Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) uatarajia kutoa kompyuta 800 kwa shule mbalimbali nchini ikiwa ni mkakati wa kupeleka ujuzi wa TEHAMA kwa vijana Watanzania hasa katika ulimwingu huu wa digitali na teknonolojia ya mawasiliano.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Justina Mashiba amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la mfuko huo lililoko katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea mkoani Dar es Salaam baada ya kutembelewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk.Faustine Ndugulile.
Amesema wapo katika maonesho hayo kwa lengo la kuwafikisha taarifa Watanzania kwamba kuna taasisi ya Serikali inayopeleka huduma za mawasiliano vijijini na wanafanya jukumu hilo kwa kushirikiana na kampuni za simu ambazo zimepewa leseni na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA)na kuongeza kazi kubwa.
"Tuko hapa mbali ya kueleza shughuli tunazofanya tunapokea changamoto mbalimbali ambazo watanzania wanazipata kuhusiana na huduma za mawasiliano nchini, tuko hapa tumetembelewa na wageni takribani 500 na kati ya hao wageni 63 walikuwa na changamoto ya mawasiliano katika maeneo yao.
"Kwa hiyo tunachukua changamoto hizo na tutaenda kuzifanya kazi kwa kupeleka huduma.Moja ya changamoto tunazoshughulikia ni za simu za mkononi maeneo ya vijijini, hilo ndilo jukumu letu kubwa, kuna watu wanatoka vijiji vya mbali ambapo kuna ugumu wa mawasiliano.
"Lakini kuna maeneo hakuna usikivu wa redio na kama mnavyofahamu nchi yetu ni kubwa tumepakana na nchi karibu nane, kwa hiyo unakuta baadhi ya maeneo wanasikiliza redio za nchi jirani,kwa hiyo changamoto hizo tunazipokea.Lakini mbali ya hapo tunanunua vifaa vya Tehama kwenye mashule, mwaka huu tumenunua kompyuta 800 kwa ajili ya kuzipeleka mashuleni na kila shule itapata itapata kompyuta tano na printa moja.
"Hatukuishia hapo tunapeleka na mtandao wa Intanenti kwa ajili ya kuhakikisha katika shule zetu kuna kuwa na fursa ya kupatikana kwa taarifa,"amesema Mashiba na kusisitiza kote ambako kuna changamoto za mawasiliano wataendelea kuzitatua kwani hilo ni sehemu ya wajibu wao.
Awali Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk.Faustine Ndugulile amesema Serikali kupitia mfuko huo wamefanya kazi kubwa kuhakikisha maeneo ya pembezoni ambayo hayana mvuto wa biashara wanapeleka mawasiliano.
"Sisi kama Serikali tunaamini mawasiliano ni haki ya kila Mtanzania, na hapa ninavyoongea na ninyi asilimia 94 ya Watanzania tumewafikia kwa njia ya mawasiliano.Katika eneo la kijiografia la Tanzania zaidi ya 60 tumeifikia na mawasiliano.
"Kwa hiyo ni hatua kubwa na tunaendelea kujipanga ,na katika zabuni ambayo tumeitangaza hivi karibuni ,sisi tumesikia maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ametutaka kuhakikisha pembezoni mwa nchi yetu ambapo ukifika kule unapokelewa na mawasiliano ya nchi jirani tunakwenda kutatua changamoto hiyo,"amesema.
Amefafanua kwa hiyo wametangaza zabuni maeneo yote ya mipakani ambapo usikivu ulikuwa unapata mawasiliano ya nchi jirani, katika zabuni hiyo tunakwenda kutatua hali hiyo huku akieleza wametekeleza katika halmashauri 10 nchini ambazo mawasiliano yake hayana mawasiliano sasa wamefikisha mawasiliano.
Aidha amesema hawakuishia tu katika kuhakikisha mawasiliano yanafika ,mfuko huo una kazi ya ziada wa usikivu wa redio ndani ya nchi sasa hivi wanataka kujikita kuongeza usikivu wa redio.
Dk.Ndugulile amesema kupitia mfuko wa mawasiliano wameenda mbali zaidi kuhakikisha katika Tanzania ya Tehama na mapinduzi ya kidigitali wanakwenda nayo , hivyo watagawa kompyuta kwenye shule ili kujenga uwezo wa vijana kupata mafunzo ya tehama.
"Kwa hiyo mfuko huu sio kazi ya kujenga minara peke yake inafanya kazi kubwa kuhakikisha mawasiliano yanafika maeneo yote ya nchi yetu na katika awamu hii kama nilivyosema maeneo ya mipakani nadhani yatabaki machache ambayo ukifika unapokelewa na mawasiliano ya nchi jirani,"amesema Dk.Ndugulile.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk.Faustine Ndugulile (kushoto) akikabidhiwa kalenda na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Justina Mashiba baada ya kutembelea banda la mfuko huo kwenye maonesho ya 45 ya biashara ya kimataiya yanayaondelea mkoani Dar es Salaam.Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk.Faustine Ndugulile(kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa mfuko huo hasa katika kufikisha mawasiliano maeneo ya pembezoni mwa nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Justina Mashiba(kulia) akifafanua jambo kwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk.Faustine Ndugulile(kushoto).
Ofisa wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(kushoto) akimhudumia mwananchi aliyefika kwenye banda lao.
Baadhi ya wananchi waliofika katika banda la Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote wakipata maelezo kutoka kwa maofisa wa mfuko huo.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk.Faustine Ndugulile(kushoto) akisisitiza jambo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Justina Mashiba.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...