwa na wazazi wenye historia ya kuwa na ndugu mwenye matatizo ya kusikia au kiziwi wapelekwe kwenye kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...