Na Godwin Myovela, Singida.


MKUU wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge ameagiza Halmashauri zote mkoani hapa kuanza mchakato wa kutenga maeneo ya mashamba makubwa kama ajenda mahususi ya kufanikisha ongezeko la uzalishaji wa zao la alizeti kwa wawekezaji.

Dk. Mahenge aliagiza hayo aliposhiriki na kuhutubia Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani hapa jana, ambalo lilikutana kujadili majibu ya Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Juni 30, 2020.

Agizo hilo limelenga kupunguza hali halisi iliyopo ya uhaba wa uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula, ambapo kiwango cha mafuta hayo kinachozalishwa nchini kwa sasa ni Tani 150,000 pekee, ikilinganishwa na kiwango kikubwa cha takribani Tani 300,000 ambazo huagizwa kutoka nje ya nchi ili kutosheleza mahitaji.

"Tutakuwa na wawekezaji wakubwa hapa Singida watakaohitaji kuanzia ekari 500 hadi 1000, hivyo tunahitaji mashamba makubwa ili tuongeze wigo mpana wa uzalishaji na tija ya zao hili," alisisitiza Dk. Mahenge.

Alisema kwa sasa viwanda vingi vya ukamuaji mafuta ya alizeti vilivyopo mkoani Singida vinafanya kazi chini ya uwezo, yaani vinazalisha kwa miezi 3 pekee kwa mwaka kisha vinazimwa kwa miezi 9 iliyobaki kutokana na uhaba wa malighafi.

Hata hivyo, Dk. Mahenge alihamasisha kila mwana-Singida na yeyote anayehitaji kuwekeza kwenye alizeti ndani ya mkoa huo milango ipo wazi, na atapewa kila aina ya ushirikiano katika kufanikisha azma yake hiyo.

Alisema Mkoa huo una hali ya hewa rafiki, na kutokana na jiografia yake ndio kiini hasa cha ustawi sahihi wa zao hilo, huku akisisitiza upana wa soko lake kwamba mkulima haitaji kwenda nje ya nchi kutafuta soko kutokana na uhitaji mkubwa wa bidhaa hiyo uliopo nchini.

"Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kulivalia njuga suala la alizeti na tayari imeteua mikoa mitatu ya Singida, Dodoma na Simiyu kwa ajili ya kuelekeza nguvu kuhakikisha zao hili linaleta tija," alisema Dk. Mahenge .

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa mkoa alipongeza juhudi kubwa inayofanywa na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa kuwa waaminifu kwenye eneo la ukusanyaji wa mapato, sambamba na kutumia vizuri kwa mujibu wa sheria za matumizi ya fedha za Serikali.

"Nilipofika Singida na kupewa taarifa za maendeleo ya mkoa na kufungua baadhi ya vitabu nikaona Ikungi mko vizuri kwenye eneo hili, kwa sasa mmevuka malengo kwa kukusanya asilimia 82 mkizidisha ile 80 ya lengo. Na nambiwa hapa kwa miaka saba mfululizo mmekuwa mkipewa hati safi...hongereni" alisema Dk. Mahenge.

Katika hilo aliwataka kuongeza jitihada hizo mara mbili zaidi ili kuifanya halmashauri hiyo kuwa namba moja kitaifa, na hatimaye kuleta chachu ya mageuzi ya kiuchumi kwa wana-Ikungi na Singida kwa ujumla.

Aidha, alitoa wito kwa Halmashauri zote za Mkoa kusimamia vyanzo vyote vya mapato ipasavyo ili kuinua mapato, huku akisisitiza kwamba kila chanzo kilichopo kiainishwe na kuhakikisha kinachangia asilimia 100 kwa usimamizi wake.

"Na katika hili nasisitiza sana ili tufanikiwe ni lazima tukubali mabadiliko na mkubali kubadilika tushirikiane kama timu moja ili wananchi wetu wapate maendeleo," alisema.

Dk. Mahenge.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga alimhakikishia Mkuu wa mkoa kwamba watampa kila aina ya ushirikiano, huku akisisitiza utayari wao wa kutoa mashamba makubwa kulingana na mahitaji ya uwekezaji katika kuunga mkono juhudi zilizopo kwenye uzalishaji wa zao la alizeti.

Kuhusu ajenda ya hoja za ukaguzi, Mkaguzi wa Ndani Mkoa wa Singida, Naomi Kalinga aliipongeza Ikungi kwa kufanikiwa kufanyia kazi vizuri hoja za ukaguzi kwa kuzipunguza kutoka 71 hadi 26, jambo linalothibitisha kuwa kuna kazi kubwa imefanyika.

Aidha, Kalinga aliwataka kutobweteka na badala yake waendelee kuwa waaminifu na kuchapa kazi bila ya kuruhusu hoja zilizofungwa kujirudia, ili kuifanya Ikungi kuwa mahali salama pa kufanyia kazi.

Mkaguzi Mkuu Mkoa (CAG) Nkanyila Makawa, akikazia hilo aliwasihi watumishi na watendaji wote wa mkoa kuendelea kufuata sheria za matumizi ya fedha za Serikali ili kuepuka hoja zisizo za lazima zinazoweza kuibuliwa na jicho la pili ambalo liko nyuma ya kila mtumishi. Mkuu wa Mkoa Singida, Dk. Binilith Mahenge akitoa maagizo na mwelekeo wa Singida Mpya kwenye mageuzi ya kiuchumi katika muktadha wa ushirikiano, uwajibikaji, kukusanya ipasavyo na kuongeza vyanzo vipya vya mapato, maboresho ya miundombinu, afya, elimu, kuinua tija kwenye kilimo, umuhimu wa Bima' ya Afya CHF wakati akihutubia Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi lililo keti jana kujadili Majibu ya Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha ulioishia Juni 30, 2020. alipohutubia mkutano huo.

Maafisa Wakaguzi wa Ndani na Nje wakifuatilia mkutano huo.

Madiwani wakishiriki kikamilifu kwenye ajenda ya Mkutano huo Maalum.
.Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Revocatus Mohabe, akizungumza kwenye mkutano huo.Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu kwa niaba ya Wabunge, Madiwani na Watendaji wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi akimkaribisha rasmi wilayani hapo Mkuu wa Mkoa Dk. Mahenge na Katibu Tawala Mkoa Doroth Mwaluko kwa kumkabidhi zawadi ya Mbuzi kama ishara ya upendo na mshikamano.


Mkuu wa Mkoa Singida, Dk. Binilith Mahenge akipokelewa na Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally Mwanga, alipowasili wilayani hapo jana kuungana na Madiwani hao kushiriki Mkutano Maalum wa Baraza hilo uliojikita kujadili Majibu ya Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha ulioishia Juni 30, 2020.

Mkaguzi Mkuu Mkoa Singida Nkanyila Makawa, akizungumza kwenye mkutano huo

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...