Kamishna Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa  Rukwa Ralph Meela akichangia kikao kati ya Wadau wa vyombo vya Utoaji Haki Mkoani Rukwa  na Makatibu Wakuu  wa Katiba na Sheria, Utumishi na Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto katika mchango wake, Mkuu huyo wa upelelezi aliomba wadau kama wapelelezi kushirikishwa katika vikao vya uchambuzi wawafungwa wanaostahili kupata msamaha. Kikao hicho kilifanyika siku ya Alhamisi katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Makatibu Wakuu, Profesa Sifuni Mchome, Laurian Ndumbalo na  John Jingu wakibadilishana  mawazo na  kupeana mrejesho mara tu baada ya kumalizika kwa kikao chao na Wadau wa Vyombo vya Utoaji haki Mkoani  Rukwa siku ya Alhamisi



WADAU wa  vyombo vya utoaji haki Mkoani Rukwa, wameomba  kushirikishwa katika  vikao  vya uchambuzi wa wafungwa wanaostahili kupata msamaha wa Rais.

Wamesema  kushiriki kwako   katika vikao hivyo  kutasaidia sana  katika kuhakikisha kwamba, wale wanaopata msamaha  huo hawatojihusisha tena na vitendo vya uhalifu warudipo  uraiani.

Ombi  hilo limetolewa na  Mkuu  wa Upelelezi Mkoa wa Rukwa  Kamishna Msaidizi wa Polisi Ralph Meela, wakati  alipopewa fursa ya kutoa tathimini yake  kuhusu  hali ya utoaji hakijinai katika mkoa wa Rukwa, mafanikio na changamoto wanazokabiliana  nazo.

Ilikuwa katika kikao cha pamoja kati ya  Makatibu Wakuu  watatu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na  Wadau wa vyombo  vya utoaji haki, kikao kilichofanyika leo ( Alhamisi) katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

“ Tunashukuru sana kwa ujio wenu katika Mkoa wa Rukwa,    hali ya utoaji Hakijinai kwa mkoa wetu kwa kweli ni nzuri. Ila ningependa nigusie katika kipengele cha  msamaha wa wafungwa. Tungeomba na sisi wadau wa upelelezi katika Jeshi la Polisi na wadau wengine tushirikishwe katika vikao vya uchambuzi” akaomba Mkuu wa Upelelezi  Mkoa wa Rukwa.

Amebanisha kwamba,  kwa kushiriki vikao vya  uchambuzi kunaweza kusaidia katika kutoa mchango wa mawazo na maoni yao yatakayosaidia kubainisha ni mfungwa gani kweli anastahili kupata msamaha na hata akirudi uraiani hata leta matatizo

“Katika mkoa wetu wafungwa 58 walipasa msamaha wa Rais, lakini wiki moja baadaye wawili kati yao walikamatwa kwa makoa ya  kuiba mbuzi na mwingine kuvunja duka.  Kama wapelelezi wangeshirikishwa katika vikao  uchambuzi pengine hawa wawili wasingestahili kupata msahama  kwa sababu tunafahamu mienendo ya wafungwa wengi”akasisitiza

Akichangia  kipengele hicho cha msamaha wa wafungwa, Mrakibu wa Magereza Mkoa wa Rukwa SP Daniel Ndamgilire yeye alieleza kuwa  linatakiwa  jopo la madaktari watano watakaowafanyia uchunguzi wafungwa   ili kubaini wale wanaostahili kupata msamaha jambo ambalo amesema linachangamoto kubwa katika kulitekeleza.  

“ Na mimi nichangie kidogo katika kipengele hiki cha msamaha wa Rais,  kunatakiwa uwepo  wa jopo la madaktari watano, kwa mfano anatakiwa awepo  daktari wa kuwapima wazee, daktari wa watoto, daktari wa wamama wajawazito, na wengineo, hii ni changamoto kubwa kwetu kuwapata madaktari wote hao kwa wakati mmoja, tunaomba hili nalo liangaliwe” akasema  SP Ndamgilire

Katika hatua nyingine  Mkoa wa Rukwa  umetoa mapendekezo kadhaa yatakayosaidia kuboresha utoaji  haki katika Mkoa huo.

Baadhi ya mapendekezo hayo ni   kupewa kipaumbela  kwa  ujenzi wa gereza na mahabusu ya watoto    wakati wa  ujenzi wa miundombinu ya vyombo vya kutoa haki.

“Mkoa wetu katika ujenzi wa miundombinu ya vyombo vya utoaji haki unapendekeza gereza na mahabusu ya watoto ipewe kipaumbele wakati ya ujenzi huo ili kuwasaidia na kuwaepusha watoto wanaokinzana na sheria wasipelekwe magereza ya watu wakubwa” imesema Taarifa ya Mkoa iliyosomwa na Wakili Frida Hava.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uwepo wa gereza na mahabusu ya watoto siyo tu kutawaepusha watoto hao  kujinfuza mbinu zaidi za kufanya uhalifu lakini pia kutawaepusha kufanyiwa vitendo vya kikatili.

Pendekezo hilo la  kuwapo kwa  gereza na mahabusu za watato liliungwa mkono pia  na Mama Varelia  ambaye ni mmoja wa waratibu wa  Kamati  za ulinzi wa wanawake na watoto (MTAKUWA) alisema kutowekuwapo kwa gereza na mahabusu ya watoto mkoani humo  kunawaweka watoto katika mazingira hatarishi.

“Hata sasa hivi ukiendea pale  gerezani utakuta watoto wamewekwa  koridoni kwa sababu hawawezi kuchangwa na wafungwa wengine, wanaishi katika mazingira magumu sana, nisisitize na mimi  ujengi wa gereza na mahabusu ya watoto katika mkoa wetu  upewe kipaumbele,

Wakati huo huo wadau hao wa Hakijinai katika Mkoa wa Rukwa wametoa  pendekezo  kwa Serikali  la    marekebisho ya Sheria zinazochelesha mtuhumumiwa kupata haki yake yafanyike mapema.

Mfano wa Sheria wanayoshauri ifanyiwe marekebisho ya mapema ni  Sheria inayomtaka binti aliyepata ujauzito kusubiri hadi  ajifungue ndipo vinasaba vya mtoto (  DNA) viende kulinganishwa na mtuhumiwa.

Wamesema Sheria hii inaleta mkanganyiko ambao ni pamoja na watuhumiwa na mashahidi kutopatikana tena na au tatizo hili kumalizwa kimila au kifamilia jambo ambalo wanasema  linachangia kumyima  haki Binti.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...