Charles James, Michuzi TV
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kufanya uchunguzi wake katika Shule ya Sekondari Itiso wilayani Chamwino, Dodoma ili kubaini kama kuna ubadhirifu wa fedha umefanyika kwenye Shule hiyo.
Pia amesema atawasiliana na Mamlaka ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuivunja Bodi ya Shule hiyo kwa kushindwa kusimamia ujenzi wa shule hiyo kwa weledi.
Ndejembi ambaye pia ni Mbunge wa Chamwino ametoa agizo hilo baada ya kufanya ziara kwenye Shule hiyo kukagua ujenzi wa chumba cha maabara, mabweni na madarasa ambapo ameeleza kutoridhishwa na namna ambavyo fedha zimetumika.
Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, Ndejembi amesema kiasi ambacho kilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha maabara ni Sh Milioni 30 lakini cha kushangaza fedha yote imeisha huku maabara ikiwa haijakamilika na wala hairidhishi.
" Ndugu zangu wa Chamwino sijaridhishwa na ujenzi unaoendelea hapa, haiwezekani Milioni 30 iliyotoka hapa Ndio waliyopewa wenzenu wa Kata ya Dabalo lakini wao wamemaliza ujenzi na wamebakiwa na fedha Sh Milioni Nane, hapa fedha imeisha na ujenzi hauridhishi.
Naiagiza TAKUKURU kuja kufanya uchunguzi hapa kwa kuwahoji Bodi ya Shule na watumishi wa Shule hii, hatuwezi kukubali kuona fedha hizi ambazo tumepewa na Rais Samia zinatumika hovyo bila kunufaisha watanzania ambao wamekusudiwa kutatuliwa changamoto zao," Amesema Naibu Waziri Ndejembi.
Ndejembi pia amemuagiza Mhandisi wa Wilaya kufika ofisini kwake siku ya Jumatatu kumpa maelezo ni kwanini alizuia ujenzi wa shule hiyo kufanyika kwa fedha za ndani (force account) na badala yake akaagiza aletwe Mkandarasi ambaye ameshindwa kumaliza kazi kwa ubora.
"Mhandisi wa Wilaya Jumatatu nahitaji aje ofisini kwangu akiwa na majibu ya kueleweka kwanini amezuia ujenzi kufanyika kwa force account, tungetumia fundi wetu wa hapa gharama zingekua ndogo na tungepata majengo yenye ubora.
Lakini pia nimegundua Bodi ya Shule haina ushirikiano na WDC, kwa sababu Bodi imeshindwa kusimamia ujenzi wa vyumba hivi, nitaenda Tamisemi kuomba Bodi hii ivunjwe maana haina manufaa yoyote kwa wananchi wa Itiso," Amesema Ndejembi.
Amesema yeye kama Mbunge hawezi kukubali kuona upotevu wa fedha za umma unafanyika kwenye Jimbo lake huku akitoa onyo kwa watumishi wa umma na wote wanaopewa kazi ya kusimamia miradi ya wananchi kusimamia kwa weledi na uaminifu.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora na Mbunge wa Chamwino Mkoani Dodoma, Deo Ndejembi akiambatana na viongozi wa Kata ya Itiso wilayani Chamwino na wananchi wake akikagua ujenzi wa Sekondari ya Itiso ambapo anatekeleza miradi ya Ujenzi wa Chumba Cha Maabara, Darasa na Mabweni.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi akikagua ujenzi wa chumba cha maabara katika Shule ya Sekondari Itiso wilayani Chamwino ambapo yeye ndie Mbunge wa Jimbo hilo.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Chamwino Mkoani Dodoma, Deo Ndejembi akizungumza na viongozi na wananchi wa Kata ya Itiso alipofika kukagua ujenzi katika Shule ya Sekondari ya Itiso.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...