Na Muhidin Amri,Ruvuma
JUMLA ya askari 106 kati 110 wa wanyamapori wa vijiji(VGS)kutoka
jumuiya za wanyamapori nchini, wamehitimu mafunzo ya kozi maalum katika
chuo cha mafunzo ya uhifadhi wa maliasili kwa jamii Likuyu Sekamaganga
wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Mkuu wa chuo hicho Jane Nyau amesema,mafunzo hayo ni mkakati wa Serikali
kupitia wizara ya maliasili na utalii kuwajengea uwezo na kuwapa mbinu
askari hao wa vijiji kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu
kwa jamii zinazoishi kando kando ya maeneo yaliyohifadhiwa.
Nyau alitaja jumuiya wanazotoka wanafunzi hao hao ni hifadhi ya msitu
wa Engoserosambu wilaya ya Ngorongoro ni 6 , na 100 wanatoka jumuiya za
Mbarang’andu,Kimbanda na Kisungule zilizopo wilaya ya Namtumbo na
jumuiya ya Nalika na Chingolo iliyopo katika wilaya ya Tunduru kwa
ufadhili wa Shirika la Word Wide Fund For Nature(WWF).
Hata hivyo amesema, wanafunzi wanne waligomea mafunzo na kuondoka
chuoni ambao ni Jafari Abdala,Mohamed Mchamedi wa jumuiya ya
Chingoli,Swalehe Mbalale wa jumuiya ya Nalika na Milkion Ponera wa
jumuiya ya Kimbanda.
Amesema, chuo hicho ni mojawapo ya vyuo vya Serikali chini ya Wizara ya
maliasili na utali chenye wajibu wa kutekeleza mkakati huo kwa kuijengea
jamii uwezo kwa njia ya mafunzo ili iweze kukabiliana na wanyamapori
wakali na waharibifu kwa lengo la kupunguza migogoro kati ya binadamu na
wanyamapori.
Mkuu huyo wa chuo amesema, ni ukweli usiopingika kuwa,kwa sasa idadi ya
watu nchini imeongezeka na ongezeko hilo linakwenda sambamba na
shughuli za kibinadamu kama kilimo,ufugaji na nyinginezo hali
inayopelekea mwingiliano kati ya shughuli za binadamu na rasilimali za
maliasili.
Alibainisha kuwa, kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu kumepelekea
kukithiri kwa uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji miti,kuziba kwa
shoroba, maeneo mtawanyiko wa wanyamapori,uharibifu wa vyanzo vya maji
na athari nyingine.
Amesema, matumaini ya serikali chini ya wizara ya maliasili na utalii
wahitimu hao watakuwa mabalozi na walimu wazuri kwa jamii na kupeleka
elimu hiyo kwa wananchi wa maeneo yao ili nao waweze kunufaika.
Aidha,amewashauri wananchi hasa wanaoishi kando kando ya maeneo ya
hifadhi, kuanza kulima mazao ambayo hayapendwi kuliwa na wanyamapori
kama Tembo,ikiwemo ufuta,alizeti na kupanda pilipili kuzunguka mashamba
yao kama njia mbadala ya kuepuka kuvamiwa na wanyama hao katika maeneo
yao.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Alkwin Ndimbo
amewaasa wahitimu hao kutambua kwamba, kazi ya uhifadhi inahitaji
uzalendo,uadilifu na uaminifu katika ulinzi wa rasilimali za nchi yetu.
Hivyo amewataka kwenda kusimamia vyema tunu na rasilimali za nchi, na
kujiepush na tamaa wakati wote wa majukumu yao ya ulinzi ili kuleta tija
kwa jamii na nchi kwa jumla.
Amesisitiza, suala la uzalendo na uvumilifu kwani ndiyo sehemu wajibu
katika kazi za kila siku na ni sehemu ya kiapo chao tofauti na
watumishi wengine wa umma.
Amewaasa kwenda kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia sheria za
uhifadhi na kuonyesha nidhamu ya hali ya juu kwa jamii inayowazunguka
badala ya kutumia mafunzo waliyopata kunyanyasa wananchi wengine hasa
pale zinapofanyika operesheni za kuwaondoa wavamizi kwenye misitu na
rasilimali mbalimbali.
Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu Masoud Nyoni amesema, katika
mafunzo hayo wamepata elimu stahiki juu ya uhifadhi na matumizi ya
endelevu ya maliasili vijijini kwa maendeleo endelevu.
Amesema,elimu hiyo imegusa nyanja mbalimbali za uhifadhi wa maliasili
kupitia masomo tofauti kama sheria za uhifadhi,utambuzi wa wanyamapori
na matumizi ya silaha hifadhini.
Kwa mujibu wa Nyoni,mafunzo mengine ni matumizi ya GPS na ramani,huduma
ya kwanza,maadili katika uhifadhi,ukakamavu,haki za binadamu,mbinu za
doria,intelejensia,upelelezi,upekuzi na ukamataji majangili.
Ameiomba Serikali kuboresha mazingira ya mafunzo kwa wanafunzi wa chuo
kama upungufu wa mabweni,vitendea kazi kama
silaha,fedha,mahema,GPS,radio call, na viona mbali.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya kozi maalum namba 17/2021 ya askari wanyamapori wa vijiji(VGS)katika chuo cha Mafunzo ya uhifadhi wa maliasili kwa jamii(CBCTC)Likuyu Sekamaganga wilayani Namtumbo, wakimsikiliza jana mwakilishi wa Mkuu wa wilaya hiyo Alkwin Ndimbo(hayupo pichani) wakati wa kufunga mafunzo hayo kwa askari 106 wa wanyamapori wa vijiji.
Picha zote na Muhidin Amri
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...