Na Chalila Kibuda, Michuzi TV
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesema kuwa litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi kwa kutoa huduma za usafirishaji wa shehena ndani ya nchi na nje ya nchi.
Akizungumza na katika mkutano wa wadau wa usafirishaji wa shehena nje ya nchi, Mkurugenzi Udhibibiti Huduma za Bandari na Usafiri wa Meli wa TASAC Bw. Deogratius Mukasa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, amesema kuwa kuna umuhimu wa kuwajengea uwezo wasafirishaji wa shehena kwa kutoa elimu ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.
Amesema kuwa, elimu hiyo ni endelelevu kwa wadau kwani baada ya kutolewa jijini Dar es Salaam itatolewa pia katika mikoa ya Tanga na Arusha ili kuweza kuwapa elimu mawakala wa usafirishaji wa shehena za kwenda nje ya nchi na zile za kuingia nchini.
Mukasa amesema TASAC inawasikiliza sana wadau, na hata inapounda kanuni huwashirikisha wadau ili kupata maoni yao.
Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu Shirika la Wasafirishaji wa Shehena ISCOS kutoka Kenya Bw. Daniel Kiangi amesema kuwa, Shirika hilo lina wanachama wanne ambao ni Tanzania, Kenya Uganda na Zambia. Vilevile wamekuwa na ushirikiano wa karibu na wadau wa usafirishaji shehena kwa njia ya maji ikiwemo TASAC, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari(TPA), Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), n.k.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Baraza la Wasafirishaji wa Shehena kwa njia ya Maji nchini Tanzania, Bw. Ashraf Khan amesema kuwa wasafirishaji wa mizigo kwa njia ya maji wanahitaji kuwa na elimu na sio kufanya biashara hiyo kiholela ili kuepuka changamoto mbalimbali ambazo wanaweza kukutana nazo.
Amesema kuwa tangu kuundwa kwa TASAC, changamoto mbalimbali zimeweza kutatuliwa kwa kuwa Baraza hili kwa kushirikiana na TASAC limeweza kuwasaidia wanachama wake kupunguza gharama kutokana na kujua taratibu zilizowekwa kwa wasafirishaji ndani na nje ya nchi, pamoja na kufanya kazi kwa weledi pande zote mbili za mdau na mdhibiti.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...