Charles James, Michuzi TV
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa hatua yake aliyoionesha ya kuitaka Wizara ya Fedha na Mipango kupitia upya tozo za kodi za miamala ya simu.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka leo jijini Dodoma ambapo amesema agizo hilo la Rais Samia ni muendelezo wa hatua zake za kuwatumikia watanzania kwa uzalendo na kuziishi changamoto zao.
Amesema pamoja na kauli hiyo wao kama Chama kinachoongoza dola kinaielekeza Serikali iangalie namna gani ya kufanya mapitio ya sera na sheria ya kodi ili kupunguza malalamiko ambayo yamejitokeza wiki hii juu ya tozo hizo z miamala.
" Wiki hii kumekua na malalamiko kutoka kwa wananchi na kwenye mitandao juu ya tozo hizi za miamala ya simu lakini kama Chama tunamshukuru Rais Samia kwa kudhihirisha hekima yake na uzalendo katika utendaji kwa kuonesha namna anavyoguswa na changamoto za wananchi," Amesema Shaka Hamdu Shaka.
UCHAGUZI KONDE, PEMBA
Akizungumzia matokeo ya uchaguzi mdogo wa Ubunge uliofanyika jana Julai 18 katika Jimbo la Konde Wilaya ya Michewani Kaskazini Pemba, Shaka amewashukuru wananchi wa Jimbo hilo kwa kumchagua mwakilishi wa CCM.
Amesema kwa miaka 15 Jimbo la Konde lilikua ngome ya upinzani hivyo kitendo cha wananchi kumchagua Mbunge wa CCM kwa kura 1796 ni uthibitisho wa Imani yao juu ya chama hicho.
" Tunawashukuru sana wananchi wa Konde kwa Imani waliyotuonesha kwa kumchagua mgombea wetu, Shekha Mpemba Fakhi hii imetokana na Imani yao kwetu na kampeni za kisayansi zilizofanywa na mgombea wetu.
Kama Chama tunawahakikishia wananchi kama ulivyo utamaduni wetu wa kuwasimamia viongozi wetu tutafanya hivyo kwa kulinda maslahi mapana ya wananchi wetu," Amesema Shaka.
Jimbo la Konde limefanya uchaguzi kufuatia kifo cha aliyekua Mbunge wa Jimbo hilo Khatibu Haji na mgombea wa CCM Shekha Fakhi Mpemba kuibuka na ushindi akipata kura 1796 akifuatiwa na mgombea wa ACT Wazalendo, Mohamed S Issa aliyepata kura 1373.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...