Na Beatrice Sanga-MAELEZO
Katika kuadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amesema Serikali itaboresha mazingira katika sekta ya habari ili Waandishi wa Habari watekeleze majukumu yao bila hofu, na kwa kujiamini.
Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo Arusha kwenye kilele cha maadhimisho hayo ambayo yalihusisha sekta mbalimbali.
"Serikali itaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya habari ili muweze kutekeleza majukumu yenu bila hofu, na kwa kujiamini huku mkizingatia sheria, kanuni, maadili na weledi ili wananchi waweze kupata habari sahihi kwa ajili ya manufaa na maendeleo yao,"amesema.
Waziri Bashungwa amesema ili kuendana na lengo namba 16 la Maendeleo Endelevu (SDG16), Tanzania itahitaji kuwa na ukusanyaji wa fedha wenye tija na wa kudumu, takwimu zenye ubora zinazozalishwa na kushirikishwa kwa umma, ambapo matokeo yake yanaweza kufanyiwa majaribio na kupimwa maendeleo yake.
"Ni muhimu kuwa na mpango wa maendeleo ili kuviwezeshe vyombo vya habari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi. Waandishi wa Habari wanashindwa kutekeleza majukumu yao kwa sababu mbalimbali zikiwemo za matunzo, na mishahara midogo kwa wafanyakazi, mapato yasiyotosheleza, na kukosa kinga bima ya afya kwa waandishi pamoja na wasaidizi wao. Mambo haya yamekuwa ni tatizo na kuleta wasiwasi kwa wanahabari," amesema.
Amesema Serikali inahimiza wadau wote wa habari, kuhakikisha wanaweka utaratibu unaowawezesha kufanya ufuatiliaji, na uwajibikaji katika kutekeleza sera na sheria za nchi, pamoja na miongozo kwa umma na jamii kwa ujumla. Miongozo hiyo itazingatia kuwepo kwa mazingira na hali bora ya kazi, ulinzi na usalama wa waandishi, kujua kufanya kazi za kiuandishi, ikiwa ni pamoja na uelewa wa matumizi ya kijiditali.
"Serikali ya awamu ya sita inathamini na kutambua uhuru wa vyombo vya habari na katika muktadha huo hivi karibuni Serikali ilivifungulia vyombo vya habari vya kielektroniki vya online TV vilivyokuwa vimefungiwa kwa makosa mbalimbali ili kuhakikisha kuwa vinafanya kazi kwa uhuru na kukuza ajira za vijana nchini,"amesema.
Amesema Tanzania ni miongozi mwa nchi chache zenye vyombo vingi vya habari Barani Afrika ambapo mpaka sasa kuna jumla ya Magazeti 246, Televisheni 53, Redio 194, Redio za Mtandaoni (Online Radio) 23, Blogs 120 na Televishenio Mtandao (Online TV) 440. Hii ni ishara kuwa nchi yetu inathamini na kuenzi vyombo na taaluma ya habari, hivyo basi katika kusisitiza umuhimu wa habari ndani ya ikolojia ya habari, majadiliano ya leo yataangazia hatua za kuhakikisha vyombo vya habari vina hali nzuri kiuchumi, kunakuwa na njia za kuhakikisha na kunakuwepo na uwazi katika upatikanaji wa habari kwa Watoa Huduma ya Mitandao, na kuvisaidia vyombo vya habari vichanga kwa kuviongezea uwezo wa kiutendaji, kama sehemu muhimu ya habari kwa manufaa ya umma.
“Ni vyema mkatambua kuwa jukumu lenu kubwa kama washiriki katika mjadala huu ni kuhakikisha kuwa mapendekezo mtakayotoa yataleta mafanikio. Mafanikio hayo yatapatikana iwapo wadau wote tutashirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa mapendekezo na maazimio. Kwa upande wa Serikali ya Awamu ya Sita (06) inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, tunawahakikishia ushirikiano mkubwa.”
Aidha, nitoe wito kwa Viongozi wenzangu ndani ya Serikali kuhakikisha tunaondoa vikwazo na kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari pale wanapohitaji taarifa muhimu kwa Manufaa ya Umma na maslahi ya Taifa letu kwa ujumla.
Kuhusu changamoto amesema "Kuna changamoto nyingi mnazokumbana nazo wakati wa kutekeleza majukumu yenu, zikiwemo kunyimwa taarifa bila sababu ya msingi hata kama una kitambulisho kinachotolewa na Serikali kukutambulisha kama ni mwandishi wa habari.
Hivyo nipende kutumia fursa hii adhimu kuwahakikishia tena ndugu zangu wanahabari kwamba Serikali yenu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ipo pamoja nanyi na itaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya habari ili muweze kutekeleza majukumu yenu bila hofu, na kwa kujiamini huku mkizingatia sheria, kanuni, maadili na weledi ili wananchi waweze kupata habari sahihi kwa ajili ya manufaa na maendeleo yao,"amesema Bashungwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...