KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Daniel Godfrey Chongolo amewaagiza wabunge wote wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wanaotokana na CCM kufanya ziara katika majimbo yao yote kueleza yaliyopitishwa na Bunge la bajeti na kupokea changamoto zingine wanazokabiliana nazo kwa kuwashirikisha madiwani na wananchi kwa ujumla.

Ametoa maelekezo hayo katika kikao cha ndani cha viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali siku ya kwanza ya ziara ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya  CCM Taifa katika mji mdogo wa Laela,  Sumbawanga vijijini leo tarehe 7 Julai,  2021  alipokuwa akipokea taarifa ya kazi ya Chama na serikali mkoa wa Rukwa.

"Nawapongeza wabunge niliowakuta kwenye mikoa yao baada ya Bunge la bajeti, sasa Kazi yenu wabunge ni kupita kwenye jimbo lote kuwaeleza wananchi yaliyopitishwa kwenye bajeti, yanayowagusa. Pia wabunge kaeni kwanza na madiwani muwasikilize ndipo mpange ratiba ya ziara zenu kwenda kwa wananchi." Alisema Chongolo.

Chongolo amesema baada ya kuona wabunge wamelalamika sana kuhusu bajeti ndogo ya TARURA , Mhe Rais baada ya kusikia kilio Cha wabunge ametoa shilingi milioni mia tano kwa kila jimbo kwa ajili ya kuimarisha barabara za vijijini na mijini zinazohudumiwa na wakala wa barabara mjini na vijijini TARURA.

"Natoa maagizo kwa wabunge wote nchini ambao ni zao la CCM kwa sasa wamemaliza bunge la bajeti, wabunge wote waende kwenye majimbo yao wakawaeleze wananchi yaliyomo kwenye bajeti na hususani yanayowagusa ili waelewe nini serikali inataka kufanya kwao". Alisema Chongolo

Aidha, Chongolo amewataka viongozi wa CCM ngazi za mikoa, wilaya na kata kwenda kwenye mashina na matawi kufanya mikutano ya kuwasikiliza na kutoa muongozo wa CCM katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ili kubaini changamoto na kuzishughulikia kwa wakati.

Amesema Mara ya mwisho alipofika Rukwa katika ziara za Viongozi  bonde la ziwa Rukwa kulikuwepo na changamoto ya barabara lakini pia kulikuwepo na  Mti mmoja kule Wampembe umebanduliwa magome na watu ukianza kunyauka na hivi sasa nimeambiwa ule Mti umekauka na kuanguka na sasa hakuna Mti kule, hali kadhalika ndivyo ilivyo na kwa wananchi wanaolalamika wasiposikilizwa na kutatuliwa kero zao kwa wakati huongeza changamoto na kusababisha hasara kubwa.

Kuelekea uchaguzi mkuu wa ndani ya Chama hicho mwaka 2022, Chongolo alisema ni marufuku kupanga safu za uongozi kwa lengo la kujipatia nafasi, hilo ni tatizo kwetu na kwa uhai wa Chama Cha Mapinduzi.

Niwasisitize, kwenye Chama chetu kumekuwa na tabia ya safu, kupangana safu ili wa chini amchague wa juu. Huo sio utaratibu wa chama chetu, utaratibu ni kufuata katiba, kanuni na miongozo ya chama katika kuwapata viongozi wenye sifa stahiki na wanaotakiwa na wanachama. Kupanga safu ni tabia ya hovyo na watu hao wana ajenda nyingine binafsi sio ya kukiimarisha chama chetu" amesema Chongolo

Kuhusu ziara ya sekretarieti ya CCM Taifa alisema wamemua kufanya ziara hiyo ili kila mkoa upate ujumbe kwa kutumia gharama ndogo kwani wakifika kwenye mkoa wanagawana wilaya na kila mjumbe wa sekretarieti ya CCM Taifa anaenda kwenye wilaya moja kufikisha ujumbe na hivyo wanatumia muda mfupi gharama ndogo kuwafikia wananchi wengi.

"CCM lazima tuwe wabunifu katika kufikisha ujumbe na kufanikisha mambo ya wananchi kwa ubora na kwa gharama ndogo kama tunavyofanya sasa" alisema Chongolo.

Katika hatua nyingine, Chongolo ameagiza kamati za siasa za kata kuwapima madiwani katika kutimiza wajibu wao na za wilaya kuwapima wabunge na kamati ya siasa mkoa kufanya hivyo hivyo, ili kuwa na taarifa sahihi za kila kiongozi wa CCM aliyeko kwenye nafasi za dola kuhusu utendaji wake na namna anavyotumia muda wake kushughulika na changamoto za watu wake pamoja na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Alisema lengo ni kuweka uwajibikaji kwa tuliowapa dhamana ya kukiwakilisha Chama kwa wananchi  wakiwemo wabunge na madiwani.

Ziara hii inajumuisha wajumbe wa Sekretarieti ya Halmshauri Kuu ya CCM Taifa wakiwemo Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Ndugu Shaka Hamdu Shaka, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Ndugu Ngemela Lubinga na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Ndugu Kennan Kihongosi ambapo watatembelea mikoa ya Rukwa, Songwe na Mbeya.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...