Charles James, Michuzi TV

SERIKALI nchini imepokea kiasi cha Dola Milioni 425 sawa na Sh Bilioni 980 kutoka Benki ya Dunia ili kuimarisha na kuboresha  miundombinu ya elimu ya juu.

Kiasi hicho cha fedha kimeidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia Mei 27 mwaka huu ambapo kitasaidia kuongeza udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kwa asilimia 30 na kuongeza walimu takribani 600.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako leo jijini Dodoma wakati akizungumza na wandishi wa habari baada ya kumaliza mazungumzo yake na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Afrika ambapo kikao hiko kimehudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Ummy Mwalimu.

Prof Ndalichako amesema ujio huo wa Mkurugenzi huyo wa Benki ya Dunia Ukanda wa Afrika ulikua kuangalia namna ambavyo Serikali ya Tanzania imekua ikitekeleza fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya elimu nchini.

Amesema Benki ya Dunia imekua ikiipatia Tanzania kiasi kikubwa cha fedha na asilimia 30 ya fedha hizo zinazotolewa zimekua zikielekeezwa na kutekelezeka kwenye miradi ya elimu.

" Niwashukuru sana ndugu zetu wa Benki ya Dunia, wamekua wakichangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa elimu nchini, kupitia wao tumeweza kujenga Shule mpya, mabwalo, matundu ya vyoo na kukarabati shule kongwe kupitia mradi wa EP4R.

Lakini pia Benki ya Dunia walitupatia kiasi cha Sh Trilioni 1.1 kwa ajili ya kusaidia kuimarisha elimu Sekondari ambapo Shule 26 zinatarajiwa kujengwa Nchi nzima kila Mkoa ukipata Shule yake ili kusaidia kupunguza tatizo la wanafunzi kukosa Shule na kutembea umbali mrefu kwenda Shule," Amesema Prof Ndalichako.

Amesema kwa sasa wanaendelea na mazungumzo ya kupata mradi wa kuimarisha elimu msingi na haswa kwenye eneo la teknolojia lengo likiwa ni kuzalisha kundi kubwa la vijana wenye uelewa mpana wa sayansi na teknolojia kuanzia ngazi za chini.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Ummy Mwalimu ameahidi wao kama watekelezaji wa elimu nchini watahakikisha fedha hizo zinatumika kama zilivyoelekezwa.

Amesema Serikali imekua ikitoa elimu bila malipo kwa wanafunzi wake kwa ngazi ya msingi hadi kidato cha nne ambapo pia wamekua wakichagua hata wale walioacha Shule na kurejea baadaye kusoma.

" Mwaka huu tumechagua zaidi ya wanafunzi 200 ambao waliacha Shule na kisha kurejea kusoma kupitia Taasisi ya Watu Wazima Tanzania (TEWW), lengo letu ni kuhakikisha kila mwanafunzi anapata haki ya kusoma," Amesema Waziri Ummy.

Nae Mkurugenzi huyo wa Benki Kuu, Dk Taufila Nyamadzabo ameihakikishia serikali kuwa wataendelea kushirikiana kwa karibu kuhakikishaTanzania inafikia lengo la kuwa na shida nyingi na kuepuka changamoto za wanafunzi kukosa Shule lakini pia kuboresha miundombinu na kuwa na walimu wengi zaidi.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma leo, baada ya kumaliza mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Bara la Afrika.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako (Kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika,  Dk Taufila Nyamadzabo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Ummy Mwalimu (kulia) baada ya kumaliza mazungumzo yao jijini Dodoma leo.

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Ummy Mwalimu akizungumza baada ya kumaliza kikao Cha pamoja na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Bara la Afrika, Dk Taufila Nyamadzabo leo jijini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...