**************************

Adeladius Makwega

Chamwino-WHUSM

JULAI 25, 2021 ni siku itakayokumbukwa milele kwa wapenzi wa muziki nchini Tanzania, kwani ni siku ambayo ndugu yetu, rafiki yetu, kaka yetu, baba yetu na mzee wetu Waziri Ally Seifu (Waziri Njenje ) amezikwa huku kwao Pongwe, Mkoani Tanga.

Walio wengi wanamfahamu Waziri Ally kama Kiongozi tu wa-The Kilimanjaro Band(Wana Njenje) bila ya kufahamu kuwa gwiji huyu aliwahi kufanya kazi kubwa sana za muziki wa dansi akiwa na bendi kongwe za wakati huo nchini Tanzania.

Kumuenzi mwanamuziki huyu, leo hii nakata mbuga hadi mwaka 1979 na nakukuta na na wimbo wa Sogea Karibu ulioimbwa na wana Juwata Jazz Band (Wana J.J.B) ambayo ilikuwa bendi inayomilikiwa na Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania(JUWATA).

Akiwa na wana J.J.B Waziri Ally alifanya kazi kubwa sana kuliokoa jahazi la Juwata Jazz Band katika wimbo huo vinginevyo wimbo huo usingerekodiwa au kuwa kama ulivyo leo hii.

Nisimalize uhondo ebu soma mashairi ya wimbo huo:

Sogea karibu, Nikueleze

Usije shangaa, Imekuwaje



Upate fahamu sasa, Nakueleza

Ndoa yetu (changa), Imevunjika

Nilikupeleka kwa wakwe zako, Ukaonane na ndugu zangu ehhh

Hata mama yako alifurahi sana, Ndugu zangu walikupenda sana

Lengo letu dada ni kuoana, Kama tukichunga heshima yetu ehhh.



Ehh Bwana Waziri Waziri(Kinanda kinachezwa)



Nilikupeleka kwa wakwe zako, Ukaonane na ndugu zangu ehhh

Hata mama yako alifurahi sana, Ndugu zangu walikupenda sana

Lengo letu dada ni kuoana, Kama tukichunga heshima yetu ehhh.

Sasa nasikia, Umefanya visa vingi ee,

Hata mama yangu, Umthamieee

Ikiwa mambo yenyewe ni hivyo, Mbona mazito

Dada mimi nimeshindwa, Siwezi kukuoa tena.



Nilikueleza toka zamani, Kitu kimoja,

Uchunge heshima kwa wakwe zako, Ukapuuza



Sasa nasikia, Umefanya visa vingi ee,

Hata mama yangu, Umthamieee



Maji yakishamwagika, Hayazoleki

Kilichobakia sasa ni majuto

Nenda kwenu kwa salama

Sasa nasikia, Umefanya visa vingi ee,

Hata mama yangu, Umthamieee



Ponda

Mashairi ya wimbo huu yametungwa na Kakere Besela mnamo mwaka 1979 ndani ya albam ya Mpenzi Zarina yenye nyimbo nane nazo ni Mpenzi Zarina, Mwana Acha Wizi, Uzuri si Shani, Epuka Tabia Mbaya, Sogea Karibu, Vijana Tujitokeze, Selemani, na Talaka. Sogea Karibu uliimbwa na Hassan Bitchuka na unapousikiliza utabaini kuwa kinanda kimepigwa kwa ustadi mkubwa mno, hiyo ni kazi yake Waziri Ally.

“Sababu kubwa za kupigwa kinanda sehemu kubwa ya wimbo huu ni kuwa wapigaji wa vyombo vya upepo (Tarumbeta na Sax) waligoma kwa sababu wakidai kuwa wimbo huo ni mbaya mara baada ya mashairi kutungwa na wakati wa mazoezi ndipo mzozo huo uliibuka.” Anasema Masoud Masoud Mtangazaji Mkongwe wa TBC ambaye pia ni mdau wa muziki wa dansi nchini.

Masoud Masoud anasema kuwa mgogoro huo ukiwa chini ya uongozi wa mwanamuziki Joseph Lusungu wakaamua kutoshiriki katika kazi hiyo. Cha kushangaza wimbo huo uliporekodiwa Waziri Ally aliziba pengo la waliofanya mgomo huo na Bwana Waziri Ally akakipiga kinanda kwa ustadi mkubwa.

“Sogea Karibu ukawa wimbo maarufu sana kati ya miaka 1970 na 1990 na hilo likawa mshangao mkubwa sana si kwa akina Joseph Lusungu tu bali kwa Watanzania wote na wapenzi wa muziki wa dansi.” Anasema Masoud Masoud.

Waziri Ally ameonyesha ubunifu na umahiri mkubwa hata ukiangalia nyimbo zake na mtindo wake akiwa na Wananjenje utabaini kuwa ilikuwa ni ngumu mtu kusikia muziki wake pahala pengine bali kwa ni Wananjenje tu anasema kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa wa Wizara ya Habari , Utamaduni , Sanaa na MIchezo Ndugu Mfaume Said.

“ Alichokifanya katika wimbo wa Sogea Karibu ni Uzalendo wa Kimuziki maana wengine waligoma kuimba na kurekodi lakini yeye akaamua kuokoa jahazi la muziki lakini pia aliokoa jahazi la Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania (JUWATA) kwani wafanyakzi wanamsemo wao kuwa Solidarity Forever-Mshikamano Daima.” Aliongeza Kaimu Mkurugenzi huyo wa Maendeleo ya Sanaa wa Wizara ya Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo.

Naweka kalamu yangu chini katika makala haya kwa kusema Waziri Ally anawaaga-akisema Pongwe Kwaheri, Tanga Kwaheri, CHAMUDATA Kwaheri, Wapenzi wa muziki wa Tanzania Kwaheri, The Kilimanjaro Band Kwaheri na Watanzania Kwaherini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...