NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
KATIKA kuhakikisha huduma za tathmini za ulemavu uliotokana na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi zinawafikia walengwa huko waliko kwa, haraka na kwa wakati, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umezidi kuongeza mtandao wa madaktari na watoa huduma za afya kwa kuwajengea uwezo wa kuwapatia mafunzo ya kufanya kazi hiyo.
Akizungumza mjini Morogoro wiki hii wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kufanya tahmini za ulemavu uliotokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi madaktari na watoa huduma za afya 93 kutoka mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam na Morogoro, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma alisema baada ya mafunzo hayo idadi ya madaktari na watoa huduma za afya wenye ujuzi wa kufanya tathmini itaongezeka kutoka 1,085 iliyokuwepo na kufikia 1, 178 nchi nzima.
“Lengo ni kuongeza mtandao wa wataalamu wenye ujuzi kwenye hospitali za umma na binafsi nchini kote ili kuondoa changamoto ya kuwafikia walengwa kwa muda na kwa haraka na hivyo kutoa tathmini stahiki na kwa wakati.” Alisema Dkt. Mduma
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini, WCF, Dkt. Abdulsalaam Omary akizunguzma wakati wa kufunga mafunzo hayo Ijumaa Juni 18, 2021 alisema mafunzo hayo yaliendeshwa na wataalamu kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa kushirikiana na wataalamu wabobezi wa masuala ya tathmini za ulemavu uliotokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
“Tuna hakika watakuwa wamefaidika sana na utaalamu huu ambao ni mpya kwao na kwetu sisi kama Mfuko tumedhamiria kwa dhati kuhakikisha huduma zetu zinafika kila pembe ya nchi yetu na hivyo kurahisisha utoaji wa huduma kwa wafanyakazi watakaokuwa wamepatwa na matatizo hayo kazini.” Alisema Dkt. Omary.
Baadhi ya madaktari walioshiriki mafunzo hayo walieleza jinsi yalivyowawezesha kuwapa utaalamu na uwelewa kuhusu masuala ya Fidia na jinsi wanavyotakiwa kufanya tathmini kwa mtu aliyepata ulemavu uliotokana na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi kwa weledi.
“Nitakuwa balozi mzuri kwa wataalamu wenzangu kwenye kituo changu cha kazi kwani nimeelewa kuwa tathmini za ulemavu uliotokana na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi, itafanyika tu pale mgonjwa atakapokuwa amepona na kwamba hakuna tena tatizo litakaloendelea baada ya matibabu (Maximum Medical Improvement-MMI) na sio kabla.”Alisema Dkt. Mohammed Khalifa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Newala mkoani Mtwara.
Naye Dkt. Noel Saitoti kutoka Hospitali ya Ikenywa jijini Dar es Salaam alisema kabla ya kufika kwenye mafunzo hayo licha ya kuifahamu WCF kama ni Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi mafunzo yamesaidia kujenga uelewa zaidi wa majukumu ya Mfuko kuwa ni zaidi ya kulipa fidia.
“Baada ya mafunzo haya nimejifunza kuwa Mfuko pia unatoa mafao mbalimbali kama vile Fao la matibabu, na ikitokea mfanyakazi amefariki kutokana na kazi basi wale wategemezi wanapata fidia.” Alisema Dkt. Saitoti.
Akieleza zaidi kuhusu manufaa aliyoyapata baada ya mafunzo, Dkt. Saitoti alisema mafunzo aliyoyapata hakuwahi kujifunza hapo kabla, kwa hiyo ameongeza utaalamu kwenye eneo maalum na kuupongeza Mfuko kwa kuandaa mafunzo hayo na kuomba mafunzo yaendelee ili kuweza kuwapata wataalamu wengi zaidi wenye uwezo wa kufanya tathmini.
“Nawaasa watoa huduma wenzangu (madaktari) tunatakiwa kuwa katikati yaani tutende haki, kama mtu anastahili kupata mafao tufanye tathmini kama tulivyojifunza ili kuusaidia Mfuko kutenda haki, kwa sababu mtu anayeonana na yule mgonjwa ni sisi madaktari kwa hiyo maelezo ya kina kuhusu tatizo lililompata muathirika ni sisi madaktari ndio tunaolibeba kwa hiyo tunaowajibu mkubwa wa kimaadili kuona tatizo lilipo na kuwasilisha kwa Mfuko ili aweze kupata haki inayostahili.” Alisema Dkt. Noel Saitoti kutoka Hospitali ya Ekenywa ya jijini Dar es Salaam.
Aidha Dkt. Husna Lusasi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, yeye alisema wilaya ya Mkuranga ina viwanda vingi sana na kumekuwepo na idadi kubwa ya vijana wanaoumia kutokana na kazi hivyo pamoja na Mfuko kuwahudumia kwa kuwapatia fao la matibabu na wakati mwingine fidia, kuna haja ya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha wenye viwanda wanatoa vifaa vya kujikinga kwa wafanyakazi wao na wawe wanavitumia.
“Tuwasaide vijana hawa kwa kufanya assessment ya mara kwa mara ili tuwanusuru na ajali, taifa linahitaji nguvu kazi hii kwa ajili ya maendeleo.” Alisema Dkt. Lusasi.
Mafunzo haya yametupa elimu kuu mbili mosi ni kwa waajiri kutambua watumishi wao wanatakiwa kuwa kwenye mazingira sahihi na salama ya kazi mfano kwa kutoa vitendea kazi maalum kwa ajili ya kuwalinda wakiwa kazini na pili ikibidi mfanyakazi kaumia au kuugua kutokana na kazi basi mfuko utatoa matibabu sahihi ili waweze kurudi kazini mapema iwezekanavyo.
Akifunga mafunzo hayo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Ukio Kusirye aliwataka madaktari hao kuitumia elimu iliyotolewa katika mafunzo hayo ili kuwawezesha kufanya tathmini ya ulemavu (Impairment Assessment) kwa ufanisi na uweledi wa hali ya juu na hatimaye kuwasaidia wagonjwa na kusaidia Mfuko utimize lengo la kutoa fidia stahiki na kwa wakati.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...