Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  imetoa zaidi ya shilingi bilioni tatu kwa Taasisi mbalimbali zinazofanya utafiti  katika masuala ya Kilimo, Viwanda, Afya na Mifungo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako leo Julai 3, 2021 wilayani Kibaha wakati alipotembelea na kufanya ukaguzi wa namna fedha shilingi milioni 400 zilizopelekwa katika Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) zilivyotumika.

Profesa Ndalichako amesema fedha hizo zilipelekwa katika Taasisi hiyo kwa lengo la kuiwezesha kupata vifaa muhimu vinavyotumika katika uthibiti ubora wa chanjo zinazozalishwa nchini pamoja na kufadhili mradi unaolenga kupata mbegu kuu ya chanjo ya magonjwa ya Homa ya Mapafu ya Mbuzi.

"Taasisi hii ni kati  ya taasisi zilizopatiwa fedha na Wizara kupitia COSTECH ili kuwezesha kufanya utafiti katika eneo lao la mifugo, ninayo furaha kuona fedha walizopata wamezitumia kununulia vifaa muhimu pamoja na kuwapeleka mafunzo wataalamu wao ili kuongeza ujuzi na weledi katika kazi" amesema Waziri Ndalichako.

Waziri huyo amesema ufadhali huo umesaidia sana katika kuongeza tija katika taasisi hiyo, hivyo Wizara yake itaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya utafiti ambayo inaendana na malengo ya Maendeleo ya Taifa.

Amesema fedha hiyo siyo fedha nyingi katika utafiti lakini imesaidia kwani ni muhimu kama Taifa kuwa na madawa na chanjo zake yenyewe ambazo zinaaminika.

Aidha ameridhishwa na namna Wizara ya Mifugo ilivyoweza kusimamia Taasisi yake katika kuhakikisha fedha ambazo wamepata inatumika kama ilivyokusudiwa na kuleta matunda kwa Taifa.

 Naye Mtendaji Mkuu wa  Wakala ya Maabara ya Veterinari  nchini  Dkt.Stella Bitanyi ameishukuru Wizara ya Elimu kwa ufadhili huo ambao umesaidia Taasisi   yake kuongeza ufanisi katika kuzalisha chanjo na kuongeza kiwango cha uzalishaji ambapo mwanzo walikuwa wakizalisha dose milioni 40 lakini baada ya ufadhili imefikia dose milioni 60.

Batinyi ameendelea kueleza kuwa ufadhili huo pia umewezesha Taasisi hiyo kuzalisha chanjo za kimkakati zinazotumia teknolojia ya cell culture. Hivyo Wizara ya Elimu imekuwa na mchango mkubwa  katika kuboresha sekta ya Mifigo nchini hususan katika kudhibiti magonjwa ya mifugo kupitia chanjo bora zinazoendelea kuzalishwa ambazo hatima yake ni kuwa na mazao mifugo iliyo bora ambayo pia itatoa  mazao bora.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa  COSTECH Dkt. Amos Nungu amesema  kuwa ufadhili unaotolewa kwa ajili ya utafiti unaangalia tafiti ambazo zinaendana na  ajenda za  maendeleo za  Kitaifa. Hivyo utafiti huu pia ni muhimu na unaendana ajenda za maendeleo kupitia Sekta ya Mifugo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akijaribu kutumia moja ya kifaa cha upimaji sampuli ya chanjo bora  katika Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) wakati alipokwenda kukagua vifaa vilivyonunuliwa na fedha zilizotolewa na Wizara hiyo kupitia COSTECH.
Mmoja wa wataalamu wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) akimweleza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako matumizi ya moja ya vifaa vilivyonunuliwa na Wizara ya Elimu kwa ajili ya utafiti

 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari, Dkt Stella Bitanyi wakiangalia moja ya sampuli ya chanjo bora ya mifugo katika Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) alipokwenda kukagua vifaa vilivyonunuliwa na fedha zilizotolewa na Wizara

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...